Watafiti, Dk.Beatrice Lyimo (wa tano kushoto) na Bestina Daniel (wa pili kulia), kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH),wakiwakabidhi mbegu bora ya mihogo Wanakikundi cha Chapakazi katika Kijiji cha Kalebezo wilayani Biharamulo mkoani Kagera jana, kwa ajili ya kuanzisha shamba darasa wakati wa uzinduzi wa shamba hilo wilayani humo.
Mwakilishi wa Ofisa Kilimo wa wilaya hiyo, Bruno Ngawagala (kulia), akizungumza na wakulima wakati wa uzinduzi wa upandaji wa mbegu ya mhogo kwenye shamba darasa katika Kijiji Kalebezo wilayani humo.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Chapakazi, Thadeo Kibuka akizungumza katika uzinduzi huo.
Mtafiti kutoka COSTECH, Bestina Daniel, akizungumza.
Mtafiti, Dk.Beatrice Lyimo kutoka COSTECH, akizungumzia kuhusu mradi huo wa mbegu bora
Mtafiti wa mazao jamii ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti cha ARI-Maruku mkoani Kagera, Josianas Kabura (mwenye mbegu), akitoa mafunzo kwa wakulima jinsi ya kupanda mbegu hiyo ya mhogo aina ya Mkombozi iliyozalishwa kitaalamu.
Mtafiti wa mazao jamii ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti cha ARI-Maruku mkoani Kagera, Josianas Kabura, akielekeza namna ya upandaji wa mbegu ya viazi lishe katika kijijini cha Msenyi
Mwakilishi wa Ofisa Kilimo wa wilaya hiyo, Bruno Ngawagala, akipanda mbegu hiyo katika shamba darasa kijijini Kalebezo.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Chapakazi, Thadeo Kibuka akipanda mbegu ya mhogo.
Ofisa Ugani, Jonas Kamugisha akipanda mbegu ya mhogo.
Ofisa Ugani wa Kijiji cha Kalebezo, Juster Nkuna akipanda mbegu ya mhogo.
Mbegu ya mhogo ikishushwa kutoka kwenye gari tayari kwa uzinduzi wa shamba darasa katika Kijiji cha Kalebezo.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Chapajembe wa Kijiji cha Msenyi, Josia Kagwingi, akizungumza wakati wa uzinduzi wa shamba darasa la viazi lishe katika kijiji hicho. Kutoka kushoto ni Katibu wa Kikundi hicho, Mariana Mariko na kulia ni mwanakikundi, Zabia Emanuel.
Mkulima wa Kijiji cha Msenyi, Martin Tibenda akipanda mbegu ya viazi lishe katika uzinduzi wa shamba darasa.
Na Dotto Mwaibale, Biharamulo Kagera.
WAKULIMA wilayani Biharamulo mkoani Kagera wameipongeza Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) pamoja na Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB) kwa kuwapelekea mbegu bora ya migomba,mihogo na viazi lishe ambayo itapandwa katika mashamba darasa na kusambazwa kwa wakulima wengine katika wilaya hiyo.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwakilishi wa Ofisa Kilimo wa wilaya hiyo, Bruno Ngawagala wakati wa uzinduzi wa upandaji wa mbegu ya mhogo kwenye shamba darasa katika Kijiji Kalebezo wilayani humo.
"Kwa niaba ya Ofisa Kilimo wa wilaya napenda kuishukuru COSTECH kwa kutuletea mbegu hizo katika wilaya yetu hasa baada ya kuona changamoto tuliyokuwa tukikabiliana nayo ya magonjwa ya mihogo kama batobato" alisema Ngawagala.
Ngawagala alisema msaada huo hautapotea bure kwani watahakikisha wanayahudumia vizuri mashamba darasa hayo likiwemo la mihogo lililopo katika Kijiji Kalebezo na lile la viazi lishe lililopo Kijiji cha Msenyi ambayo yamezinduliwa na kuhudhuriwa na wakulima kutoka vikundi vya Chapakazi katika Kijiji cha Kalebezo na Chapajembe cha Kijiji cha Msenyi vyote vya wilaya hiyo.
Mwenyekiti wa kikundi hicho cha Chapakazi, Thadeo Kibuka alisema mbegu hiyo waliyoletewa itakuwa mkombozi wao kwani kwa muda mrefu walikuwa na changamoto ya kupata mazao yenye magonjwa kutokana na kukosa mbegu bora na ukame.
"Tutahakikisha shamba ili tunalo lizindua leo hii kwa msaada wa COSTECH na OFAB linakuwa la mfano wa kuzalisha mbegu bora katika wilaya hii" alisema Kibuka.
Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi wa COSTECH, Mtafiti Dk. Beatrice Lyimo alisema COSTECH kwa kushirikiana na OFAB wanaendesha mradi huo ili kuhakikisha kuhakikisha matokeo mazuri ya kazi za tafiti yanawafikia wakulima na kupata chakula cha kutosha.
Alisema COSTECH ndio mshauri mkubwa wa serikali katika masuala ya kilimo cha kitafiti hivyo wanakila sababu ya kuhakikisha tafiti zinazofanyika nchini zikiwafikia walengwa ili waweze kufanya vizuri katika kilimo.
Dk. Lyimo aliwataka wakulima hao kwa kushirikiana na maofisa ugani kuyatunza mashamba darasa hayo ili kupata mbegu nyingi za mazao hayo na kuzisambaza kwa wakulima wengine.
Ofisa Kilimo Mkoa wa Kagera, Louis Baraka alisema mkoa huo umepata bahati kubwa kwa kupelekewa mbegu hizo katika wilaya tano ambapo katika kila wilaya vijiji viwili vilichaguliwa kuanzisha shamba darasa la mbegu ya mhogo na migomba na viazi lishe kutegemea uhitaji wa zao gani katika kijiji husika.
"Tuna bahati kubwa kuletewa mradi huu katika mkoa wetu hivyo tusiwaangushe hawa wenzetu tuwe wa mfano tuyatunze haya mashamba ili tupate matokeo mazuri" alisema Baraka.
Mtafiti wa mazao jamii ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti cha ARI-Maruku mkoani Kagera, Josianas Kabura amewataka wakulima hao kutambua kuwa mbegu hizo za mihogo walizokabidhiwa zinatunzwa vizuri kwani zinauwezo wa kutoa tani 32 za mhogo kwa ekari moja na kwa viazi lishe zinatoa tani 7 hadi 9 kwa ekari tofauti na mbegu za zamani ambazo hazina tija.
Mashamba darasa ya mbegu bora za Mihogo,Viazi lishe na Migomba iliyozalishwa kwa njia ya chupa yaliyoanzishwa katika mkoa huo yanajumuisha wilaya tano za Mkoa wa Kagera baada ya COSTECH na OFAB kutoa mafunzo kwa wataalamu wa kilimo wa wilaya hizo na kata zote ikiwa na lengo la kuwasaidia wakulima kuzalisha mazao yao kwa tija na kuachana na kilimo kisicho bora na tija.
Mashamba darasa ya mbegu bora za Mihogo,Viazi lishe na Migomba iliyozalishwa kwa njia ya chupa yaliyoanzishwa katika mkoa huo yanajumuisha wilaya tano za Mkoa wa Kagera baada ya COSTECH na OFAB kutoa mafunzo kwa wataalamu wa kilimo wa wilaya hizo na kata zote ikiwa na lengo la kuwasaidia wakulima kuzalisha mazao yao kwa tija na kuachana na kilimo kisicho bora na tija.
No comments:
Post a Comment