WATU 4 wamepoteza maisha na wengine 35 wamejeruhiwa baadhi yao wakiwa katika hali mbaya baada ya basi la abiria mali ya kampuni ya LUWINZO linalofanya safari zake kati ya Dar Es Salaam na Njombe kuligonga kwa nyuma gari kubwa la mizigo katika kijiji cha Kinegembasi kata ya Mbalamaziwa wilayani Mufindi mkoani Iringa.
Ajali hiyo imetokea leo asubuhi majira ya saa 3 ambapo basi hilo lilikuwa likitokea mkoani Njombe kuelekea jijini Dar Es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Iringa, Peter Kakamba amezitaja nambari za usajili za magari hayo yaliyohusika katika ajali hiyo kuwa ni T 782 AZR ambalo ni basi la LUWINZO na T 718 CRV lori la mizigo lililokuwa limebeba shehena ya makaa ya mawe.
Kamanda Kakamba amesema ajali hiyo imetokea baada ya dereva wa basi hilo kujaribu kulipita lori la mizigo lililokuwa likitokea mkoani Ruvuma kuelekea mkoani Tanga na kwamba watu wawili wamepoteza maisha katika eneo la ajali na wengine wawili wamefariki wakiwa njiani wakati wakipelekwa hospitalini kwa matibabu zaidi.
Amewataja waliopoteza maisha katika ajali hiyo kuwa ni Rashidi Kibalala,. Salim Changwila ambao wote walikuwa wafanyakazi wa basi hilo.
Aidha amesema majina ya marehemu wengine wawaili bado hayajajulikana huku akibainisha chanzo cha ajali hiyo kuwa ni uzembe wa madereva na mwendo kasi.
No comments:
Post a Comment