BREAKING

Monday, 30 July 2018

NGULI WA MUZIKI AFRIKA YVONNE CHAKA CHAKA KUFANYA KAZI NA MSANII TANZANIA

Yvonne Chakachaka kufanya kazi na msanii mwingine kutoka Tanzania.



Miezi kadhaa iliyopita King wa Bongo Flava Ali Kiba alitangaza rasmi ujio wa ngoma yake na mwanamuziki mkongwe, maarufu na wa zamani kutoka Afrika ya Kusini Yvonne Chakachaka. Hii ilikuwa ni hatua muhimu sana ya kimuziki kwa nguli huyo wa muziki kutoka Tanzania katika juhudi za kuutangaza muziki wa Tanzania nje ya mipaka, lakini pia kuuthibitisha umma juu ya uwezo wake kimuziki. 

Lakini inaonekana kwamba Yvonne Chakachaka aliyetamba na nyimbo kama "Mama Afrika", "Thank you Mr. Dj" na "Umqombothi" miaka ya 80, amevutiwa sana na muziki wa Bongo na hivyo kuwa tayari kufanya kazi na wasanii wengine kutoka hapa nchini. Hii inathibitika baada ya hivi karibuni, kupitia account yake ya instagram kuonesha kuwa yuko studio na moja ya wasanii wa Tanzania, Otuck William, wakirekodi wimbo. Legend huyo wa muziki wa Africa AKA "The Princess of Africa" aliandika, "Spending some time with my son @otuck_william in Kigali, doing some work for the youth. Day well spent, thank you @mrmingz". 

Yvonne Chakachaka alikua jijini Kigali, nchini Rwanda kwa ajili ya onesho na kukutana na Otuck, ambaye pia alikua huko kwenye shughuli zake za kikazi na kimuziki, hivyo tutegemee kikubwa kutoka kwa hivi vichwa viwili. Otuck ni msanii mkongwe wa RnB nchini anayetambulika sana na ngoma zake kama Deja Vu, Roho Juu alitomshirikisha Heri Muziki na So Cold aliyoitoa hivi karibuni. 

Thursday, 26 July 2018

SIMBA WAPAMBANA NA MVUA KUBWA UTURUKI.....


Mvua  kubwa yenye ukungu uliopita kiasi, radi na ngurumo za kutisha, juzi vilisitisha mazoezi ya mab­ingwa wa Tanzania, Simba.

Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems alilazimika kusitisha mazoezi na kuondoa kikosi chake uwanja­ni wakati wa mazoezi ya asubuhi kutokana na mvua hiyo kubwa.

Hali ya hewa ilianza kubadilika taratibu wakati Simba wakijifua na ukungu ukaanza kutanda uki­washangaza wachezaji na benchi la ufundi.

Lakini ghafla, wakati mazoezi yakiendelea mvua kubwa ilianza kunyesha na kusababisha kocha huyo Mbelgiji kusitisha mazoezi.

Kocha mpya wa viungo wa Simba, Adel Zrane alishindwa kuendelea na kazi yake ikiwa ndiyo siku ya kwanza ameanza kazi.

Aussems ali­waambia wache­zaji wake, mazoezi ya jana jioni wangeangalia hali ya hewa. Kama bado ingeen­delea kutishia amani, basi ratiba ingebadilika na kuwa gym kwa kuwa katika eneo la Kartepe gym iko katika vyumba vilivyo chini ya ardhi yani underground.

KUMBUKUMBU YA SIKU YA MASHUJAA, AMANI NA UZALENDO KWA TAIFA LETU


Leo ni Julai 25 siku ya Maadhimisho ya Mashujaa waliopambana kwa hali na mali kutetea nchi yetu ya Tanzania katika maeneo mbalimbali.

Hawa walimea uzalendo mkubwa, mwili na nafsi zao walikubali kuviweka rehani kwa ajili ya Tanzania. Bado tunawakumbuka na kuwaombea kheri kutokana na kujali na kudumisha misingi ya amani.

Misingi mizuri iliyojengwa na waasisi wa Taifa, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume , imesababisha Wananchi wa Tanzania kwa muda mrefu kuishi kwa amani na utulivu, huku wakifanya mambo yao kwa uhuru bila ya kuingiliwa na mtu yeyote wa ndani ama wa nje.

