Serikali imetoa wito kwa Vyama,Vilabu na
Mashirikisho ya mpira wa miguu kuzingatia na kufuata taratibu
zilizowekwa kwa mujibu wa katiba zao ili kupunguza migogoro inayoweza
kujitokeza katika uendeshaji na uendelezaji wa soka nchini.
Hayo yamesemwa Leo Bungeni Mjini Dodoma na
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Annastazia
Wambura wakati akijibu swali la Mhe. Khatibu Saidi Haji Mbunge wa Konde
(CUF) kuhusu makosa yanayofanywa na klabu za soka nchini kwa kupeleka
mambo ya kisoka katika mahakama ambapo ni kinyume cha sheria za FIFA.
Mhe. Annastazia Wambura amesema ni kweli
kuwa Sheria za FIFA zinakataa mambo yanayohusiana na soka kupekekwa
mahakamani hivyo hatua hiyo ya Vyama na Klabu kuzingatia Sheria na
taratibu inalenga kuwezesha masuala ya soka kuendeshwa kwa kuzingatia
taratibu na miongozo iliyowekwa na Mamlaka za Michezo huo kwa ngazi
mbalimbali.
Aidha amesema hatua hiyo imewezesha mchezo
wa soka kuchezwa na kupata matokeo kwa wakati na hivyo kuepusha mazuio
ya mahakama ambayo yanaweza kusababisha usumbufu usio wa lazima kwa
washiriki wengine hata kupelekea kufungiwa kwa Shirikisho la Soka
Tanzania(TFF).
Maendeleo ya michezo
hapa nchini yanaendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Baraza la Michezo ya
mwaka 1967, kama ilivyorekebishwa kwa mujibu wa Sheria Na 6 ya mwaka
1971 lakini bado Sheria hii inakinzana na Sheria za FIFA ila serikali
inafanya mapitio ya Sheria hiyo ili iendane na wakati kwa lengo la
kuboresha na kuendeleza michezo nchini.
No comments:
Post a Comment