BREAKING

Thursday, 26 July 2018

KUMBUKUMBU YA SIKU YA MASHUJAA, AMANI NA UZALENDO KWA TAIFA LETU


Leo ni Julai 25 siku ya Maadhimisho ya Mashujaa waliopambana kwa hali na mali kutetea nchi yetu ya Tanzania katika maeneo mbalimbali.

Hawa walimea uzalendo mkubwa, mwili na nafsi zao walikubali kuviweka rehani kwa ajili ya Tanzania. Bado tunawakumbuka na kuwaombea kheri kutokana na kujali na kudumisha misingi ya amani.

Misingi mizuri iliyojengwa na waasisi wa Taifa, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume , imesababisha Wananchi wa Tanzania kwa muda mrefu kuishi kwa amani na utulivu, huku wakifanya mambo yao kwa uhuru bila ya kuingiliwa na mtu yeyote wa ndani ama wa nje.

Tofauti na mataifa mengine, Watanzania wako huru zaidi kwenda kokote wanakotaka na hata kuishi ama kufanya kazi au biashara bila ya bughudha yeyote endapo kanuni, taratibu na sheria za nchi zitafuatwa ama kuzingatiwa vyema. Hali hiyo ni tofauti kabisa na nchi nyingine zikiwamo zile za jirani zetu kama Kenya, Rwanda, Burundi, Kongo na hata Uganda, nchi ambazo kwa kiasi kikubwa ukabila na chokochoko za kisiasa zimetamalaki kuanzia ngazi za kijiji hadi Taifa. Hapa kwetu tumeishi kama Ndugu bila ya u-rangi, udini, ukabila wala harakati za kiitikadi na kisiasa kutugawa.
Jambo la kushangaza ni kuwa misingi hiyo ya amani na utulivu iliyogharamikiwa na Waasisi wetu, hivi sasa ipo shakani na hatarini kutoweka kwani ilishaanza kuchezewa na chokochoko za aina mpya ya siasa (kwa maana ya ukosefu wa uvumilivu na uchu wa madaraka) iliyoanza kurindima katika siku za hivi karibuni.

Tukiwa tunawakumbuka Mashujaa hao inabidi nasi tujitathmini nafasi yetu kwa Taifa letu endapo inaedana na hali ya uzalendo. Hali ilivyo sasa kiwango cha uzalendo kimeshuka sana. Mtu yupo radhi kulalamika na kudai haki pasipo kutimiza wajibu wake kwa Taifa. Wameshajiuliza, wamelifanyia nini Taifa kabla ya kudai haki?

Vijana walio wengi wameweka pembeni uzalendo wa kulipenda Taifa lao kiasi cha kufikia hatua ya kukufuru kwa maneno ya kashfa dhidi ya Taifa lao. Hali hiyo ni tofauti kabisa na mataifa mengine ambayo hatuoni wakiyakashifu mataifa yao hadharani. Hii tabia ya kujivua nguo hadharani ni kwa faida ya nani?

Hapo hapo utakuta kuna baadhi ya Watanzania wanenda nchi za kimataifa na kuanza kuikashfu nchi yao kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vya kimataifa. Laiti kama Wazee wetu waliotutangulia wangekuwa na akili mbovu kama hizi, leo hii sidhani kama tungelikuta Taifa hili likiwa salama kama lilivyo. Umejiuliza haya ya kulichafua Taifa letu unataka uache urithi gani kwa vizazi vijavyo kwa Taifa letu?

Vijana wengi wa Leo, wananyooshewa vidole kwa kutothamini tunu ya kuwa Mtanzania. Je, U-Miongoni mwao? Kwako uzalendo ni nini? Kwako amani unailindaje?

Ndugu zangu, Wapo wanaosema kuwa amani ni sawa na yai mkononi, ukilivunja hautaweza kuliunganisha kamwe; wengine wanasema kuwa amani haina bei na ikipotea haina soko la kununua. Tuitunze amani yetu na kamwe tusiizoee wala kuichoka, tuige uzalendo waliokuwa nao Mashujaa wetu ambao walihakikisha amani ya nchi wanailinda vilivyo kwa machozi, jasho na damu.

No comments:

Post a Comment

 
Copyright © 2016 Shamakala
Designed by Switch International | SHAMAKALA 360
    Twitter Facebook Google Plus Vimeo Videosmall Flickr YouTube