BREAKING

Wednesday, 8 March 2017

MANISPAA YA UBUNGO YABAINISHA MPANGO WA KUKUZA UCHUMI NA KUPUNGUZA UMASIKINI ILI KUFIKIA MAENDELEO ENDELEVU

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo Mhe Boniface Jacob akisisitiza jambo mbele ya waandishi wa habari ofisini kwake.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo Mhe Boniface Jacob akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake  kuelezea Makadirio ya Mapato na Matumizi ya maendeleo kwa kipindi cha mwaka 2017/2018
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo Mhe Boniface Jacob akielezea jinsi Bajeti ya Manispaa hiyo ilivyopitishwa kwa kuungwa mkono kwa 100% kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa hiyo kilichofanyika 4/03/2017.

Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo imebainisha namna ya  kuboresha maisha ya wakazi wake kwa kuweka mpango mzuri wa muda wa kati wa mwaka 2017/2018 2019/2020 ambao  unalenga kukuza uchumi, na kupunguza umaskini ili kufikia maendeleo endelevu ya kijamii, kiuchumi na kimazingira kwa wananchi wake.

Mpango huo umeandaliwa kwa kuzingatia sera na miongozo ya Kitaifa, kwa mujibu wa sheria ya bajeti  Na. 11 ya mwaka 2015,   Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ambapo Mpango mkakati ni  kutekelezwa kwa matokeo makubwa sasa (BRN), Sera ya Taifa ya UKIMWI, Sera za kisekta, Mipango Shirikishi Jamii ya Fursa na Vikwazo kwa Maendeleo (O&OD) ya Kata na Mitaa.

Hayo yamebainishwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo Mhe Boniface Jacob alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake  kuelezea juu ya  Makadirio ya Mapato na Matumizi ya kawaida na ya maendeleo kwa kipindi cha mwaka 2017/2018, Makadirio yalijadiliwa na Waheshimiwa Madiwani katika Kamati za Kudumu,na kuidhinishwa na baraza maalumu la madiwani jumamosi ya tarehe 04/03/2017 kwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.   


Mstahiki Meya alisema kuwa ili kutekeleza dhana nzima ya ung’atuaji wa madaraka, mpango huu umeshirikisha jamii katika mpango shirikishi ambao huanzia ngazi ya Mtaa ambapo Hali hiyo imezingatia vipaumbele na mahitaji halisi ya wananchi katika maeneo yao.

Alisema kuwa Mpango huo umejielekeza katika kutoa kipaumbele maeneo yanayoweza kutoa matokeo ya haraka (quick wins) ambayo yatasaidia ukuaji wa uchumi kwa haraka katika kipindi kifupi na kutoa huduma bora kwa wananchi wa Ubungo.


Aidha alieleza maeneo yaliyopewa kipaumbele katika mpango huo kuwa ni pamoja na Kuboresha na kuimarisha ukusanyaji wa Mapato ya Manispaa, Ujenzi wa ofisi za makao makuu ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Kuboresha miundombinu ya Afya, Shule za Msingi na Sekondari, Kuboresha miundombinu ya maji, mifereji, taa za barabarani barabara na Kilimo mjini, Kuboresha hifadhi ya mazingira na ukusanyaji wa taka, Kuimarisha ushirikishwaji wa jamii katika upangaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo na Kuboresha mazingira ya wafanyabiashara ndogo ndogo.

Katika harakati za kuyafikia mafanikio yaliyotajwa Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo ameeleza kuwa Manispaa hiyo Uimarisha mahusiano mazuri kati ya Serikali, mashirika yasiyo ya Kiserikali na wadau wengine, Kuendelea kujenga uwezo na ujuzi kwa watumishi katika utoaji wa huduma zilizo bora na haraka, Kuimarisha Utawala bora, Uwajibikaji na Uwazi sambamba na Kujenga uwezo wa viongozi wakiwemo Madiwani, Wenyeviti wa serikali za mitaa katika kusimamia shughuli za wananchi.

Sambamba na hayo pia amesema kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kwa mwaka 2016/2017 ilikadiria kutumia Sh. 116,045,935,228.99 ikiwa ni pamoja na fedha za mfuko wa barabara.

