BREAKING

Thursday, 5 July 2018

DKT TIZEBA AKABIDHIWA MATREKTA 500 YA URSUS NA WAZIRI MKUU

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim M. Majaliwa (Mb) akimkabidhi hati ya makabidhiano Waziri wa kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba  ya matrekta 500 yaliyonunuliwa na wadau mbalimbali wa kilimo nchini katika maonyesho ya 42 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es salaam Julai 4, 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal-WK)
Waziri  Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe  ikiwa ni ishara ya kukabidhi matrekta 560 yaliyonunuliwa na wadau mbalimbali wa kilimo nchini katika maonyesho ya 42 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es salaam Julai 4, 2018.  Watatu kulia ni Waziri wa Viwanda, Biashara ya Uwekezaji, Charles Mwijage, Wapili kulia ni Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba na kulia ni Naibu Waziri wake, Dkt, Mary Mwanjelwa
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Waziri wa kilimo Dkt Charles Tizeba Kitabu cha Mwongozo wa Taratibu za Kujenga Kiwanda Nchini Tanzania baada ya kufungua Maonyesho ya 42 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es salaam Julai 4, 2018. 


Waziri wa kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba (Mwenye maiki) akizungumza kabla ya kukabidhiwa matrekta 500 yaliyonunuliwa na wadau mbalimbali wa kilimo nchini katika maonyesho ya 42 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es salaam Julai 4, 2018.  
Waziri  Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe  ikiwa ni ishra ya kukabidhi matrekta 560 yaliyonunuliwa na wadau mbalimbali wa kilimo nchini katika maonyesho ya 42 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es salaam Julai 4, 2018.  Watatu kulia ni Waziri wa Viwanda, Biashara ya Uwekezaji, Charles Mwijage na kushoto ni Naibu Waziri wake, Mhandishi Stella Manyanya. Wapili kulia ni Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba na kulia ni Naibu Waziri wake, Dkt, Mary Mwanjelwa


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) leo 4 Julai 2018 amemkabidhi Waziri wa kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba jumla ya matrekta 500 yatakayopelekwa kwa vyama vya ushirika vya msingi ili wakulima kunufaika na tija katika kilimo hususani zao la Pamba.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo yaliyofanyika wakati wa uzinduzi wa maonesho ya 42 ya sabasaba katika viwanja vya Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es salaam, Mhe. Dkt Tizeba alisema kuwa sekta ya kilimo nchini bado inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo tija ndogo inayosababishwa na matumizi madogo ya pembejeo, huduma duni za ugani na matumizi ya zana duni za kilimo ambapo wakulima wengi wanatumia majembe ya mkono au kutumia maksai wakati wa kulima.

“Katika kilimo cha Pamba msimu wa mwaka 2017/2018 ushahidi unaonyesha kwamba wakulima walichelewa kuanza kuandaa mashamba yao kwa sababu Maksai wakati wa kiangazi wanadhoofu sana, na mara mvua inaponyesha hawawezi kulima mpaka majani yawe mengi ndio wapate nguvu za kuanza kulima, hali hii inaondoa uwezekano wa wakulima kutumia teknolojia mpya katika kilimo kama vile kilimo hifadhi ambacho kimedhihirika kuongeza tija zaidi ya mara mbili” Alikaririwa Mhe Dkt. Tizeba

Aliitaja mikoa itakayoanza kunufaika na mpango huo katika awamu hii ya kwanza kuwa ni pamoja na Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Tabora na Geita, awamu ya pili ikijumuisha mikoa ya Singida, Kagera, na Kigoma huku awamu ya tatu ikitarajiwa kuhusisha mikoa ya Kanda ya Mashariki kwa kuzingatia ongezeko la uzalishaji wa pamba katika maeneo hayo.

Mhe Tizeba alisema mtazamo wa mpango huo ni kuunganisha nguvu za mkulima mmoja mmoja ili kuharakisha kuleta maendeleo yao ambapo utatekelezwa kwa kutumia sehemu ya fedha zinazolipwa AMCOS kama kamisheni ya kusimamia ununuzi wa pamba ambapo matarajio ni kukusanya Bilioni 6 kama uzalishaji wa pamba utafika kilo milioni 400 kwa mwaka.

Mhe. Dkt Tizeba alimuhakikishia Waziri Mkuu kuwa Wizara ya kilimo itatekeleza mpango huo kupitia kwa Mrajis na Bodi ya Pamba ambapo kutakuwa na vituo vinane (8) vya kusimamia Trekta hizo huku kituo kimoja kikiwa ni kwa kila mkoa na viwili kwa mikoa mikubwa inayozalisha pamba kwa wingi.

Aidha, alisema kuwa vituo vitatoa mafunzo kwa madereva na vitafuatilia matengenezo na ushauri wa kitaalamu kuhusu usimamizi wa zana hizo ambapo hadi sasa wizara ya kilimo imepeleka wahandisi wanne (4) na wengine wawili (2) watapelekwa hivi karibuni katika kituo cha kuunganisha matrekta kilichopo Wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani ambapo lengo ni kuwapa uzoezfu na uelewa mpana wa kitaalamu wa usimamizi wa matrekta hayo.

Aliongeza kuwa ili kufanikisha azma hiyo ya kimapinduzi itafanya kazi kwa ufasaha na wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri ili utekelezaji uweze kupata mafanikio na kufanikisha mtazamo wa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli katika hatua anazozichukua za kuboresha kilimo nchini ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika sherehe hizo Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa amemkabidhi  waziri wa kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba matrekta 500 ya Ursus kwa ajili ya wateja wa mwanzo katika awamu ya kwanza ya uunganishaji wa matrekta maalumu kwa ajili ya shughuli za kilimo vijijini huku Jeshi la Magereza likikabidhiwa matrekta 50 na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) Matrekta 10.

No comments:

Post a Comment

 
Copyright © 2016 Shamakala
Designed by Switch International | SHAMAKALA 360
    Twitter Facebook Google Plus Vimeo Videosmall Flickr YouTube