BREAKING

Saturday 11 July 2015

WAJUMBE WA KAMATI KUU(CC) YA CHAMA CHA MAPINDUZI, EMMANUEL NCHIMBI, SOPHIA SIMBA NA ADAM KIMBISA WAPINGA MAAMUZI YA KAMATI KUU (CC)

Mhe. Emmanuel Nchimbi akitangaza mbele ya wanahabari kwa kutoridhishwa na maamuzi yao kamati kuu(CC). (Picha na Kajunason Blog)

KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (CC-NEC) imetoa orodha ya wagombea watano bila ya jina la Edward Lowassa kuwemo ndani. Lakini katika hali inayoonesha mpasuko, baadhi ya wajumbe wa kamati kuu wamepinga uamuzi huo.
Majina yaliyopatikana, ambayo hata hivyo hayajatangazwa rasmi na chama, ni ya Bernard Membe, Dk. John Magufuli, Dk. Asha Rose-Migiro, January Makamba na Balozi Amina Salum Ali.
Membe ni mbunge wa Mtama na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Magufuli ni mbunge wa Chato na Waziri wa Ujenzi, Dk. Migiro ni mbunge wa kuteuliwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Makamba ni mbunge wa Bumbuli na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, na Balozi Amina ni Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Tume ya Umoja wa Afrika kwenye Umoja wa Mataifa, Marekani.
Maamuzi hayo hayakuwaridhisha baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu hasahasa wanaojulikana kuwa ni waungaji mkono wa Lowassa, na wametokeza hadharani kuyapinga huku wakilalamika kuwa kanuni zimevunjwa.
Dk. Emmanuel Nchimbi, Sophia Simba na Adam Kimbisa wamefika mbele ya vyombo vya habari mara tu kamati kuu ilipomaliza kikao chake usiku huu, na kusema hawakubaliani na kilichotendwa.
Wajumbe hao wakizungumza kwa kupokezana huku wakitoa kauli kali, wamesema kanuni za utendaji katika vikao vilivyotangulia Kamati Kuu zimekiukwa. Kamati Kuu ina wajumbe 32.
Wamesema ukiukaji umekuja pale Kamati Kuu ilipopatiwa majina matano, badala ya kupokea majina yote ya wanachama walioomba kuteuliwa, ili yenyewe ndiyo itoke na majina matano baada ya kuyafanyia uchambuzi.
“Kanuni zinasema Kamati Kuu itapokea majina ya waombaji wote na ikishafanya uchambuzi wa kila muombaji, yakiwemo maoni ya kamati ya usalama na maadili, ndiyo huchagua majina matano yanayofikishwa mbele ya Halmashauri Kuu,” alisema Dk. Nchimbi ambaye alitokea kama kiongozi wa hao wajumbe watatu.
Kimbisa ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, amesema hawakubaliani na maamuzi yaliyofanywa na Kamati Kuu kwa sababu hawakutarajia Kamati Kuu itakiukwa na kupokea majina ya baadhi tu ya waombaji.
“Haijawahi kutokea tangu nilipoingia katika Kamati Kuu kushuhudia ukiukaji wa kanuni kama ilivyotokea leo (jana) hii. Tumejitahidi kuuliza kwa mwenyekiti imekuaje kanuni inakiukwa lakini tumekosa maelezo ya kuridhisha,” amesema Simba, waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.


No comments:

Post a Comment

 
Copyright © 2016 Shamakala
Designed by Switch International | SHAMAKALA 360
    Twitter Facebook Google Plus Vimeo Videosmall Flickr YouTube