Kuanzia Julai hadi Disemba, 2016, Halmashauri ilikuwa imekusanya Sh. 1,024,839,737.74 fedha za vyanzo vya ndani sawa na asilimia 8 ya maoteo ya Tsh 13,300,416,090.50 ya vyanzo vya ndani yaliyotarajiwa kukusanywa kwa nusu mwaka wa bajeti yaani Julai 2016 hadi Disemba 2016.

Katika kipindi hiki Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo imeweza kutumia kiasi cha Sh. 150,764,997.88. ya makusanyo yake ya ndani yaliyoanza kukusanywa mwezi Novemba  2016,  na hakuna fedha yoyote ya ruzuku iliyopokelewa hadi sasa kama inavyooneshwa katika Jedwali hapa chini.  


Jacob ametaja changamoto mbalimbali zinazopelekea ucheleweshaji katika kutoa huduma na kuleta maendeleo kwa wananchi ikiwa ni pamoja na Mwamko mdogo wa wananchi kuchangia shughuli za maendeleo, Fedha za miradi za Serikali kuu na wafadhili kutoletwa kwa wakati na hivyo kuathiri utekelezaji wa miradi kama ilivyopangwa. Miradi yote iliyopangwa kutekelezwa kwa fedha za ruzuku haijaanza, Makusanyo hafifu ya mapato ya ndani kutokana na mgawanyo wa Halmashauri na upya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo. Hivyo miradi  iliyopangwa kutekelezwa kwa mapato ya ndani mingi haijaanza kutekelezwa, Ukosefu wa maeneo ya kujenga majengo mapya kama vile Shule za Msingi na Sekondari, pamoja na Madai makubwa ya fedha za fidia katika maeneo mbalimbali.

Hata hivyo Sababu zilizopelekea kukusanya mapato ya ndani  chini ya malengo ni pamoja na Serikali kuhamishia kodi ya Majengo kukusanywa na Mamlaka ya mapato TRA ambapo kwa wigo wa makusanyo uliopo wa kodi ya majengo ni shilingi bilioni 6, kwa bajeti ya mwaka 2016/2017 ya makusanyo ya ndani yenye makadirio ya Tsh. 26.6 bilioni, Kushuka kwa mauzo ya wafanyabiashara hali inayopelekea biashara kufungwa na malipo ya ushuru wa huduma kupungua, na SUMATRA kubadilisha route za mabasi ya kariakoo (160) na mikoani (350) kimepunguza makusanyo katika kituo chetu cha Simu 2000 (Sinza bus terminal) ambapo takribani magari  kati ya 510 yaliyokuwa yanaingia kituoni yamepungua na kusababisha upungufu wa Sh. 12,900,000/= kwa kila mwezi.

Sababu zingine ni Upungufu wa vitendea kazi baada ya Mgawanyo wa Halmashauri na hasa ukosefu wa magari yanayotumika kukusanyia mapato, Kipindi cha mpito tangu kuanzishwa kwa Halmashauri hadi kuanza kukusanya mapato ya ndani kwa Halmashauri yetu mpya ilipoanzishwa rasmi tarehe 1/07/ 2016, imeanza kukusanya mapato yake ya ndani yenyewe kuanzia mwezi Novemba 2016, Walipakodi kuendelea kulipia katika Halmashauri mama (Kinondoni) kwa kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2016 kwa mazoea kiasi cha takriban Sh. milioni 500 kimekusanywa kimakosa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni  mawasiliano yanafanyika ili kurejesha makusanyo hayo.


Ili kukabiliana na changamoto hizo Mikakati ya Halmashauri imetajwa kuwa ni pamoja na Kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha wananchi ili kutambua kuwa miradi ya maendeleo wanayochangia ni kwa ajili ya manufaa yao wenyewe na vizazi vijavyo, Kendelea kupanua wigo wa ukusanyaji wa mapato kwa kubuni vyanzo vipya kwa mujibu wa sheria na kuimairisha ukusanyaji wa mapato katika vyanzo vilivyopo.