Tofauti na mataifa mengine, Watanzania wako huru zaidi kwenda kokote wanakotaka na hata kuishi ama kufanya kazi au biashara bila ya bughudha yeyote endapo kanuni, taratibu na sheria za nchi zitafuatwa ama kuzingatiwa vyema. Hali hiyo ni tofauti kabisa na nchi nyingine zikiwamo zile za jirani zetu kama Kenya, Rwanda, Burundi, Kongo na hata Uganda, nchi ambazo kwa kiasi kikubwa ukabila na chokochoko za kisiasa zimetamalaki kuanzia ngazi za kijiji hadi Taifa. Hapa kwetu tumeishi kama Ndugu bila ya u-rangi, udini, ukabila wala harakati za kiitikadi na kisiasa kutugawa.
Jambo la kushangaza ni kuwa misingi hiyo ya amani na utulivu iliyogharamikiwa na Waasisi wetu, hivi sasa ipo shakani na hatarini kutoweka kwani ilishaanza kuchezewa na chokochoko za aina mpya ya siasa (kwa maana ya ukosefu wa uvumilivu na uchu wa madaraka) iliyoanza kurindima katika siku za hivi karibuni.

Tukiwa tunawakumbuka Mashujaa hao inabidi nasi tujitathmini nafasi yetu kwa Taifa letu endapo inaedana na hali ya uzalendo. Hali ilivyo sasa kiwango cha uzalendo kimeshuka sana. Mtu yupo radhi kulalamika na kudai haki pasipo kutimiza wajibu wake kwa Taifa. Wameshajiuliza, wamelifanyia nini Taifa kabla ya kudai haki?

Vijana walio wengi wameweka pembeni uzalendo wa kulipenda Taifa lao kiasi cha kufikia hatua ya kukufuru kwa maneno ya kashfa dhidi ya Taifa lao. Hali hiyo ni tofauti kabisa na mataifa mengine ambayo hatuoni wakiyakashifu mataifa yao hadharani. Hii tabia ya kujivua nguo hadharani ni kwa faida ya nani?

Hapo hapo utakuta kuna baadhi ya Watanzania wanenda nchi za kimataifa na kuanza kuikashfu nchi yao kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vya kimataifa. Laiti kama Wazee wetu waliotutangulia wangekuwa na akili mbovu kama hizi, leo hii sidhani kama tungelikuta Taifa hili likiwa salama kama lilivyo. Umejiuliza haya ya kulichafua Taifa letu unataka uache urithi gani kwa vizazi vijavyo kwa Taifa letu?

Vijana wengi wa Leo, wananyooshewa vidole kwa kutothamini tunu ya kuwa Mtanzania. Je, U-Miongoni mwao? Kwako uzalendo ni nini? Kwako amani unailindaje?

Ndugu zangu, Wapo wanaosema kuwa amani ni sawa na yai mkononi, ukilivunja hautaweza kuliunganisha kamwe; wengine wanasema kuwa amani haina bei na ikipotea haina soko la kununua. Tuitunze amani yetu na kamwe tusiizoee wala kuichoka, tuige uzalendo waliokuwa nao Mashujaa wetu ambao walihakikisha amani ya nchi wanailinda vilivyo kwa machozi, jasho na damu.

Monday, 23 July 2018

SIMBA WAANZA KUJIFUA UTURUKI CHINI YA KOCHA MPYA MBELGIJI PATRICK AUSSEMS




Kikosi  cha Simba SC kimewasili salama mjini Istanbul, Uturuki baada ya kuondoka Aflajiri ya Jumapili kuweka kambi ya muda wa wiki mbili kujiandaa na Ligi Kuu ya Tanzania bara inayotarajiwa kuanza Agosti 22, mwaka huu.

Na mara baada ya kuwasili, Simba SC walipumzika kidogo kabla ya kwenda kufanya mazoezi yao ya kwanza jioni ya leo Istanbul ambayo pia yalikuwa mazoezi ya kwanza chini ya kocha mpya, Mbelgiji Patrick J Aussems. 

