BREAKING

Tuesday 29 June 2021

RC SENDIGA APIGA MARUFUKU WANANCHI WA IRINGA KUTUPA TAKA HOVYO UKIKUTWA FAINI 50,000


Mkuu wa mkoa wa Iringa Queen Sendiga akiongea na wananchi wa manispaa ya Iringa juu ya umuhimu wa kufanya usafi wa mitaa yao na kuacha tabia ya kuharibu mazingira kwa makusudi
Mkuu wa mkoa wa Iringa Queen Sendiga akiongea na wananchi wa manispaa ya Iringa juu ya umuhimu wa kufanya usafi wa mitaa yao na kuacha tabia ya kuharibu mazingira kwa makusudi
Mkuu wa mkoa wa Iringa Queen Sendiga akimueleza jambo mama ntilie wa maeneo ya vibanda vya CCM manispaa ya Iringa na wa kwanza kushiro ni mwandishi wa habari Neema Msafiri akiwa makini mno akimsikiliza mkuu wa mkoa alipokuwa anatoa maagizo kwa mama natalie huyo

Mkuu wa mkoa wa Iringa Queen Sendiga amepiga marufuku wananchi wote kutupa takataka na kuchafua mazingira hovyo ili kuendelea kuyaweka mazingira kuwa masafi na na kuepuka kukumbana na magonjwa ya mlipuko.

Akizungumza mara baada ya kumaliza kufanya usafi kwenye maeneo mbalimbali ya mkoa huo,mkuu wa mkoa wa Iringa Queen Sendiga alisema kuwa mkoa wa huo umekuwa na sifa ya kuwa mkoa ambao unafanya vizuri kwenye swala la usafi hivyo wanapaswa kuendelea kufanya usafi na kuyaweka mazingira safi.

Alisema kuwa wananchi wa mkoa wa Iringa wanatakiwa kuzingatia kutotupa takataka hovyo kuanzia kwenye magari,nyumbani na kwa wananchi wanaotembea kwa miguu ili  kuuweka mji safi na kuwa mkoa wenye mazingira bora.

Sendiga alisema kuwa kuna changamoto za wananchi kutupa takataka kwenye mifereji ya maji machafu na kuzitelekeza taka hizo ambazo zimekuwa zikichafua mazingira hivyo wananchi wanatakiwa kusafisha mifereji yote kwa wakati ili kuokoa kusitokee mafuriko kipindi vua zikianza kunyesha.

Alisema kuwa licha ya mazingira ya mkoa wa Iringa kuendelea kuwa masafi lakini bado kuna changamoto kubwa kwa kuwa na baadhi ya maeneo hayaridhishi kama maeneo mengi hivyo juhudi binafsi za viongozi zinatakiwa kuhakikisha mitaa hiyo usafi unafanyika.

Sendiga alisema kuwa lengo lake ni kuhakikisha kuwa mkoa wa Iringa unashika namba moja kwa kuwa na mazingira bora na masafi na kuongoza kwa usafi kitaifa kama ambavyo ilikuwa miaka ya nyuma.

Kwa upande wake afisa mazingira wa manispaa ya Iringa Abdon Mapunda alisema kuwa wamejipanga kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu ya usafi kwa wananchi wote ili wajue umhimu wa kutunza mazingira yanayowazunguka.

Alisema kuwa wananchi wanatakiwa kuendelea kulipa ada ya taka ili kuviwezesha vikundi vya usafi kuendelea kufanya usafi na kutunza mazingira vizuri ya halmashauri ya manispaa ya Iringa.

Mapunda alisema kuwa mwananchi akikamatwa ametupa takataka hovyo na kuchafua mazingira atatozwa faini ya shilingi elfu hamsini (50,000) huku lengo lake likiwa kuhakikisha wananchi wanajifunza namna bora ya utunzaji wa mazingira.

Mapunda alisema kuwa wananchi wa manispaa ya Iringa wanatakiwa kuendelea kufanya usafi na kuyatunza mazingira kwa lengo la kuendelea kulinda afya kwa kuishi katika mazingira masafi.

Alimalizia kwa kusema kuwa wamezindua kampeni ya Iringa safi lakini bado wanakabiliwa na changamoto ya kuharibika kwa magari ya kubebea taka mara kwa mara jambo linalosababisha kupunguza kasi ya uzoaji wa taka. 

Naye mratibu wa kampeni ya Iringa safi Paulo Myovela alisema kuwa lengo la kampeni hiyo ni kuhakikisha wananchi wa manispaa ya Iringa wanafanya usafi na kuyapenda mazingira yao.

Alisema kuwa kampeni hiyo inakabiliwa na changamoto za ukosefu wa vifaa vya kukusanyia taka taka katika halmashauri hiyo hivyo viongozi na wadau mbalimbali kuhakikisha wanachangia jinsi ya kupatikana kwa vifaa hivyo.

No comments:

Post a Comment

 
Copyright © 2016 Shamakala
Designed by Switch International | SHAMAKALA 360
    Twitter Facebook Google Plus Vimeo Videosmall Flickr YouTube