Thursday, 30 March 2017
MTANZANIA ALIYEWEKA REKODI YA KUPANDA MLIMA KILIMANJARO KWA MUDA MFUPI AMUANGUKIA WAZIRI MWAKYEMBE
Gaudence Lekule akiwa katika kilele cha Uhuru ,Mlima Kilimanjaro baada
ya kukimbia kwa muda wa wa saa 8:36 mpya akiwa Mwafrika na Mtanzania wa kwanza
kutumia muda huo kupanda kilele cha mlima Kilimanjaro na kushuka.
Gaudence Lekule akipanda mlima Kilimanjaro huku akikimbia wakati akiweka
rekodi baada ya kutumia muda wa saa 8:36 mapema mwaka huu.
Lekule akifurahia mara baada ya kufanikiwa kuweka ekodi ya kutumia muda wa saa 8:36 kupanda Mlima Kilimajaro na kushuka.
Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii Kanda ya Kaskazini.
MTANZANIA ,Gaudence Lekule (31) anayeshiriki michezo ya kupanda milima
kwa kasi (Mountain Run) amemuomba Waziri mpya wa Habari,Utamaduni Sanaa na
Michezo ,Dkt Harison Mwakyembe kutupia jicho michezo mingine kwani ina nafasi
kubwa ya kutangaza na kuletea sifa taifa.
Lekule anayeshikilia rekodi ya kuwa Mwafrika wa kwanza Duniani kupanda
kwa muda mfupi katika Mlima Kilimanjaro akitumia muda wa jumla wa saa 8:36
alitoa wito pia kwa kampuni,taasisi binafsi na za serikali kujitokeza kudhamini
wanamichezo kutokana na eneo hilo upo uwezekano wa kujitangaza zaidi kidunia.
Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalum,Gaudence alisema kwa
sasa yupo katika maandalizi ya kuweka rekodi mpya katika milima mirefu na
maarufu Duniani kwa kufanya mazoezi ya awali hapa nchini na baadae nje ya
nchi.
“ Nashukuru kuitangaza Tanzania kidunia na tayari nimepata mialiko
mingi ya kwenda nje kushiriki mashindano ya Mountain Run ,Lengo langu ni
kuweka rekodi katika milima mirefu duniani hivyo bado naendelea na mazoezi na
nitaendelea kufanya mazoezi hapa kwetu na badaae nje ya Tanzania”alisema
Gaudence .
Alisema hadi sasa rekodi ya Dunia inashikiliwa na raia wa nchi ya
Ecuador, Karl Egloff aliyetumia muda wa saa 6:53 kupanda na kushuka Mlima
Kilimanjaro ,rekodi aliyoweka mwaka 2014 akivunja rekodi ya Kilians
Jornet raia wa Hispania aliyetumia muda wa saa 7:20 kupanda na kushuka
mlima Kilimanjaro mwaka 2010.
Lekule alisema changamoto iliyopo kwa sasa ni mabadiliko hali ya hewa
inayochangia kushindwa kufanya mazoezi na upatikanaji wa mahitaji kama chakula
pamoja na mavazi kwa ajili ya mchezo huo unafanyika kuanzia urefu wa mita 3500
hadi 5800.
Akizungumzia kilichomsukuma kushiriki mcezo mchezo huo,Lekule ,mkazi wa
kiraracha Marangu wilaya ya Moshi alisema raia wa kigeni wamekuwa wakishiriki
katika michezo ya aina hiyo kwa ajili ya kuweka rekodi hivyo akaona ni wakati
wa waafrika pia kushiriki katika uwekaji wa rekodi Duniani.
Alisema raia wa Ecuador ,anayeshikilia rekodi ya dunia aliposikia
ameweka rekodi akiwa ni mwafrika na Mtanzania wa Kwanza alituma salamu za
pongezi huku akimtaka kwenda kwenye milima iliyopo nchi za nje kutafuta rekodi
nyinine.
“ Egloff alifurahi sana na kunipa moyo na kunitaka nikatafute
rekodi nje ya Afrika kwa sababu nina uwezo mkubwa wa kufanya vizuri Ulaya
na kuipa sifa Tanzania,ni ngumu sana mtu kukimbia kwenye urefu kama uliopo
Mlima Kilimanjaro na katika maisha inahitaji moyo sana.”alisema Lekule.
Rekodi za kidunia.
Mara ya kwanza rekodi ya kupanda Mlima Kilimanjaro kwa kasi kwa
Afrika ilikua inashikiliwa na Saimon Mtui akitumia muda wa saa 9 : 20 mwaka
2006, baadae raia wa Hspania Kilians Jornet alitumia muda
wa saa 7:20 mwaka 2010.
