Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akisisitiza jambo wakati akizindua Bodi ya wakurugenzi wa Bodi ya Kahawa yenye makao makuu Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro tarehe 28 Juni 2021. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda ameitaka Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Kahawa ambayo ipo chini ya wizara ya kilimo kujiimarisha kiutendaji kwa ajili ya kufanya utafiti ili kuongeza tija ya uzalishaji wa kahawa.
Waziri Mkenda ametoa maelekezo hayo tarehe 29 Juni 2021 wakati akizindua Bodi ya wakurugenzi wa Bodi ya Kahawa Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro.
Waziri Mkenda ameitaka Bodi hiyo kuhakikisha kuwa inaongoza sekta hiyo kwa kuwa na mawazo ya kibiashara ili kuwanufaisha wakulima na kuinufaisha nchi.
“Ninyi nyote mlioteuliwa wasifu wenu ndio muelekeo wetu, mnapaswa kufanya maamuzi mazuri kwani tunachotaka ni wakulima wetu kupata pesa za kukidhi mahitaji yao, mkifanya maamuzi ya kumuumiza mkulima yatakuwa hayatusaidiii” Amekaririwa Waziri Mkenda
Kadhalika Waziri Mkenda ameitaka Bodi hiyo kutathmini wingi wa minada ya kahawa ambayo imegawanywa kwenye kanda kama ina tija kwa maendeleo ya zao la kahawa nchini.
“Mimi sijaja kuwashauri ninyi kwa kuwa ninyi ndio mmeteuliwa pia kwa ajili ya kunishauri mimi lakini hili la minada tazameni muone kama lina akisi matakwa ya biashara ya kahawa” Amekaririwa Prof Mkenda
“Pia hakikisheni tunaimarisha uzalishaji na tija kwenye kahawa ili tuweze kuuza kwa bei nzuri na kuwashinda wengine, kwani namna pekee ya kushindana kwenye bei ni kuongeza tija”
Wajumbe walioteuliwa kuunda Bodi ya Kahawa inayoongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Prof. Aurelia K. N. Kamuzora, ni Enock Chimagu Nyasebwa, Edson M. Rugaimukamu, Shadrack A. Issangya, Gotham Filipo Haule, Tinson Nzunda, Neel Vohora, Nangula H. Mwampamba, na Bahati Ludhabiho Mlwilo.
No comments:
Post a Comment