BREAKING

Tuesday 16 February 2016

SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU NCHINI 'TFF' LAMTANGAZA JONESIA RUKYAA KUTOKA KAGERA KUWA MWAMUZI WA KATI KWENYE PAMBANO LA WATANI WA JADI SIMBA NA YANGA JUMAMOSI HII

Jonesia Rukyaa akiwa tayari kwa ajili ya kuchezesha pambano la watani wa Jadi Simba na Yanga msimu uliopita.

Jonesia Rukyaa akikabidhiwa Beji  ya FIFA na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania Jamal Malinzi


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF  limemtangaza Mwamuzi mwanamama Jonesia Rukyaa kuwa mwamuzi wa kati kwenye pambano la watani wa jadi kati ya Simba na Yanga, mchezo utakaopigwa mwishoni mwa juma hili katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam

Aidha mwamuzi huyo mwenye beji ya FIFA atasaidiwa na Josephati Bulali kutoka Tanga pamoja na Samweli Mpenzu mkazi wa Arusha, mwamuzi wa akiba anatarajiwa kuwa Elly Sasii wa Dar es Salaam huku kamisaa wa mchezo huo akiwa Khalid Bitebo wa Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya TFF afisa habari wa shirikisho hilo Baraka Kizuguto amesema maandalizi kuelekea mchezo huo yamekamilika hivyo akiwasihi wadau pamoja na mashabiki wa soka kujitokeza kwa wingi kununua tiketi kwa ajili ya mchezo huo ambazo zitaanza kuuzwa rasmi majira ya saa mbili asubuhi siku ya ijumaa.

Kizuguto ametaja pia viingilio vya mchezo huo kuwa  Shilingi 7000 kwa viti vya Blue na Kijani, elfu 10, kwa viti vyenye rangi ya Machungwa, shilingi elfu 20 kwa VIP B na C, huku viti vya VIP A vikiwa shilingi elfu 30.

Sambamba na mechi hiyo ya simba na yanga, kuna michezo mingine itakayopigwa siku hiyo ambapo Mbeya City watacheza na Azam katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Stand United itacheza na JKT Ruvu uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Toto Africans na Kagera Sugar CCM Kirumba jijini Mwanza, Mgambo Shooting dhidi ya Tanzania Prisons katika Uwanja wa Mkwakwani Tanga, n Majimaji fc wao wakiwa wageni wa Mtibwa katika uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Ligi hiyo pia itaendelea siku ya jumapili kwa michezo miwili ambapo Mwadui FC dhidi ya Coastal Union kwenye uwanja wa Mwadui Complex, na Ndanda FC watacheza na African Sports uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.



No comments:

Post a Comment

 
Copyright © 2016 Shamakala
Designed by Switch International | SHAMAKALA 360
    Twitter Facebook Google Plus Vimeo Videosmall Flickr YouTube