Wakulima Mkoani Njombe wamewashukuru watafiti na Serikali
kwa kuwezesha kupatikana kwa mbegu bora za muhogo ambazo zinauwezo wa kustawi
kwenye maeneo ya baridi hasa nyanda za juu kusini baada ya utafiti wa mwaka mmoja ulifanywa na watafiti kutoka
kituo cha utafiti wa kilimo cha Mikocheni MARI na chuo kikuu cha Dar es salaam.
Wakulima na wakazi wa kata ya Lupembe Mkoani Njombe wakifurahia mavuno makubwa ya mbegu za Muhogo zinazostawi kwenye maeneo ya baridi kali. |
Wakiongea kwa furaha wakati wa zoezi la kuvuna mihogo hiyo ambayo ilipandwa mwaka mmoja uliopita wakulima hao wamesema sasa wamepata zao la biashara la uhakika baada ya zao la la chai kusumbua biashara yake .
Akiongea kwa niaba ya wakulima wenzake bwana Mapambano
Luhongori Mkazi wa kijiji cha Lupembe wilaya ya njombe mkoani humo amesema kuwa
Zao la Muhogo sasa litakuwa mkombozi kwa wakulima wengi ambao wamekuwa na
shauku ya kulima zao hilo ili kuweza kunufaika na fursa kubwa ambazo wanazipata
wakulima wa mikoa mingine kama vile Mara, Geita na Pwani.
‘’ Kutokana na uhitaji na soko kubwa la muhogo mkoani njombe
nimejaribu mara kadhaa kulima zao la muhogo bila mafanikio lakini siamini macho
yangu leo kuona katika eneo hilihili ambalo tulipanda mbegu hizi bora za
watafiti kwenye shamba darasa imetoka mihogo mingi na mizuri kiasi hiki, ila
nimegundua kuwa mbegu tulizokuwa tunatumia za kienyeji hazifai ukanda wetu’’
Alisema Luhongoli mkulima kutoka mkoa huo.
Mtafiti kiongozi wa Utafiti huo Dkt. Joseph Ndunguru akifafanua jambo kwa wakulima mara baada ya kuvuna baadhi ya mashina hayo kwenye kila aina 75 walizopanda eneo hilo. |
Kwa upande wake Bi Rehema Malekela ambaye pia alishiriki
kuanzia mwazo wa utafiti mpaka wakati huu wa kuvuna amesema kilimo cha zao hilo
kilikuwa kidogo sana ambapo familia zimekuwa zikilima mashina machache
kuzunguka nyumba kwaajili ya vitafunywa vya chai tu baada ya kuona zao hilo
haliwezi kuwapatia tija kama wakulima wa maene mengine nchini.
Bi Malekela ameongeza kuwa wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu
wa ramadhani waislamu hupata shida sana kupata muhogo na hivyo kuwalazimu
baadahi ya wafanyabiashara wengi kwenda kufuata mihogo kwenye mikoa mingine
inayozalisha zao hilo kwa wingi na kuja kuiuza mkoani humo kwa bei kubwa.
“ Kwakweli ukifunua moyo wangu na moyo wa kila mtu
unayemuona hapa aliyekuja kushiriki zoezi hili utaona furaha isiyo na kifani
ndio maana unaona tumejitokeza kwa wingi watu kutoka Tarafa nzima kuja
kushuhudia kupatikana kwa zao linguine la biashara kwenye eneo letu” Alisema
Bi. Malekela kwa niaba ya wakina mama wengine.
Mamia ya wakulima na wakazi wa Kata ya Lupembe na maeneo mengine waliojitokeza kuangalia matokeo hayo ya utafiti kuona kama wanaweza kulima Muhogo kwenye ukanda huo wa baridi kali. |
Aliongeza kuwa kingine kikubwa wanachowashukuru watafiti hao
ni kuwaahidi kuwapelekea mbegu hizo kila mkulima kupitia vikundi vyao na
kuwafundisha namna ya kuchakata muhogo na kupata bidhaa mbalimbali kama vile
clips,Biskuti,Maandazi na aina zingine za vyakula ili kuongeza thamani ya zao
hilo.
