BREAKING

Friday, 25 June 2021

MAWAZIRI SEKTA YA KILIMO WA AFRIKA MASHARIKI WAKUTANA, WAZIRI MKENDA ABAINISHA MKAKATI WA TANZANIA KUKABILIANA NA SUMUKUVU


Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano wa Mawaziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ulioketi tarehe 25 Juni 2021 katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa mjini Arusha (AICC).
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano wa Mawaziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ulioketi tarehe 25 Juni 2021 katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa mjini Arusha (AICC). 
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano wa Mawaziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ulioketi tarehe 25 Juni 2021 katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa mjini Arusha (AICC). 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Ndg Andrew Massawe (Katika) akifuatilia kwa makini mkutano wa Mawaziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliojumuisha pia wataalamu wa wizara za kisekta tarehe 25 Juni 2021 katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa mjini Arusha (AICC). 
Sehemu ya wataalamu mbalimbali wa Wizara ya Kilimo wakifuatilia kwa makini mkutano wa Mawaziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ulioketi tarehe 25 Juni 2021 katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa mjini Arusha (AICC). 
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Mashimba Ndaki wakiwa katika picha ya pamoja na wawakilishi wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki mara baada ya kumalizika kwa amkutano wa Mawaziri wa sekta hizo, tarehe 25 Juni 2021 katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa mjini Arusha (AICC). 

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Arusha

Mawaziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekutana tarehe 25 Juni 2021 katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa mjini Arusha (AICC ) kwa ajili ya kuweka mikakati ya pamoja ya kuendeleza sekta ya kilimo, mifugo na Uvuvi ikiwa ni pamoja na mambo mengine ya kupambana na nzige.


Kadhalika Mawaziri hao wamejadili na kuweka mikakati ya kuchochea na kuongeza biashara ya mazao na mifugo kwa kupitisha itifaki inayotoa mwelekeo wa namna ya kukagua usalama wa chakula.


Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo, Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa utekelezaji wa mikakati ya bara la Afrika katika sekta hizo na kuona kiasi kilimo kinachangia maendeleo ya uchumi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.


“Tanzania ni nchi yenye maslahi makubwa katika mkutano huu kwakuwa ni kapu la chakula katika nchi za Afrika Mashariki hivyo ni sehemu yetu nzuri ya kujenga mazingira ya biashara” Amesema Waziri Mkenda


Pamoja na mambo mengine kikao hicho kimekubaliana kwa kauli moja kuwa na ufuatiliaji na tathmini kwa mambo yote ambayo mikutano kama hiyo imekuwa ikikubaliana.


Waziri Mkenda amesema kuwa mkutano huo umejadili pia kuhusu upatikanaji wa mbolea kwa urahisi kwa wakulima ambapo sera maalumu imewasilishwa kwa ajili ya mapitio kwa nchi hizo zote ili kuwa na juhudi za pamoja ambazo zitapelekea kuweza kupata mbolea kwa bei rahisi katika nchi zote za Afrika Mashariki.


Kuhusu swala la Sumukuvu, Waziri Mkenda amesema kuwa Tanzania na nchi zingine zitaendelea kufuata itifaki za Afrika Mashariki kwani kuna kiwango ambacho kimewekwa na jumuiya hiyo ambacho kinavumilika.


“Hatutaki sisi tumuuzie mtu chakula ambacho kina madhara na kwa bahati nzuri vipimo vinafanyika mipakani na karibia asilimia 99.9999% ya mahindi yanapopimwa yapo vizuri na haya mengine ambayo tunakuta yana utata kidogo ni matatizo ya vipimo, kwa hiyo itifaki ya namna ya kushughulikia swala la sumu kuvu ilikuwepo katika jumuiya ya Afrika Mashariki na tuna wajibu wa kuitekeleza” Amekaririwa Prof Mkenda


Waziri Mkenda ameongeza kuwa Tanzania inalijali swala la Sumukuvu sio kwa sababu serikali inataka kuuza mazao nje bali ni kwa usalama wa wananchi watanzania na nje ya nchi ndio maana kuna mradi mkubwa kuliko nchi yoyote Afrika kwa ajili yakuhakikisha Sumukuvu inaendelea kupunguzwa katika mazao.


No comments:

Post a Comment

 
Copyright © 2016 Shamakala
Designed by Switch International | SHAMAKALA 360
    Twitter Facebook Google Plus Vimeo Videosmall Flickr YouTube