BREAKING

Saturday, 14 July 2018

WAZIRI KALEMANI AWASHA UMEME KIJIJI CHA KISANGA

 
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akiwasha umeme katika Kijiji cha Kisanga Kata ya Kisanga wilaya ya Sikonge tarehe 12 Julai, 2018. Wengine wanaoshuhudia ni Viongozi Waandamizi kutoka kwa Mkuu wa Wilaya Sikonge, REA, TANESCO, Wakandarasi pamoja na wananchi.


WAZIRI wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, jana tarehe 12 Julai, 2018   amewasha rasmi umeme  katika kijiji cha Kisanga kata ya Kisanga wilaya ya Sikonge mkoa wa Tabora.
Waziri Kalemani amewasha umeme huo baada ya kufanya uzinduzi wa mradi husika mwaka jana wilayani Sikonge.
“Leo nimekuja kuwasha umeme, kukagua utekelezaji wa mradi wa REA hapa Sikonge na kuwakabizi Wakandarasi ili kumalizia vijiji vilivyobakia,” alisema Waziri Kalemani.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Kalemani alisema kuwa Wilaya ya Sikonge ina jumla ya vijiji 71 na hadi sasa vijiji 30 tayari vina umeme ingawa sio kikamilifu, vijiji 40 vilivyobakia vyote vitapelekewa umeme.
Aliongeza kuwa, mradi huu wa REA III awamu ya kwanza takriban vijiji 26 vitaletewa umeme, vijiji 4 vipo off gridi kwa hiyo vitapatiwa umeme wa Jua (Solar) na vijiji vingine 11 vilivyobakia vitaendelea kuunganishiwa umeme.
“Wakandarasi hawa watawaletea umeme Kijiji kwa Kijiji, Kitongo kwa Kitongoji, Nyumba kwa Nyumba bila kuruka nyumba yoyote” alisisitiza Waziri Kalemani.
Pia, Waziri Kalemani aliendelea kuwahimiza Wafanyakazi wa Halmashauri kutenga pesa kwa ajili ya kuunganishia umeme Taasisi zote za Umma.
Alisema kuwa, ikiwa suala la kutenga pesa hiyo itakuwa ngumu basi, Ofisi zenye chumba kimoja hadi vitatu wekeni kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) ambacho hakihitaji wiring ili taasisi zote za umma zipate nishati hii ya umeme.
Aidha kwa upande wake, Naibu Waziri wa TAMISEMI, Joseph Kakuda ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Sikonge alimshukuru sana Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani kwa ushirikiano mkubwa anaoendelea kumpa na kusema kuwa wananchi wa Sikonge wanahitaji umeme ili kuendelea kufungua Viwanda vidogo vidogo na hata kuboresha kipato cha kiuchumi katika miongoni mwao.

  Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akijiandaa kukata utepe na kuwasha umeme katika Kijiji cha Kisanga. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa TAMISEMI, Joseph Kakuda ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Sikonge.

  Wananchi wa kijiji cha Kisanga wakisalimia viongozi waliofika katika kijiji hicho.

  Kamishna wa Nishati, Mhandisi Innocent Luoga akiwasalimia wananchi katika mkutano huo wa kuwasha umeme katika kijiji cha Kisanga Kata ya Kisanga.


Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini, Gidion Kaunda akiwasalimia wananchi kabla ya zoezi la kuwasha umeme.

No comments:

Post a Comment

 
Copyright © 2016 Shamakala
Designed by Switch International | SHAMAKALA 360
    Twitter Facebook Google Plus Vimeo Videosmall Flickr YouTube