Timu
ya Taifa ya Riadha inayoshiriki mashindano ya Dunia ya riadha
yanayoendelea jijini London inaanza kibarua cha kuipeperusha bendera
yetu kesho (Jumamosi 05/08/2017) ambapo mfukuza upepo Failuna Abdi
Matanga atakimbia mbio za mita 10,000 kesho (Jumamosi Agosti 6, 2017).
Failuna atashuhudiwa na maelfu ya watanzania kupitia DStv Muda wa saa
mbili usiku.
Akithibitisha
kuonekana kwa matangazo hayo kupitia DStv, Mkurugenzi Mtendaji wa
Multichoice Tanzania Maharage Chande amesema DStv imefanya jitihada
kubwa na kuhakikisha kuwa watanzania wanaishuhudia timu yetu
ikituwakilisha katika mashindano hayo muhimu ulimwenguni.
“Tunawahakikishia
watanzania burudani hii moja kwa moja kupitia DStv chaneli za
Supersport. Tunaamini sote tutakuwa nyuma yao wachezaji wetu
kuwashuhudia jinsi wanavyotuwakilisha” alisema Maharage.
“Suala
la watanzania kuwashuhudia vijana wetu wakishiriki katika mashindano
makubwa kama haya lina maana kubwa sana. Vijana wadogo wakiwaona dada
zao na kaka zao wakishiriki mashindano makubwa kama haya inawatia moyo
na kuwapa ari na tamaa ya wao kujitahidi na kufika hatua kama hizo. Hili
ni jambo la muhimu sana na sisi DStv tunalitilia mkazo sana. Ni njia
moja wapo ya kuwashawishi na kuwatia moyo vijana wetu wanaochipukia na
kuwajengea kujiamini.”
Baada
ya Failuna anayekimbia mita 10,000, watanzania watashuhudia tena
shughuli pevu siku ya jumapili kupitia DStv kuanzia majira ya saa nne
asubuhi ambapo vidume watatu - Alphonce Felix Simbu, Ezekiel Jafari
Ng’imba na Stefano Huche Gwandu watakuwa wakikata upepo katika viunga
vya jiji la Malkia London ikiwa ni mbio ndefu za kilomita 42.
Baada
ya vidume hao kukamilisha kazi tuliyowatuma, wanawake wetu wa shoka nao
wataingia barabarani ambapo Tanzania inawakilishwa na Sara Ramadhani
Makera na Magdalena Crispin Shauri ambao nao watafukuza upepo umbali wa
kilomita 42 majira ya saa nane mchana. Patashika yote hii itaonekana
DStv.
Wanariadha
wengine wawili wa mbio fupi za mita 5,000 ambao ni Emmanuel Giniki
Gisamoda na Gabriel Gerald Geay watatimka siku ya Jumatano tarehe 9
Agosti majira ya mbili usiku hii ikiwa ni raundi ya mchujo na wakifuzu
watashiriki fainali ya mita 5,000 siku ya Jumamosi tarehe 12 Agost
majira ya mbili usiku. Nao pia watashuhudiwa mubashara kupitia DStv.
Mashindano
ya Dunia ya Riadha yalianza rasmi 1983 ambapo Tanzania imewahi kupata
medali 1 tu ya Fedha kupitia mwanariadha Christopher Isegwe kwenye mbio
za Marathon 2005 Helsinki Finland.
Ni
mashindano ya pili kwa ukubwa baada ya Olimpiki ambapo nchi 204
zinashiriki mashindano hayo mwaka huu. Tangu kuanzishwa kwa mashindano
hayo mwaka huu ndiyo mwaka ambao Tanzania imeleta timu kubwa ya
wanariadha 8, ambao ina mchanganyiko wa wanaume na wanawake na pia kuna
wakimbiaji wa mbio za uwanjani.
Wanariadha wote wanaoshiriki wamefikia viwango vinavyotakiwa na Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF)
No comments:
Post a Comment