Grace Gwamagobe-Songwe.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe
Chiku Gallawa amesema atahakikisha anasimamia kwa ukaribu fedha zilizotolewa na
serikali Mkoani hapa kwa ajili ya upanuzi wa vituo vya afya ili zifanye kazi zaidi
ya ile iliyopangwa awali kutokana na kuongezeka kwa nguvu za wananchi.
Gallawa ameyasema hayo
mapema jana wakati wa ziara yake Wilaya ya Mbozi alipokagua maendeleo ya
upanuzi wa vituo vya afya vya Isansa kilichopokea milioni 500 na kituo cha Afya
cha Iyula Kilichopokea milioni 400, kwa ajili ya ujenzi wa maabara, nyumba ya daktari,
chumba cha upasuaji, jengo la mama na mtoto na chumba cha kuhifadhia maiti.
“Fedha hizi lazima
zifanye kazi iliyopangwa vizuri na pia tuongeze kazi nyingine ya ziada kutokana
na kuwa tumepata nguvu ya wananchi lakini pia mafundi wetu hawa tunaowatumia ni
wazawa na wenyeji wa maeneo ya kwetu kwahiyo gharama zao zitatupa unafuu ambao
tunatakiwa kuutumia kuongeza kazi nyingine”, amesema Gallawa.
Ameongeza kuwa licha ya
upanuzi wa vituo vya afya kuchelewa kuanza bado ana Imani kuwa wataweza
kumaliza ndani ya muda uliopangwa kutokana na uchapakazi wa mafundi wazawa wa
maeneo hayo.
Gallawa amesema kukamilika
upanuzi wa vituo hivyo vya afya kutavifanya vituo hivyo vivutie na hata mgonjwa
akifika apate matumaini ya kupona na sio kukatishwa tamaa na hali mbovu ya
mazingira.
“Tiba ya kwanza ya
mgonjwa akifika kituo cha afya akute mazingira yanavutia na sio majengo mabovu
na uchafu hivyo vitamfanya akate tamaa ya kupata matibabu sahihi, tukimaliza
ujenzi wa hayo majengo tutahakikisha tunapaka rangi paa za majengo yote
zifanane ili vituo vyetu vya afya vivutie”, amefafanua Gallawa.
Aidha Gallawa amemtaka Kaimu
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi Lauteri Kanoni kuhakikisha anaweka
mfumo wa maji safi katika vituo hivyo hasa mfumo wa kuvuna maji ya mvua ili vituo
vikikamilika maji yawepo kwa ajili ya matumizi.
Naye Mkazi wa kijiji
cha Isansa Wilaya ya Mbozi Bi Stela Mkeya ameonyeshwa kufurahishwa na upanuzi
wa kituo cha Afya Isansa huku akieleza baadhi ya kero walizokuwa wakizipata
awali.
“Tunaishukuru sana
serikali ya Magufuli kwakweli wametusaidia, tulikuwa tunapata shida kufuata
huduma za upasuaji wa akina mama wajawazito huko hospitali ya Wilaya iliyopo
Vwawa lakini pia hapa kwenye kituo cha afya mzazi akijifungua hata mazingira ya
kwenda kujisafisha vizuri kama vile mabafu yakiwa hayatoshi kabisa”, ameeleza
Bi Mkeya.
Kwa upande wao mafundi
waliokabidhiwa kazi ya upanuzi wa vituo hivyo vya Afya wameonyesha ari ya
kufanya kazi hiyo kwa ufanisi na haraka huku wakimuomba Mkuu wa Mkoa Chiku
Gallawa awasaidie upatikanaji wa taa ili waweze kufanya kazi mchana na usiku
naye Mkuu wa Mkoa amekubaliana na mapendekezo hayo.
No comments:
Post a Comment