Simba SC imeondoka na wachezaji wote iliyowasajili kwa ajili ya msimu ujao chini ya kocha wake mpya Aussems atakayekuwa chini ya Msaidizi Mrundi, Masoud Juma aliyekuwa Msaidizi pia wa makocha wawili waliopita, Mcameroon Joseph Omog na Mfaransa, Pierre Lechantre.

Ikiwa nchini Uturuki, Simba SC itapata mazoezi katika mazungira na viwanja bora, pamoja na mechi za kirafiki za kujipima nguvu kabla ya kurejea nchini kwa ajili ya tamasha la Simba Day Agosti 8 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.

Ikumbukwe Simba SC, mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania watauanza msimu kwa mchezo wa wa Ngao ya Jamii dhidi ya washindi wa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu Azam Sports Federation Cup (ASFC), Mtibwa Sugar Agosti 18, mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.  
             
Katika Ligi Kuu, Simba itaanza na Tanzania Prisons Agosti 22, mechi itakayochezwa Saa 1:00 usiku Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.

Na watakutana na mahasimu wao wa jadi, Yanga watakutana Septemba 30, mwaka huu katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kuanzia Saa 10:00 jioni Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

MAKAMU WA RAIS AENDELEA NA ZIARA MKOANI SONGWE...

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan yupo  Mkoani Songwe katika  ziara ya kikazi ya siku tano.

Thursday, 19 July 2018

DSTV WALIVYOJIACHIA WAKATI WA UZINDUA WA MSIMU WA TATU WA HARUSI YETU






Kampuni ya Multichoice Tanzania jioni ya leo imezindua msimu mpya wa Kipindi cha Harusi yetu ambacho hurushwa katik king’amuzi chake kwenye chanel namba 160.


Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa chaneli ya Maisha Magic Bongo,  Barbara Kambogi, alisema baada ya kipindi hicho kuonekana kuwa na mashabiki wengi ambao walikuwa wakikifuatilia kwa ukaribu zaidi wamelazimika kuzindua sehemu hiyo ya tatu  ili waweze kuwaonyesha mauzui bora zaidi.

Pamoja na uzinduzi huo pia Kambogi ameeleza kuwa kwa muda wote sasa watakuwa wakiendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na waigizaji wote nchini ili waweze kuitumia chanel hiyo kutangaza kazi zao.



Kwakuanza sasa wana vipindi kibao ambavyo hurusha tamthiria mbalimbali na filamu za hapa nchini na pia kuna tamthilia nzuri za wasanii wa kitanzania kama vile Uber na mwantumu ambazo kwa pamoja zinafanya vyema.


 





 

Saturday, 14 July 2018

MOTO HAUZIMWI DSTV .........

MOTO HAUZIMWI……….

Kutoka DStv tunakuambia hivi, moto hauzimwii

Utakuwa ni wakati wa burudani ya aina yake ,kuanzia Julai 13 hadi 31, kila mteja wa DStv ambaye akaunti yake iko hewani atazawadiwa chaneli zote za michezo na za Watoto buree kabisa!

Amini usiamini…., utashuhudia mieleka na mbio za magari za langalanga(Formula 1) kupitia Supersport 1,2,3,4,5,6,7 na 8.

Ofa hii haijawaacha Watoto kwani nao wataweza kushuhudia katuni mpya za peppa pig/munki and trunk na cloudy with a chance of meetballs kupitia Cartoon network, Disney, Nickleodeon na Cbeebies.

Hii si ya kukosa…….. au vipi?

Hakikiksha tu akaunti yako haijakatika na kama imeatika wahi kulipia akauti yako leo usipitwe na of a hii ya aina yake!

Kumbuka ni chaneli zote za Supersport na katuni (Watoto) bila kijali kifurushi ulichopo.Unangoja nini?


#KamaSioDStvPotezea

WAZIRI KALEMANI AWASHA UMEME KIJIJI CHA KISANGA

 
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akiwasha umeme katika Kijiji cha Kisanga Kata ya Kisanga wilaya ya Sikonge tarehe 12 Julai, 2018. Wengine wanaoshuhudia ni Viongozi Waandamizi kutoka kwa Mkuu wa Wilaya Sikonge, REA, TANESCO, Wakandarasi pamoja na wananchi.


