BREAKING

Tuesday 9 February 2016

KWA NINI MKULIMA MWAMWINDI ALIMPIGA RISASI RC DK.KLERUU?,KWA HISANI YA MJENGWA BLOG



Ndugu zangu,
Mwaka 2011 nilipata bahati ya kukutana na kuongea mwana wa Mkulima Saidi Mwamwindi aitwaye Amani Mwamwindi ( Pichani). Tulikutana nyumbani kwake Mlandege, Iringa. Wakati huo, Amani Mwamwindi alikuwa ni Meya wa Manispaa ya Iringa.
Tukiwa tumekaa wawili sebuleni, Mzee Amani Mwamwindi alikuwa na haya ya kusema juu ya tukio lile la Desemba 25, 1971, siku ya Krismasi.
“Niliporudi nyumbani kutoka Ifunda nikazikuta habari hizo mbaya. Nikaenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa Mzee pale Mshindo. Nikawakuta akina mama wanalia.
“Ilikuwa ni kilio. Hiyo bado ilikuwa ni siku ya Krismasi. Nikauliza; kuna aliyekwenda kumwona baba pale polisi? Jibu likawa hapana. Nikaenda moja kwa moja polisi ili nikamwone baba na nimsikie kauli yake.
Nilipofika polisi nikaanza kujieleza kwa askari polisi kuomba ruhusa ya kuongea na Mzee. Wakati nikifanya hivyo mzee nae alisikia sauti yangu. Akatamka;
” Mwanangu huyo, mruhusu niongee nae”.
Nikaongea na Mzee.
“Niliweza kuongea na Mzee na kupata picha ya kilichotokea. Niliondoka kurudi nyumbani. Habari zilishasambaa. Hali haikuwa nzuri. Mji wa Iringa ulitulia sana. Halafu ukaja mtikisiko mkubwa. Wazee wengi walioishi mjini na waliokuwa wakilima na Mzee kule Isimani walisombwa na vyombo vya usalama.”
Je, ni kina nani hao? Namwuliza Amani Mwamwindi. Anajibu;
“Mzee kama Ibrahim Khalili, Mursali na wengine. Watu kama 30 hivi walisombwa na kupelekwa sehemu mbalimbali za nchi. Kuna waliopelekwa Mwanza, Shinyanga hata Zanzibar. Kwa namna fulani walitenganishwa katika sehemu hizo.”
Je, na wewe ulikumbwa na msukosuko huo?
“Ndio, hata mimi nilihojiwa ingawa niliachwa niendelee na kazi zangu. Kumbuka nilikuwa kijana wa miaka 21 tu, na siku ya tukio nilikuwa shambani kwangu Ifunda. Hapa nyumbani kwangu kulikuwa na askari wa FFU muda wote. Katika kuhojiwa kwangu maswali mengine yalikuwa hayana msingi.
Kwa mfano, niliulizwa;
Mzee alipokuja hapa kwako kutoka Isimani siku ya tukio alitaka kukwambia nini? Sasa, mimi hakunikuta nyumbani na hatukuongea, nitajuaje alichotaka kuniambia siku hiyo? Anaeleza Amani Mwamwindi, akionyesha kushangaa, hata hii leo.
Je, kwa wakati huo, wewe na familia yenu mlihisi kutengwa na jamii kutokana na kitendo alichofanya Mzee Mwamwindi? Namwuliza.
Namwona Amani Mwamwindi akionyesha kuguswa sana na swali hili.
“Tulikuwa na wakati mgumu sana kama familia. Kibaya zaidi kwetu ilikuwa ni kuingia kwenye uhasama na ndugu wa jamaa ambao wazee wao walisombwa na vyombo vya usalama na kwenda kusikojulikana.
“Kwao waliamini kama isingekuwa Mzee wetu Mwamwindi kufanya tendo lile, basi, wazee wao wangebaki salama na kuendelea na shughuli zao za kilimo. Hivyo basi tulisakamwa na wengine ambao ni ndugu zetu.”
Mlifanyaje kuikabiili hali hiyo?
“Tulifikia uamuzi mimi niende Dodoma kwenye gereza alikokuwa Mzee Mwamwindi. Niende nikamjulishe baba juu ya hali iliyotokea huku nyumbani. Kwamba tuna uhasama na jamaa wa waliosombwa na vyombo vya dola.
Nilipata kibali cha DC hapa Iringa. Kibali cha kwenda kumwona Mzee kule Dodoma. Nilipofika Dodoma nikaonana naye. Tukazungumza. Nikamwambia shida ya nyumbani. Alisikitika sana.
