BREAKING

Wednesday, 14 February 2018

UKWAA LA NISHATI TANZANIA KUTOA SEMINA KWA WABUNGE



Na Mwandishi Wetu

JUKWAA la Nishati Tanzania linatarajia kutoa semina kwa wabunge ili wapate uelewa wa nishati na changamoto zake, watakapokuwa wanajibu maswali ama kuuliza wafanye hivyo kwa manufaa ya taifa.

Mratibu wa Jukwaa hilo nchini ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Hudson Nkotagu alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu shughuli wanazozifanya.

Profesa Nkotagu alisema wanaamini wabunge wakipata uelewa kuhusu nishati pale watakapokuwa wakijadili masuala hayo bungeni watakuwa na uelewa mpana, na maamuzi yake yatakuwa kwa manufaa ya taifa.

Pia alisema semina hizo zitatolewa kwa viongozi wakuu, watendaji wa serikali kutoka sekta za viwanda, mazingira, serikali za mitaa, wawekezaji pamoja na wafanya biashara mbalimbali.

Alisisitiza kuwa wananchi wengi hawana uelewa wa nishati kwamba kuna za aina mbili, aina ya kwanza inatokana na vyanzo vya nishata ambavyo vikitumika vinapoisha havirudi tena mfano gesi, mafuta, mkaa wa mawe pamoja na urani.

Na aina nyingine ni ile inayotokana na vitu ambavyo vinajiendeleza vyenyewe kiasili kwa mfano nishati ya sola, upepo, maji, mawimbi ya bahari na kuni.

“Nishati hizi zinajiendeleza kiasili. Kwa bahati nzuri zote tunazo katika nchi yetu. Tanzania imejaliwa kuwa na vyanzo vyote vya nishati, vinahitajika tu kuendelezwa,” alisema.

Alisema jukwaa hilo linashirikisha UDSM, Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT), Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST), pamoja na vyuo vikuu vine kutoka nchini Uholanzi ambavyo ni Twente, Ultreacht, Hanze na Delft.

No comments:

Post a Comment

 
Copyright © 2016 Shamakala
Designed by Switch International | SHAMAKALA 360
    Twitter Facebook Google Plus Vimeo Videosmall Flickr YouTube