WAZIRI wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, jana tarehe 12 Julai, 2018   amewasha rasmi umeme  katika kijiji cha Kisanga kata ya Kisanga wilaya ya Sikonge mkoa wa Tabora.
Waziri Kalemani amewasha umeme huo baada ya kufanya uzinduzi wa mradi husika mwaka jana wilayani Sikonge.
“Leo nimekuja kuwasha umeme, kukagua utekelezaji wa mradi wa REA hapa Sikonge na kuwakabizi Wakandarasi ili kumalizia vijiji vilivyobakia,” alisema Waziri Kalemani.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Kalemani alisema kuwa Wilaya ya Sikonge ina jumla ya vijiji 71 na hadi sasa vijiji 30 tayari vina umeme ingawa sio kikamilifu, vijiji 40 vilivyobakia vyote vitapelekewa umeme.
Aliongeza kuwa, mradi huu wa REA III awamu ya kwanza takriban vijiji 26 vitaletewa umeme, vijiji 4 vipo off gridi kwa hiyo vitapatiwa umeme wa Jua (Solar) na vijiji vingine 11 vilivyobakia vitaendelea kuunganishiwa umeme.
“Wakandarasi hawa watawaletea umeme Kijiji kwa Kijiji, Kitongo kwa Kitongoji, Nyumba kwa Nyumba bila kuruka nyumba yoyote” alisisitiza Waziri Kalemani.
Pia, Waziri Kalemani aliendelea kuwahimiza Wafanyakazi wa Halmashauri kutenga pesa kwa ajili ya kuunganishia umeme Taasisi zote za Umma.
Alisema kuwa, ikiwa suala la kutenga pesa hiyo itakuwa ngumu basi, Ofisi zenye chumba kimoja hadi vitatu wekeni kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) ambacho hakihitaji wiring ili taasisi zote za umma zipate nishati hii ya umeme.
Aidha kwa upande wake, Naibu Waziri wa TAMISEMI, Joseph Kakuda ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Sikonge alimshukuru sana Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani kwa ushirikiano mkubwa anaoendelea kumpa na kusema kuwa wananchi wa Sikonge wanahitaji umeme ili kuendelea kufungua Viwanda vidogo vidogo na hata kuboresha kipato cha kiuchumi katika miongoni mwao.

  Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akijiandaa kukata utepe na kuwasha umeme katika Kijiji cha Kisanga. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa TAMISEMI, Joseph Kakuda ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Sikonge.

  Wananchi wa kijiji cha Kisanga wakisalimia viongozi waliofika katika kijiji hicho.

  Kamishna wa Nishati, Mhandisi Innocent Luoga akiwasalimia wananchi katika mkutano huo wa kuwasha umeme katika kijiji cha Kisanga Kata ya Kisanga.


Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini, Gidion Kaunda akiwasalimia wananchi kabla ya zoezi la kuwasha umeme.

Friday, 13 July 2018

DKT TIZEBA AITAKA CRDB KULIPA FEDHA ZA USHIRIKA (KCU)



Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba akisisitiza jambo wakati akizungumza na wadau wa Kahawa Wilayani Muleba wakati wa ziara ya siku tatu ya kikazi Mkoani Kagera, Jana 12 Julai 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal-WK)
Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba akisalimiana na Mbunge wa Jimbo la Muleba kusini Mhe. Prof Anna Tibaijuka kabla ya mkutano na wadau wa Kahawa Wilayani Muleba wakati wa ziara ya siku tatu ya kikazi Mkoani Kagera, Jana 12 Julai 2018.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage akimakabidhi muongozo wa ujenzi wa viwanda Mkuu wa Wilayani ya Muleba Mhe Richard Ruyango mara baada ya kuwasili Wilayani humo kwa ajili ya mkutano wa wadau wa Kahawa wakati wa ziara ya siku tatu ya kikazi Mkoani Kagera, Jana 12 Julai 2018. Mwingine pichani ni Mkurugenzi wa viwanda vidogo na biashara ndogo kutoka Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dkt Consolata Ishebali.
Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba akisisitiza jambo wakati akizungumza na wadau wa Kahawa Wilayani Muleba wakati wa ziara ya siku tatu ya kikazi Mkoani Kagera, Jana 12 Julai 2018. 

Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba Jana 12 Julai 2018 ameitaka Benki ya CRDB kulipa haraka malipo ya fedha za Ushirika za Chama Kikuu cha Kagera (KCU) kulingana na hatma ya kesi iliyokuwa mahakamani mwaka 2003 ambapo wakulima walikuwa wakikatwa kiasi cha shilingi 10 kwa kila kilo moja ya Kahawa ili kujenga mfuko wa Mazao kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 1990 hadi 1993.

Dkt Tizeba ametoa agizo hilo wakati akizungumza kwenye mkutano uliowakutanisha wadau wa Kahawa Wilayani Muleba ikiwa ni siku ya tatu ya ziara ya kikazi mkoani Kagera iliyoanza Juzi 10 Julai 2018 na kuhudhuriwa pia na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Charles Mwijage.

Swala la madai hayo katika mkutano huo liliibuka baada ya baadhi ya wakulima kuonyesha vitabu vya mfuko huo ambapo makato hayo ya shilingi 10 kwa kilo kwa kipindi cha miaka mitatu jinsi ambavyo yalikuwa yakifanyika.

Madai ya wakulima hao yamekuwa yakilalamikiwa kwa kipindi kirefu na kuchangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa imani ya wakulima kwa chama kikuu cha ushirika Kagera (KCU).

Chanzo cha kesi hiyo ni baada ya Benki ya CRDB kuzuia fedha za malipo yaliyotokana na mauzo ya Kahawa ili kulipia deni la msimu wa mwaka 1997/1998.

Hukumu ya kesi iliyotolewa tarehe 28 Octoba 2009 na mfuko wa Mazao wa wakulima Mkoani Kagera kupewa tahfifu ulizoomba ambapo tangu wakati huo Benki ya CRDB iliweza kulipa fedha za mfuko ilizochukua kiasi cha shilingi milioni 525 na fedha zilizobaki bado hazijalipwa kwa kisingizio cha kuwa na nia ya kukata rufaa ambayo bado haijakatwa ambapo hata hivyo hawawezi kukata rufaa kutokana na muda kuwa umepita.

Dkt Tizeba alisema kuwa Jumla ya madai hayo sambamba na riba ni shilingi Bilioni sita za kitanzania huku akisisitiza kuwa Benki hiyo ya CRDB inapaswa kuwa mfano wa Benki zingine nchini hivyo kushindwa kuwalipa wakulima kwa wakati ni kushindwa kwenda na serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli.

Wakati huo huo Waziri Tizeba aliagiza Halmashauri zote nchini zinazolima Kahawa kusimamia ukusanyaji wa Kahawa kwenda vya Msingi (AMCOS) kwani kutokana na usimamizi huo ndio hupata ushuru wa Halmshauri.

Monday, 9 July 2018

DKT TIZEBA NA DKT MABULA WAMALIZA MGOGORO WA ARDHI WA CHAMA CHA USHIRIKA ULIODUMU KWA MIAKA 17


Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akizungumza jambo kwa msisitizo wakati wa mkutano wa utatuzi wa mgogoro baina ya Chama Cha Ushirika Nyamatongo dhidi ya Mwenyekiti wa kijiji cha Nyamatongo Ndg Itembwe Mnana uliodumu kwa miaka 17, Kushoto ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula, Leo 8 Julai 2018. 

Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akizungumza na wazee kijijini Nyamatongo wakati wa mkutano wa utatuzi wa mgogoro baina ya Chama Cha Ushirika Nyamatongo dhidi ya Mwenyekiti wa kijiji cha Nyamatongo Ndg Itembwe Mnana uliodumu kwa miaka 17, Leo 8 julai 2018.
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba, Naibu waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula  wakiwa katika picha ya pamoja na wananchi wa kijiji cha Nyamatongo mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa utatuzi wa mgogoro baina ya Chama Cha Ushirika Nyamatongo dhidi ya Mwenyekiti wa kijiji cha Nyamatongo Ndg Itembwe Mnana uliodumu kwa miaka 17, Leo 8 Julai 2018.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula akizungumza jambo wakati wa mkutano wa utatuzi wa mgogoro baada ya Chama Cha Ushirika Nyamatongo dhidi ya Mwenyekiti wa kijiji cha Nyamatongo Ndg Itembwe Mnana uliodumu kwa miaka 17, Leo 8 Julai 2018.
Mwenyekiti wa kijiji cha Nyamatongo Ndg Itembwe Mnana (Kushoto) akisalimiana na Mwenyekiti wa Chama cha ushirika Nyamatongo Ndg Willium Elikana mara baada ya kuridhia mgogoro kumalizika.

