BREAKING

Wednesday, 14 February 2018

RAIS MSTAAFU MKAPA AONGOZA HARAMBEE YA KUCHANGIA MFUKO WA UDHAMINI WA KUDHIBITI UKIMWI


Rais Mstaafu Benjamin Mkapa akihutubia wakati akiongoza harambee ya kuchangia Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi (ATF) katika hafla iliyofanyika Hoteli ya Serena Dar es Salaam jana usiku.
Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Mheshimiwa Jenista Mhagama akihutubia katika harambee hiyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi,Bw.  Godfrey Simbeye akihutubia.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko akihutubia.
Wasanii wakitoa Burudani katika harambee hiyo
Wadau wakiwa kwenye harambee hiyo.
Makofi yakipigwa meza kuu. Kutoka kushoto ni Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi,  Bw. Godfrey Simbeye na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa Geita Gold Mine (GGM), Bw. Tenga B. Tenga.
Wadau wakiwa kwenye harambee hiyo.
Harambee ikiendelea.
Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa akitoa zawadi ya picha iliyonunuliwa kwa sh. milioni moja katika harambee hiyo.
Rais Mkapa akimkabidhi picha  Salama Mussa kutoka Benki ya NBC baada ya kuinunua katika harambee hiyo. Kulia ni Waziri Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Mheshimiwa Jenista Mhagama na wa pili kushoto ni Mdau Teddy Mapunda mratibu wa harambee hiyo.
Rais Mstaafu, Benjamini Mkapa akimkabidhi picha Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Alvaro Rodriguez baada ya kuinunua katika harambee hiyo.
Rais Mstaafu, Benjamini Mkapa akimkabidhi picha ya simba Mkurugenzi wa Mauzo na Masoko wa Hoteli ya Serena, Bw. Seraphin Lusala baada ya kuinunua kwenye harambee hiyo.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa Geita Gold Mine (GGM),  Bw. Tenga B. Tenga akimkabidhi Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa mfano wa hundi yenye thamani ya sh.milioni 100 zilizo tolewa na mgodi huo kuchangia mfuko huo.


Na Dotto Mwaibale

RAIS Mstaafu Benjamin Mkapa amewataka wadau mbalimbali na wananchi kuendelea kuchangia Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi (ATF) kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo nchini ambapo zaidi ya sh.milioni 200 zilipatikana.

Mkapa alitoa ombi hilo wakati akiongoza harambee ya kuchangia mfuko huo iliyofanyika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam jana na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, wawakilishi wa mashirika ya nje na ndani pamoja na mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini.

"Ni wajibu kwa kila mwananchi na wadau mbalimbali kuendelea kuchangia mfuko huu ili kusaidia mapambano ya Ukimwi hapa nchini na kuwa mapmbano hayo si ya mtu mmoja" alisema Mkapa. 

Katika hatua nyingine Rais Mstaafu Mkapa ameiomba Serikali kuendelea kutenga fedha za Ukimwi katika bajeti zake.

Akizungumza katika harambee hiyo Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Mheshimiwa Jenista Mhagama alisema kwamba Serikali itaendelea kusimamia Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) katika matumizi ya  fedha hizo.

Mhagama alisema asilimia 60 ya fedha hizo zitatumika kununulia madawa, asilimia 25 itatumika katika kutoa huduma za kinga pamoja na kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi mapya ya Ukimwi na asilimia 15 zitatumika  kwa ajili ya uwezeshaji na ufuatiliaji wa programu za Ukimwi.

Mhagama aliongeza kuwa matumizi ya dawa za kufubaza VVU kwa wanawake ni asilimia 92.9 wakati wanaume ni 86.1 na kuwa katika tisini ya tatu kati ya watu wanaoishi na VVU wenye umri wa miaka 15-64 ambao wametoa taarifa kuwa wanatumia dawa za kufubaza VVU asilimia 87.7 ya watu hao inaonyesha kiasi cha VVU kimefubazwa wanawake ni asilimia 89.2 na wanaume ni asilimia 84.

Alisema utafiti huo pia umeonyesha kuwa maambukizo mapya ya VVU (HIV incidence) kwa mwaka kwa watu wenye umri wa miaka 15-64 Tanzania Bara ni asilimia 0.29 ambayo ni sawa na watu 81,000.

Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko huo, Bw. Godfrey Simbeye alisema sekta binafsi imeunga mkono kwa kiasi kikubwa katika kuchangia mfuko huo na kuwa hakutakuwa na matumizi mabaya ya fedha hizo na zitakwenda kutumika kwa kile kilichokusudiwa.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko alimshukuru Rais Mstaafu Mkapa kwa kukubali kushiriki kuongoza harambee hiyo na kueleza kuwa Tacaids imekuwa ikiendesha harambee mbalimbali pamoja na kuandaa mashindano ya michezo na viingilio vyake vimekuwa vikiingia katika mfuko huo.







No comments:

Post a Comment

 
Copyright © 2016 Shamakala
Designed by Switch International | SHAMAKALA 360
    Twitter Facebook Google Plus Vimeo Videosmall Flickr YouTube