BREAKING

Thursday 24 June 2021

WADAU WATAKA UWIANO WA KIJINSIA KWENYE USAJILI WA VYOMBO VYA HABARI.





Na Mwandishi Wetu- MAELEZO

Juni 23,2021

Wadau wa kupigania haki za Waandishi wa Habari Wanawake wameishauri Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Idara ya Habari-MAELEZO, kuweka kipengele cha uwiano wa kijinsia kwenye uongozi kuwa ni sehemu ya masharti ya usajili wa vyombo hivyo.

Wadau hao pia wamependekeza kuwepo kwa dawati la jinsia katika Idara ya Habari-MAELEZO litakalosimamia uwiano wa kijinsia kwenye vyombo vya habari na kubainisha kuwa madawati yaliyopo kwenye wizara na taasisi za serikali kutofanya kazi zilizokusudiwa.

Wadau hao wamesema vyombo vingi vya habari havijazingatia uwiano huo hatua inayowanyima haki Waandishi wa kike na wakati mwingine kusababisha ukatili wa kijinsia.

Wameyasema hayo mkoani morogoro katika mkutano wa siku nne wa kupanga mradi wa kuimarisha nafasi ya vyombo vya habari katika kukabiliana na ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto ulioandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Wadau wa kupigania haki za Wanawake na Watoto.

"Tunaiomba Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo kupitia Idara ya Habari-MAELEZO, kuweka kipengele cha uwiano wa kijinsia kuwa ni cha lazima kwenye usajili wa vyombo vya habari, hii itasaidia kuongeza Waandishi wa habari wa kike wengi kwenye uongozi, na tutaondokana na ukatili wa kijinsia kwenye Vyombo hivyo" amesema Bw. John Ambrose kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA.

Nae Mkuu wa Idara ya Jinsia wa Wizara ya Afya Bi Regina Mollel amesema ni muhimu kwa kila chombo cha Habari kuwe na dawati la Jinsia na kuiomba Idara ya Habari-MAELEZO kufuatilia suala hilo.

Mjadala wa Wadau hao kuhusu uwiano uanzie kwenye usajili umeibuka mara baada ya Afisa Habari Mkuu wa Wizara hiyo Kutoka Idara ya Habari-MAELEZO Bi Ingiahedi Mduma kuwasilisha mada kuhusu nafasi ya Wizara katika kukabiliana na ukatili wa kijinsia kwenye vyombo vya habari.

"Wizara imekua ikifanya jitihada za kuhakikisha ukatili wa kijinsia unakomeshwa kwa kutoa elimu kwa viongozi na Waandishi, na pia tunawataka wasisite kutoa taarifa endapo mtu atanyanyaswa ili tuzifanyie kazi, taarifa hizi ni siri kati ya Wizara na mtoaji taarifa" amesema Bi. Mduma wakati akitoa mada hiyo.

Mkurugenzi Msaidizi Usajili upande wa Idara ya Habari-MAELEZO Bw. Patrick Kipangula amesema wazo hilo la kuanzisha dawati la jinsia kwenye Idara hiyo ni zuri na kwamba litafanyiwa kazi kwa kuangalia uwezekano wa kuliingiza kwenye marekebisho ya mapitio ya kanuni.

"Ni wazo zuri, tumelipokea tutalifanyia kazi amesema Bw. Kipangula.


No comments:

Post a Comment

 
Copyright © 2016 Shamakala
Designed by Switch International | SHAMAKALA 360
    Twitter Facebook Google Plus Vimeo Videosmall Flickr YouTube