BREAKING

Friday 24 July 2015

HUDUMA YA UPASUAJI WA WATOTO WENYE UGONJWA WA KICHWA KUJAA MAJI NA MGONGO WAZI YAZINDULIWA RASMI KATIKA HOSPITARI YA RUFAA YA MKOA WA KAGERA


Na Faustine Ruta, Bukoba

Shirika lisilokuwa la serikali la Friends of Children with Cancer Tanzania (FOCC TZ) lazindua rasmi huduma ya upasuaji wa watoto wenye ugonjwa wa vichwa kujaa maji na mgongo wazi mkoani Kagera katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa ambapo jumla ya watoto arobaini wenye tatizo hilo wanatajiwa kufanyiwa upasuaji kuanzia Julai 25-26, 2015. 

Mkurugenzi wa shirika la FOCCTZ Bw. Walter Miya katika uzinduzi huo alisema kuwa baada ya kutoa matangazo kupitia redio za jamii mkoani Kagera kwa muda wa siku mbili wameweza kupata watoto 70 wenye tatizo la vichwa kujaa maji na mgongio wazi kutoka katika wilaya zote saba za mkao wa Kagera na nje ya mkoa. Bw. Walter alisema watoto walioweza kufikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera kwa msaada wa shirika lake ni 40 na watoto 30 wameshindwa kufika kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo wazazi kutokuwa na uwezo wa kuwasafirisha watoto hao, pia changamoto ya wananchi kuwa na imani potofu ya kuwa watoto hao wamerogwa

Huduma hiyo inatolewa mkoani Kagera na shirika la Friends of Children with Cancer Tanzania wakishirikiana na Madaktari wataalam wa upasuaji huo kutoka Hospitali ya Rufaa ya Bugando pia kutoka katika kitengo cha Muhimbili Orthopaedic Instutite (MOI) kilichopo Hospitali ya Rufaa ya Taifa Muhimbili. 




Daktari Gerald D. Mayaya kutoka idara ya upasuaji Hospitali ya Rufaa Bugando akielezea chanzo cha tatizo la ugonjwa wa kichwa kujaa maji na mgongo wazi alisema kuwa ni mishipa ya kusafirisha maji kichwani kuziba na kichwa huanza kuvimba ambapo kuna watoto huzaliwa na ugonjwa huo pia wengine upatwa na ugonjwa huo wakiwa tayari wamezaliwa na watu wazima pia hupatwa na ugojwa huo.
Lengo la kutoa huduma hiyo katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Kagera ni kupunguza gharama kwa wazazi wenye watoto wenye tatizo hilo badala ya kwenda Bugando na muhimbili wapate huduma hiyo karibu na maeneo yao. Pia kutoa ujuzi kwa wataalam wa haspitali ya Rufaa ya mkoa wa Kagera ili wawe wanatoa huduma hiyo katika hospitali hiyo. Alisema Mkurugenzi wa shirika la FOCCTZ Bw. Walter. 
Mkuu wa mkoa wa Kagera Mhe. John Mongella baada ya kuzindua huduma hiyo na kutembelea wodi ya watoto wenye tatizo la vichwa kujaa maji na mgongo wazi alisema amejifunza mambo mengi maana mwanzo alijua kuwa ugonjwa huo kwa watoto huzaliwa nao kumbe hata mara baada ya kuzaliwa au mtu mzima anaweza kupatwa na ugonjwa huo.




Mhe Mongella alitoa wito elimu kutolewa kwa wingi ili wananchi waweze kujua kuwa ugonjwa huo unatibika ili wazazi na walezi waweze kuwaleta watoto wenye tatizo hospitali ili wakatibiwe. Pia aliwashukuru Shirika la FOCCTZ kwa kuzindua huduma hiyo ambayo aliita huduma takatifu kwani inaokoa maisha ya watoto walio wengi. 

Wito, Mhe. Mongella alitoa wito kwa wananchi wenye uwezo kuweza kushirikiana na shirika hilo ili kuchagia huduma hiyo kuokoa maisha ya watoto. Pia alitoa wito kwa Wanahabari wa mkoa wa Kagera na Tanzania kwaujumla kuelimisha jamii juu ya tatizo hilo ili liweze kupunguzwa kwa kiasi kikubwa. 

Naye Vaileth John Makula (32) mzazi wa Gib Philimoni kutoka Wilaya ya Karagwe alilishukuru Shirika la FOCCTZ kuleta huduma hiyo Kagera maana anasema kuwa mwanae Gib alizaliwa katika hali ya kawaida na baada ya miezi minne tatizo la kuvimba kichwa lilianza na alimpeleka mtoto wake katika hospitali teule ya Wilaya Nyakahanga alikoambiwa ampeleke Bugando ambako hakumpeleka kwa kukosa nauli. Mama Gib alishukuru na alisema ana imani na madaktari hao kuwa watamponya mwanae Gib. 
Madhara ya ugonjwa wa kichwa kujaa maji na mgongo wazi unaweza kusababisha upofu wa macho, mtoto kutojiweza kabisa kutumia muda wote akiwa amelala tu, pia huathiri ubongo, na wakati mwingine husababisha vifo kwa watoto. 
Kwa takwimu alizotoa Bw. Walter alisema kwa kila watoto 1000 wanaozaliwa duniani watoto 2 huzaliwa na tatizo la kichwa kujaa maji, kwa nchi ya Tanzania watoto wote wanaozaliwa kwa mwaka watoto 4580 huzaliwa au hupatwa na ugonjwa huo ambapo kila watoto 1000 wanaozaliwa watoto 3 huwa na tatizo hilo. 
Shirika la Friends of Children with Cancer Tanzania lilianzishwa mwaka 2013 tayari limeweza kuwahudumia watoto 300 katika nchi nzima ya Tanzania na malengo yake ni kuendele kupunguza ukubwa wa tatizo kwa kuanzisha kambi za upasuaji kama walivyofanya mkoani Kagera. 
Mganga Mfawidhi wa Haspitalia ya Rufaa ya mkoa wa Kagera Dk. Juma Nyakina aliwashukuru shirika la FOCCTZ na liwahakikishia kuwa hospitali yake ipo tayari kwa kuwawekea mazingira mazuri wataalamu hao na kuandaa vitendanishi ili waweze kuifanya kazi yao kwa ufanisi mkubwa pia alisema wataalam wa hospitali hiyo wapo tayari kujifunza na kupata ujuzi huo. 

No comments:

Post a Comment

 
Copyright © 2016 Shamakala
Designed by Switch International | SHAMAKALA 360
    Twitter Facebook Google Plus Vimeo Videosmall Flickr YouTube