BREAKING

Wednesday, 1 February 2017

KAMBI VYUO VYA ELIMU YA JUU-CCM YAFUNGWA DODOMA

Kaimu Katibu Mtendaji wa Shirikisho la Vyuo vya Elimu ya Juu, Daniel Zenda akizungumza wakati wa kufungwa Kambi ya Vijana 219,  waliokuwa katika kambi ya kukuza Uzalendo, iliyowekwa Hombolo mkoani Dodoma.

NA MWANDISHI WETU


Shirikisho la vyuo vya Elimu ya Juu nchini, limewahimiza Vijana kuzidisha uadilifu na uzalendo ili kufikia malengo yatakayoakisi CCM mpya na Tanzania mpya, kama anavyotaka Mwenyekiti wa Chama, Rais John Magufuli.

"Ili matakwa haya ya Rais wetu na Mwenyekiti wa Chama, yaweze kufikika, ni lazima  Watanzania  hasa sisi vijana, tubadilike, kifikra na kimtazamo na kuacha kufanya kazi kwa mazoea", alisema Kaimu Katibu Mtendaji wa Shirikisho hilo, Daniel Zenda, wakati wa kufungwa kambi maalum ya siku tatu ya Vijana kutoka  vyuo mbalimbali, nchini, jana, Hombolo, mkoani Dodoma.


Zenda alisema, mabadiliko ya kifikra, mtazamo na kiutendaji, ndivyo vitakavyoonyesha udhati wa vijana na Watanzania kwa jumla katika kuendelea kumuunga mkono, Rais Dk. Magufuli, katika jitihada zake za kuiletea Tanzania mabadiliko makubwa ya kimfumo na kiutendaji kwa kushika misingi ya kuinua uchumi huku akipambana na uzembe na ubadhirifu.


Zenda, aliwapongeza vijana 219, walioshiriki katika kambi hiyo, akisema, mafunzo ya ukakamavu na yale ya kujenga utaifa, waiyopata kwa muda wa siku tatu hadi kufikia jana, yatawasaidia sana, katika kutambua nafasi yao katika kulitumikia taifa kwa uadilifu na uzalendo mkubwa.


Aliwataka Wanashirikisho la vyuo vya Elimu ya Juu katika mikoa mbalimbali kuendelea kufanya shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwa ni kutekeleza maagizo  yanayotaka kila mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuhakikisha anashiriki shughuli kama hizo ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya miaka 40 ya kuzaliwa kwa CCM.


Zenda aliipongeza Viongozi wa Shirikisho katika baadhi ya mikoa ikiwemo Dar es Salaam, Mbeya, Arusha na Dodoma ambao tayari wamekuwa wakishirikiachama na wanachama na wananchi kwa jumla katika kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kufanya usafi na kujitolea damu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho hayo ya miaka 40 ya CCM ambayo kilele chake ni Februari 5, 2017.


Kambi hiyo ya Hombolo ilifungwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Zainabu Abdalla Issa, ambaye akifunga kambi hiyo alisema, kwa kuwa CCM imekuwa ikionyesha kuwajali vijana kwa kuweka mipango mbalimbali ya kuwaendeleza sambamba na watanzania wengine, basi hawana budi nao kuhakikisha CCM inazidi kuimarika na kuwa CCM mpya.

HABARI KATIKA PICHA


 Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyuo vya Elimu ya Juu, Mkuu wa Wilaya ya Pangani mkoani Tanga, Zainabu Abdallah Issa, akizungumza wakati wa kufunga Kambi ya Vijana 219 wa Shirikisho hilo, jana, Hombolo mkoani Dodoma.
 Vijana walioshiriki Kambi wakiwa ukumbini
 Baadhi ya viongozi wa Shirikisho la Vyuo vya Elimu ya Juu, wakiwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula alipotembelea kambi ya Vijana 219 wa Shirikisho hilo, Hombolo mkoani Dodoma. Kulia ni Kaimu Katibu Mtendaji wa Shirikisho hilo Daniel Zenda
 Makamu Mwenyekiti wa CCM, Bara, Philip Mangula akishiriki kuimba wimbo wa Uzalendo, alipowasili katika ukumbi kwenye kambi ya Vijana wa Shirikisho la Vyuo vya Elimu ya Juu, iliyokuwa imewekwa Hombolo mkoani Dodoma. Kushoto ni Kaimu Katibu Mtendaji wa Shirikisho hilo Daniel Zenda
 Vijana waliokuwa katika kambi ya Uzalendo Hombolo mkoani Dodoma wakiwa ukumbini wakati wa kufunga kambi hiyo jana.
 Makamu Mwenyekiti wa CCM, Bara Philip Mangula akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Shirikisho la Vyuo vya Elimu ya Juu, alipotembelea kambi hiyo
 Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyuo vya Elimu ya Juu, Zainab Abdallah Issa akijadili jambo na Kaimu Katibu Mtendaji wa Shirikisho hilo Daniel Zenda wakati wa kufungwa Kambi ya Vujana wa Shirikisho hilo Hombolo mkoani Dodoma jana

No comments:

Post a Comment

 
Copyright © 2016 Shamakala
Designed by Switch International | SHAMAKALA 360
    Twitter Facebook Google Plus Vimeo Videosmall Flickr YouTube