Akaniuliza; “Sasa tufanyeje?”. Nikamshauri aandike barua kwenda kwa Nyerere kumwomba atusaidie. Baba aliandika barua siku hiyo hiyo. Alimwandikia Nyerere kumwambia na kumhakikishia kuwa ni yeye Said Mwamwindi na si mtu mwingine yeyote aliyehusika na tendo alilofanya; kumpiga risasi na kumuua Kleruu.
Barua ile ilifika kwa Nyerere, na haukupita muda mrefu, wazee wale wakulima wa Isimani waliachiwa huru na kurudishwa Iringa. ”
Je, hali ya uhusiano na waliowachukia ilibadilika na kuwa njema baada ya wazee hao kurudi Iringa? Namuuliza Mzee Amani Mwamwindi.
“Ndio, kabisa. Hali ikawa shwari. ” Je, wazee wale wakulima wa Isimani walirudi na kuendelea na kazi zao za kilimo?
“Niseme kuwa walirudi Iringa wakiwa wameathirika kisaikolojia. Kuna ambao hawakutaka kabisa kurudi tena Isimani. Baadhi yao hawakuishi muda mrefu, walifariki. Sijui nini kiliwatokea.”
Je, unafikiri Iringa ingekuwaje kama tukio lile la siku ya Krismasi mwaka 1971 lisingetokea?
“Naamini kabisa, Iringa isingekuwa kama ilivyo sasa. Ingeendelea sana. Unajua kulikuwa hakuna mahala pengine katika nchi hii ambapo kulikuwa kunazalishwa mahindi kushinda Isimani.
“Mzee na wenzake walilima ekari nyingi sana. Naamini wangelima zaidi. Walianza kujijenga na hata waliunda ushirika wao. Tukio lile lilisimamisha kasi ya kilimo Isimani. Ni kama laana fulani vile, maana, tangu wakati ule mvua zimekuwa za taabu Isimani,” anasema Mzee Amani Mwamwindi. Kisha namwuliza tena.
“Nilifika pale nyumbani kwenu Isimani, nikaona mnara wa kumbukumbu ya Dk. Kleruu, kwanza nilifikiri ni kumbukumbu ya Mwamwindi. Je, unajisikiaje kuona nyumbani kwenu kuna mnara wa kumbukumbu ya Dk. Kleruu na si ya baba yenu?”
“Mimi naona ni sawa kabisa kwa mnara ule kuwa pale”. Ananijibu Mzee Amani Mwamwindi huku akionyesha kuchangamka. Anaendelea.
“Unajua hata Nyerere alipofika Isimani wakati fulani aliuliza; ” Hivi huu mnara ni wa kumbukumbu ya Dk. Kleruu au Said Mwamwindi?” Nyerere alikuwa na maana yake.” Ananiambia Mzee Amani Mwamwindi. Kuna kitu anataka kufafanua, anasita. Namwacha aendelee kutafakari.
Kisha ananiuliza swali gumu. Nabaini ni mara ya kwanza katika mazungumzo yetu ameamua kunirushia swali. Kwa mtazamo wangu ni swali la kifalsafa. Mzee Amani Mwamwindi ananiuliza;
“Bwana Mjengwa, mche unaochipua ardhini unahitaji kumwagiliwa maji ili uendelee kuchipua. Ukisimama vema unauacha ukue wenyewe. Na je, ukishakua na kukomaa unaufanyaje?”. Mzee Amani Mwamwindi ananiuliza huku akinitazama usoni.
Naam, ni swali gumu lenye kunihitaji, sio tu kufikiri, bali kufikiri kwa bidii. Jibu lake lazima lifuatiwe na majadala.
Ewe msomaji mpendwa, kabla sijaingia kwenye nilichomjibu Mzee Amani Mwamwindi na mwendelezo wa mazungumzo yetu nakutoa nje ya nyumba ya Amani Mwamwindi pale Mlandege.
Maana, mpaka kufikia hapa tumemsikia Mzee Amani Mwamwindi, kama mwanafamilia ya marehemu Said Mwamwindi akisimulia kilichotokea.
Iringa Mjini kuna mmoja wa wazee wa siku nyingi, Mzee Omar Mselem Nzowa... Itaendelea...
Maggid,
Iringa.(P.T)

No comments:

Post a Comment

 
Copyright © 2016 Shamakala
Designed by Switch International | SHAMAKALA 360
    Twitter Facebook Google Plus Vimeo Videosmall Flickr YouTube