BREAKING

Thursday 11 May 2017

WATANZANIA KUISHUHUDIA SERENGETI BOY'S LIVE DSTV


Mamilioni ya watanzania watapata fursa ya kuishuhudia timu yetu ya vijana - Serengeti boys inayoshiriki michuano ya vijana ya AFCON Mubashara kupitia king’amuzi cha DStv. Michuano hiyo itakayoanza 14 hadi 28 mwezi huu wa Mei itashirikisha mataifa 8 kutoka bara la Africa.
Michuano hiyo itaonekana mubashara kupitia king’amuzi cha DStv tena katika kifurushi cha bei nafuu kabisa cha Bomba, kinachopatikana kwa shilingi 19,975/= na hivyo kuwawezesha watanzania wengi zaidi kuwashuhudia vijana wetu wanavyopambana kuliletea taifa sifa katika ulingo wa kandanda.
Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania Maharage Chande, amesema kuwa kitendo cha michuano hiyo kuonekana kwenye vifurushi vyote vya DStv, kinamaanisha watanzania tutashuhudia mtanange huo Mubashara tena kwa kiwango cha juu, hivyo kuupata uhundo huo ukiwa bado wa moto. “Tunafahamu ni jinsi gani watanzania wanasubiri kwa hamu kuwaona vijana wetu wanavyopambana kufa na kupona, hivyo sisi DStv, tumeamua kuonyesha michuano hiyo live tena katika vifurushi vyote hadi kile cha bei nafuu kabisa cha Bomba ambacho ni shilingi 29975 tu.” Alisema Maharage.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, michuano hiyo itaonekana katika chaneli 209-SuperSport9 na chaneli 233-SuperSport Select, ambayo pia inapatikana katika kifurushi cha Bomba.
Huku michuano hii ikiaminika kuwa moja ya nafasi muafaka kwa Serengeti boys kufuzu kwenda Kombe la Dunia la vijana litakalofanyika nchini india mwishoni mwa mwaka huu, Watanzania wengi wanaimani na timu hiyo hasa ukizingatia mazoezi waliyofanya ikiwemo michezo ya majaribio pamoja na muda waliokaa kambini.
Serengeti Boys watacheza mechi yao ya kwanza siku ya Jumatatu 15 Mei kabla ya kukabiliana na Angola siku ta Alhamisi 18 Mei na hatimaye Niger siku ya Jumapili 21 Mei.
Matumaini makubwa ya watanzania yapo kwenye kikosi hicho imara chenye wachezaji mahiri kama Nickson Kababage, Shaaban Ada na Kelvin Nashon  ambao wanatarajiwa kuongoza mashambulizi makali ya kuwabomoa mahasimu wao katika michuani hii. 
Michuano ya AFCON kwa wachezaji wenye umri wa miaka chini ya 17 ya mwaka huu ni ya 12 kwa kuzingatia michuano inayohusisha nchi waandaaji, inayoandaliwa na shirikisho la soka barani Afrika (CAF) kwa wachezaji wenye umri wa chini ya miaka 17.  Washindi wane watapata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Dunia la wachezaji wa umri wa chini ya miaka 17 litakalofanyika ncini India mwishoni mwa mwaka huu.
Michuano ya mwaka huu ilipaswa ifanyike nchini Madagascar tarehe 2–16 April 2017 lakini CAF ikaamua kuihamishia Gabon kwa sababu Madagascar haikukidhi vigezo.
Mataifa yaliyofuzu  kushiriki michuano hii mwaka huu ni  wenyeji Gabon, Tanzania, Mali, Angola, Cameroon, Ghana, Guinea, na Niger.

No comments:

Post a Comment

 
Copyright © 2016 Shamakala
Designed by Switch International | SHAMAKALA 360
    Twitter Facebook Google Plus Vimeo Videosmall Flickr YouTube