BREAKING

Tuesday, 9 January 2024

MLOGANZILA WAZINDUA HUDUMA YA MAFUNZO YA WAGONJWA WA KIHARUSI








Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa kushirikiana na Taasisi ya Kiharusi Duniani (The World Stroke Organization) imezindua mafunzo maalumu kwa wataalamu wanaoshughulikia magonjwa ya kiharusi kwa lengo la kuendelea kuboresha huduma kwa wagonjwa hao.

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya nje (OPD) Dkt. Elimeena Meda amesema mafunzo hayo ni muhimu kwani kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wa kiharusi hivyo ni muhimu watoa huduma wote kujua namna bora ya kuwahudumia wagonjwa hao.

“Tumeona sababu ya kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma kwa wagonjwa wa kiharusi, mafanzo haya yanahusu kada zote zinazoshiriki katika mnyororo wa kuwahudumia wagonjwa wa kiharusi ili kuboresha huduma wanapokuwa hospitalini hadi wanaporuhusiwa” ameongeza Dkt. Meda.

Kwa upande wake, muandaaji wa mafunzo hayo kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Dkt. Sarah Matuja amebainisha kwamba ugonjwa wa kiharusi umekuwa tishio nchini na unawakumba watu wenye umri wa miaka kati ya miaka 40 hadi 60 na hivyo kuathiri nguvu kazi ya jamii.

Mafunzo hayo yanatolewa na wataalamu bingwa wa magonjwa ya kiharusi duniani kuanzia leo Januari 9 hadi Machi 19, 2024 ambapo yatahusisha wakufunzi ambao ni Madaktari Bingwa wa kiharusi duniani na yatafanyika kwa nadharia na vitendo.

No comments:

Post a Comment

 
Copyright © 2016 Shamakala
Designed by Switch International | SHAMAKALA 360
    Twitter Facebook Google Plus Vimeo Videosmall Flickr YouTube