Kwa upande wake mtafiti kiongozi wa utafiti huo kutoka Kituo
cha utafiti wa Kilimo Mikocheni MARI Dkt. Joseph Ndunguru amesema kuwa kwa muda
mrefu wakulima kwenye maeneo ya baridi wamekuwa hawalimi zao hili hali ambayo
imekuwa ikiwakosesha fursa mbalimbali zitokanazo na zao hilo ambazo wakulima wa
maeneo yenye joto wanazipata kwa kuzalisha muhogo.
Amesema katika utafiti huo wamepeleka mbegu aina 75 za
muhigo katika maeneo matatu ya utafiti huo ambayo ni Mkoa wa Njombe ambapo wanaangalia aina za muhogo kati
ya hizo ambazo zitastawi na kuvumilia baridi hadi la nyuzijoto 16 -22C na eneo linguine
ni mkoa wa Dodoma kuangalia aina ya mihogo itakayoweza kuvumilia ukame na Mkoa
wa Pwani katika eneo la Chambezi ambapo wanaangalia changamoto ya joto na
magonjwa.
‘’ Kwakweli tumepata mafanikio makubwa sana kwa mfano kwa
Mkoa wa Njombe kwenye baridi ,aina 47 kati ya aina 75 tulizopanda kwenye shamba
hili kwenye eneo lenye bardi zaidi tum eona
zimefanya vizuri sana nah ii ni kutuonyesha kuwa sasa wakulima wa eneo hilo
wanaweza kunufaika na kilimo hiki’’ Alisema Dkt. Ndunguru.
Mtafiti huyo ameongeza kuwa pamoja na kufanya vizuri kwa
aina hizo 47 lakini wamegundua kuwa katika eneo hilo shina linatoa mihogo mingi
sana lakini haiwezi kukomaa kwa muda wa mwaka mmoja kama ilivyo kwenye maeneo
yenye joto na hivyo kuhitaji muda zaidi ya mwaka mmoja ili inenepe na kukomaa
vizuri.
Kwa upande wake mtafiti kutoka Chuo kikuu cha Dar es salaam
Dkt. Gladness Temu ambaye ni mtafiti katika mradi huu amesema kuwa katika
kipindi chote cha utafiti huo wamekuwa wakitembelea shamba hilo na kuchukua
takwimu mbalimbali muhimu ambazo zitakuja mwishoni kusaidia katika hitimisho na
mapendekezo kwa wakulima.
Dkt. Gladness Temu akiinua shina la Muhogo walilovuna huko Chambezi hivi karibuni. |
Amesema miongoni mwa taarifa hizo ni pamoja na kuangalia
kama mbegu hizo zinashambuliwa na magonjwa ya batobato na michirizi ya kahawia
magonjwa mabayo ni hataro sana kwa mihogo kwa sasa lakini hayakujitokeza kabisa
kwenye shamba hilo hali ambayo inawafanya kuamini uzalishaji utakuwa mkubwa
sana katika eneo hilo.
‘’ Katika kuhakikisha magonjwa hayo hayatokei kabisa
tutawaletea mbegu bora na safi ili waanze kilimo hicho bila magonjwa nah ii itawasaidia
sana sasa kuwa wazalishaji wa mbegu za muhogo wazuri maana eneo lao halina
magonjwa hayo kwa sasa’’ Alisistizia
Dkt. Gladness.
Mradi huu wa utafiti unafanywa kwa kushirkiana na nchi Tatu
za Tanzania,Kenya na Hispania kwa ufadhili wa shirikala la maenedeleo la umoja
wa Ulaya kupitia kwa shirikala la chakula na kilimo duniani FAO.
Baadhi ya wafanyakazi wa kituo cha utafiti wa Kilimo Mikocheni cha jijini Dar es salaam MARI wakifurahi wakati waliposhirikiana kuinua shina moja la Muhogo huko Chambezi Bagamoyo. |
No comments:
Post a Comment