BREAKING

Thursday 3 August 2023

MAKAMU WA RAIS MHE. DKT MPANGO AZINDUA MPANGO WA TATU WA TAIFA WA HUDUMA JUMUISHI ZA FEDHA


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akimsikiliza Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Emmanuel Tutuba akieleza juu ya makundi mbalimbali yaliolengwa kufikiwa na Mpango wa tatu wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha wa 2023-2028 wakati alipowasili katika ukumbi wa BOT Jijini Dar es salaam kuzindua mpango huo leo tarehe 03 Agosti 2023.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa Uzinduzi wa Mpango wa Tatu wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha wa 2023-2028, hafla iliofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania Jijini Dar es salaam leo tarehe 03 Agosti 2023.







Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akipokea kitabu cha Mpango wa tatu wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha wa 2023-2028 kutoka kwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Emmanuel Tutuba mara baada ya kuzindua mpango huo katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania Jijini Dar es salaam leo tarehe 03 Agosti 2023.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akionesha kitabu cha Mpango wa tatu wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha wa 2023-2028 mara baada ya kuzindua mpango huo katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania Jijini Dar es salaam leo tarehe 03 Agosti 2023.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa Baraza la Taifa la Huduma Jumuishi za Fedha mara baada ya kuzindua Mpango wa Tatu wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha wa 2023-2028, hafla iliofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania  Jijini Dar es salaam leo tarehe 03 Agosti 2023. (waliokaa kutoka kulia ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Emmanuel Tutuba, Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba, Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Wiebe de Boer na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Albert Chalamila)

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema huduma jumuishi za fedha ni miongoni mwa vipaumbele vya Nchi pia ni lengo muhimu la Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.

 Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizindua Mpango wa Tatu wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha wa 2023-2028, hafla iliofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania Jijini Dar es salaam. Amesema huduma jumuishi za fedha ni nguzo muhimu inayopaswa kuzingatiwa kwa kuhakikisha watu wa makundi yote wanafikiwa.

 Makamu wa Rais ametoa wito kwa wataalam na wadau wa huduma jumuishi za fedha kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuhakikisha wanaongeza kasi ya upatikanaji wa vitambulisho vya taifa ili kusaidia katika upatikanaji wa huduma rasmi za kifedha hususani kwa vijana. Aidha amewasihi watalaam hao kuhakikisha malengo yaliowekwa katika mpango huo wa tatu wa huduma jumuishi za fedha yanafikiwa kikamilifu ifikapo mwaka 2028 hususani kwa kuelekeza juhudi katika makundi ambayo hayajafikiwa ikiwemo watu wenye ulemavu, wakulima wadogo, wavuvi, vijana, wanawake na wafanyabiashara wadogo.

 Halikadhalika Makamu wa Rais amesema ni vema kuendelea na jitihada za kuimarisha ulinzi wa watumiaji wa huduma za kifedha dhidi ya uhalifu wa mtandaoni ili kuwajengea wateja imani ya kuendelea kutumia huduma hizo. Pia ametoa rai ya kupunguzwa kwa gharama za kutumia huduma rasmi za kifedha pamoja na kuongeza wigo wa dhamana ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo.

Makamu wa Rais ametoa wito wa kuongezwa na kurahisishwa kwa miundombinu ya malipo ya pamoja ili kuchochea matumizi ya huduma rasmi za fedha. Aidha amesema ni muhimu kuhakikisha upatikanaji wa mawasiliano kwa wote ili kupunguza matumizi ya fedha taslimu.

Kwa upande wake Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba amesema Mpango wa Tatu wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha umeandaliwa kwa lengo la kuunganisha sekta binafsi na serikali ili kutatua changamoto za huduma jumuishi za fedha. Amesema mpango huo utasaidia kuongeza uelewa wa masuala ya huduma za fedha na kuongeza matumizi ya simu janja sambamba na kuhakikisha usalama wa wateja.

No comments:

Post a Comment

 
Copyright © 2016 Shamakala
Designed by Switch International | SHAMAKALA 360
    Twitter Facebook Google Plus Vimeo Videosmall Flickr YouTube