Mikakati mingine ni Kukusanya mapato yote kwa kutumia mfumo wa kielektroniki, na Kununua maeneo ya pembezoni mwa mji na kuhakikisha tunalipa fidia kabla ya kuyatwaa maeneo ya watu.


Vipaumbele vitakuwa katika maeneo yafuatayo:-Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo Mhe Boniface Jacob amebainisha kuwa Bajeti hiyo imelenga katika kuboresha maisha ya wananchi na kukuza kipato cha mkazi ili kukuza uchumi wa ndani ambapo ametaja vipaumbele 13 ambavyo vitapaswa kufanyiwa kazi katika bajeti hiyo kuwa ni pamoja na Kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kutumia mfumo wa kielektroniki, na Kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa kununua madawa na  vifaa tiba na  kuboresha miundo mbinu ya afya kwa kupanua hospitali ya Sinza kwa kujenga ghorofa ya pili jengo la OPD, Ujenzi wa wodi ya wazazi kituo cha afya mbezi, ujenzi wa jengo la kuhifadhia chanjo Mabibo, kujenga zahanati ya King’azi Kwembe Jumla ya Tsh.   5,732,424,610.00 zimetengwa.  

Kuboresha miundombinu ya barabara kwa kujenga Madaraja/ Makalvati, barabara kwa kiwango cha lami, kufanya matengenezo ya kawaida ya barabara, muda maalum, maeneo korofi, njia za waenda kwa miguu, Ujenzi wa Mifereji katika barabara za Manispaa ambapo Jumla ya Tsh 6.2 bilion zimetengwa, Kuboresha miundo mbinu ya shule za Msingi na Sekondari kwa kununua madawati, kujenga madarasa, vyoo, nyumba za walimu, maabara na ukarabati wa miundombinu. Jumla ya Tsh.5.5 billion zimetengwa na Kutoa mikopo kwa wajasiliamali wa dogo kwa vikundi vya wanawake na vijana ili kuongeza ajira na kukuza kipato cha Mkazi. Jumla ya Tsh.1.9 billion  zimetengwa.

Kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na kutoa huduma kwa kujenga Ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo. Tsh.1.7 billion  zimetengwa, Kununua magari na mitambo magari 6 ya ofisi, gari moja la maji machafu na gari 1 la maji safi, jenereta. Jumla ya Tsh 1.35 billion  zimetengwa, Kulipa fidia kupisha ujenzi wa miradi mabali mbali ya maendeleo na kufanya uthamini wa mali za Manispaa. Jumla ya Tsh.1.2 billion zimetengwa, Kuboresha usafi wa mazingira na na ukusanyaji taka na  kununua magari makubwa ya taka Jumla ya Tsh.1 billion zimetengwa, Kuboresha upatikana maji safi na salama kwa wakazi wa Ubungo kwa kujenga na kukarabati miundo mbinu ya maji. Jumla ya Tsh.550 million zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji na Mipango miji, kupima na kumilikisha maeneo ya umma na kutekeleza mfumo wa anuani za makazi (Postcode). Jumla ya Tsh.550 million zimetengwa.

Aidha Halmashauri ya Maninspaa ya ubungo imetenga Tsh 42 milioni kwa mwaka huu kwa ajili ya kijiji cha michezo kilichopo kibwegele ambapo kijiji hicho kitakuwa na kiwanja cha mpira wa miguu na viwanja vya michezo ya watoto, kwa Mwaka wa fedha 2017/2018 ambapo Tsh 50 milioni zimetengwa, na Kuboresha na kukarabati masoko Manispaa tumetenga Tsh 1.2 Bilioni, kwa ajili ya kuboresha masoko ambayo ni Mabibo, Shekilango, Sinza one, na Mbezi pia fedha hizo zitatumika kulipa fidia na kupima maeneo kwa ajili ya wamachinga na maeneo ya uwekezaji.

No comments:

Post a Comment

 
Copyright © 2016 Shamakala
Designed by Switch International | SHAMAKALA 360
    Twitter Facebook Google Plus Vimeo Videosmall Flickr YouTube