Na Mathias Canal, Sengerema-Mwanza

Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba pamoja na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula wametatua mgogoro baina ya Chama Cha Ushirika Nyamatongo dhidi ya Mwenyekiti wa kijiji cha Nyamatongo Ndg Itembwe Mnana uliodumu kwa miaka 17.

Mgogoro huo umemalizika kwa maelewano ya pande zote mbili kuwa na kauli moja ambapo Mwenyekiti wa kijiji hicho amekubali kuketi meza moja na Uongozi wa chama hicho cha ushirika ili kukubaliana namna bora ya kuchochea Maendeleo katika kijiji na Taifa kwa ujumla badala ya kuendeleza mgogoro usiokuwa na maslahi kwa pande zote.

Alisisitiza umuhimu wa ushirika nchini ambapo aliwaeleza wananchi hao kutoendeleza vita ya kutokuwa na maelewano kwani kufanya hivyo kunarudisha nyuma shughuli za Maendeleo ya kijiji na Taifa kwa ujumla wake.

Pia, Dkt Tizeba ametangaza Kiama kwa maafisa ugani wanaokaa maofisini badala ya kuwasaidia wakulima kwenye hatua muhimu za uandaaji wa shamba na hatimaye wakati wa Kilimo.

Katika mkutano huo Naibu Waziri wa Ardhi, nyumba na Maendeleo ya makazi Mhe Dkt Angelina Mabula aliwataka wananchi hao kuwa na utamaduni wa kuketi pamoja na kujadili changamoto zinazowakabili ili kuzitatua kwa manufaa yao binafsi na Taifa kwa ujumla.

Alisisitiza kuwa migogoro kama hiyo haihitaji sintofahamu ya mashitaka ya muda mrefu kwani kufanya hivyo ni kutengeneza uhasama usio kuwa na sababu ilihali wote ni watanzania.

Dkt Mabula aliongeza kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli imekusudia kutatua changamoto zote zinazohusisha wananchi katika migogoro ya ardhi pamoja na kadhia zingine zote.

Mgogoro huo ambao ulianza tangu mwaka 2001 umekuwa na hatua za kushitakiana baina ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyamatongo dhidi ya Chama cha ushirika Nyamatongo katika maeneo mbalimbali tangu mwaka 2001 ambapo awali ulitolewa maamuzi katika ngazi ya baraza la kijiji baadae baraza la kata na hatimaye Baraza la Ardhi la Wilaya ya Sengerema ambalo ndilo liliamua kuvunja maamuzi yote ya baraza la kijiji na Kata ili kuanza upya usikilizwaji wa kesi hiyo.

Mara baada ya kumalizika kwa mgogoro huo wananchi kijijini hapo wamempongeza Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba pamoja na Naibu Waziri wa Ardhi, nyumba na Maendeleo ya makazi Mhe Dkt Angelina Mabula kwa kuzuru kijijini hapo hatimaye kutatua mgogoro huo ambao umekuwa sugu kwa miaka 17.

Aidha, katika mkutano huo wananchi wamepata nafasi ya kueleza kero mbalimbali zinazowakabili kijijini hapo ikiwemo ukosekanaji wa maji safi na salama, huku wengine wakieleza kusikitishwa na maafisa ugani kuketi maofisini pasina kuzuru kwa wakulima ili kuwafundisha mbinu bora za Kilimo.

 
Copyright © 2016 Shamakala
Designed by Switch International | SHAMAKALA 360
    Twitter Facebook Google Plus Vimeo Videosmall Flickr YouTube