Kampuni ya MultiChoice Tanzania imetoa msaada wa jumla ya shilingi milioni 120 kwa ajili ya ukamilishaji wa nyumba za waalimu katika shulya Sekondari Kizimkazi iliyopo Kusini Unguja. Msaada huo utawezesha kukamilishwa kwa nyumba mbili za waalimu katika shule hiyo ambapo ujenzi wake ulikwama kutokana na ukosefu wa fedha.
Akizungumza katika hafla fupi ya kuingia mkataba wa ufadhili huo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kusini Diwani Juma Mussa amesema ujenzi wa nyumba utasaidia kupunguza tatizo la nyumba za walimu katika shule hiyo ambapo baadhi ya walimu hulazimika kukaa mbali na shule kutokana na ukosefu wa nyumba za walimu shuleni hapo. Amesema msaada huo unaotolewa na MultiChoice utawezesha mradi huo kukamilika kabisa ikiwemo kuwekwa kwa huduma muhimu kama umeme na maji.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kusini Unguja Juma Musa akizumgumza wakati wa hafla hiyo. Kulia ni mkuu wa mawasiliano wa MultiChoice Tanzania na kushoto ni Mkurugenziwa Halmashauri ya wilaya ya Kusini Kassim Mtoro. Hafla hiyo ilifanyika halmashauri ya wilaya Kusini Unguja.
Amesema ufadhili wa MultiChoice umekuja kwa wakati muafaka kwani kwani halmashauri yake ipo katika mkakati wa kuimarisha sekta za kijamii ikiwemo elimu. “Tumefurahishwa sana na ufadhili huu wa MultiChoice na tunatoa shukrani za pekee kwa kampuni hii kwa kukubali kushirikiana nasi katika kuimarisha sekta ya elimu” alisema Juma na kuongeza kuwa halmashauri yake itahakikisha fedha hizo zinatumika kwa jinsi zilivyopangiwa ili kuhakikisha kuwa wafadhili wote wanakuwa na Imani na pia waweze kuendelea kusaidia.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mawasiliano wa MultiChoice Tanzania Johnson Mshana amesema kampuni ya MultiChoice imekuwa ikiwekeza fedha nyingi katika sekta mbalimbali za kijamii, na ufadhili huu ni ishara tosha ya ushirika wao katika kuleta maendeleo ya jamii yetu.
Kutoka kulia; Mkuu wa Uhusiano wa MultiChoice Tanzania Johnson Mshana, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kusini Unguja Mussa Juma na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kassom Mtoro wakiangalia waraka wa makubaliano ya ujenzi wa nyumba hizo
“Mbali na kutoa huduma zenye ubora wa kisasa za televisheni kupitia DStv, MultiChoice pia tumewekeza katika miradi ya kijamii na tumekuwa tukifanya hivi kwa mujibu wa sera yetu inayotutaka kuhakikisha kuwa uwepo wa kampuni yetu hapa nchini unachangia katika kuleta maendeleo endelevu” alibainisha Mshana.
Mshana amesema kuwa MultiChoice inashiriki katika miradi mbalimbali ya kijamii ikiwemo kukuza na kuimarisha vipaji katika tasnia ya michezo na filamu, miradi ya elimu, afya, mazingira pamoja na kuwawezesha vijana wa tanzania kujiajiri.
Akifafanua zaidi kuhusu Mradi huo, Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kusini Kassim Mtoro amesema taratibu zote zimeshakamilika na tayari mkandarasi ameshapatikana na kazi imeanza. Amefafanua kuwa nyumba hizo zitakuwa na uwezo wa kuhifadhi familia mbili
na hivi sasa zipo katika hatua ya kupaua.
Jengo la nyumba mbili za waalimu likiwa linaendelea kujengwa katika shule ya Kizimkazi Kusini Unguja kwa ufadhili wa kampuni ya MultiChoice.
Kwa mujibu wa Kassim, nyumba hizo zinatarajiwa kukamilika ndani ya miezi miwili ijayo na wanatarajia kuwa kila kitu kitakwenda sawa kwani tayari taratibu zote zimeshakamilika kuwawezesha MutiChoice kutoa fedha hizo.
No comments:
Post a Comment