Mwaka 2014 ndipo Karl Egloff raia wa Ecuador anayeshikilia
rekodi ya Dunia hadi sasa alitumia muda wa saa 6 :53 mwaka 2014
na sasa Mtanzania Gaudence Lekule ameweka rekodi ya kuwa
Muafrika na Mtanzania wa Kwanza akitumia muda wa saa 8:36 .
08:24
Tuesday, 28 March 2017
MAJALIWA APOKEA TAARIFA YA TUME YA FARU JOHN
09:06
Monday, 27 March 2017
MD KAYOMBO AKAGUA ENEO LITAKLOTUMIKA KWA AJILI YA MAONESHO YA NANENANE LA MANISPAA YA UBUNGO LILILOPO MKOANI MOROGORO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo akisisitiza jambo mara baada ya kutembelea Shamba litakaloandaliwa kwa ajili ya Maonesho ya Nanenane lililopo Mkoani Morogoro
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo amefanya ukaguzi wa eneo kwa ajili ya Maonesho ya Kilimo (Nane Nane) ili kujiridhisha na kutoa maelekezo ya maandalizi kwa kufyeka majani yaliyopo katika eneo la JKT Mtaa wa Nanenane ikiwa ni hatua za ufanisi kwa ajili ya kuelekea Maonesho ya Nane Nane mwanzoni kwa mwezi Agosti.
Kayombo amesema kuwa lengo kuu la kuzuru kwanza ilikuwa ni kujionea eneo hilo sambamba na kuona hali ya utendaji kazi ili kuanza ufyekaji na kuanza kulima mazao ambayo yanakusudiwa kuoneshwa na Manispaa ya Ubungo.
Amesema kuwa katika utendaji wake amekusudia kwenda mwenyewe Field ili kuona hali ya utendaji ilivyo sio kupelekewa Taarifa pekee kwani kufanya hivyo Ukurugenzi alionao utakuwa hauna maana kama ataishia ofisini.
"Rais ametupa mamlaka makubwa ya kuwatumikia wananchi sasa kama tunakaa ofisi pekee nchi haiwezi kusonga mbele badala yake ili tuweze kuwa na mafanikio katika utendaji pamoja na Kukuza uchumi kupitia sekta mbalimbali ni wazi kwamba tunapaswa kuzuru katika maeneo yote tunayoyaongoza" Alisema Kayombo
MD Kayombo amewapa maelekezo Afisa Kilimo na Afisa Mifugo na Uvuvi kuanza haraka iwezekanavyo usafishaji wa shamba hilo lenye ukubwa wa Mita za Mraba 3600 ili kulima na kupanda mazao kusudiwa kwa ajili ya Maonesho ya Kilimo Nane Nane.
Maelekezo mengine ni pamoja na kununua viuatilifu kwa ajili ya kuua wadudu waharibifu na magonjwa, kuandaa mabango na kuainisha aina mbalimbali za malisho iliyooteshwa na kujenga bwawa la samaki.
Kayombo alisema kuwa eneo hilo limenunuliwa na Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kwa ajili ya Maonesho ya Nane Nane ambayo hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuwakutanisha wakulima, Wafugaji na wavuvi kwa kuwaelimisha na kuwajengea uwezo wa kutumia teknolojia na mbinu za kuongeza uzalishaji katika eneo la Uvuvi, Kilimo na Ufugaji.
Akizungumzia utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Kaimu Afisa Kilimo wa Manispaa ya hiyo Ndg Salim Msuya amesema kuwa wanataraji kuanza kutekeleza hivi karibuni ikiwa ni pamoja na kujenga mabanda ya mifugo na sehemu za kusindika mazao ya mifugo, kuandaa mavazi rasmi kwa ajili ya washiriki wa Maonesho.
Mengine ni kukusanya bidhaa za mazao mbalimbali ya wafugaji, wakulima na wavuvi watakaoshiriki Maonesho hayo ya Kilimo Nane Nane kwa ajili ya kuyapeleka Morogoro.
Sambamba na hayo pia Msuya amesema kuwa maandalizi mengine itakuwa ni kutengeneza matuta ya kuoteshea malisho, Kununua mbolea na kuweka kwenye eneo la malisho ya mifugo, kufunga maji katika eneo la malisho yatakayotumika kwa ajili ya umwagiliaji na mifugo itakayopelekwa wakati wa Maonesho.
Msuya ameeleza kuwa maandalizi mengine itakuwa ni kuandaa mashimo katika matuta ya kuotesha miche, Vipande na Mbegu za malisho pamoja na kutayarisha eneo la kwa kusafisha eneolima na kufanya Layout ya eneo la kuchimba bwawa kwa ajili ya ufugaji samaki.
13:55
WAZIRI MWIGULU AWAASA ASKARI KUTOWABAMBIKIZIA WATU KESI
Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Mhe Mwigulu Lameck Nchemba akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha kazi cha Mwaka 2017 cha Maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi |
Mzee John Samwel Malecela akizungumza wakati wa kikao cha kazi cha Mwaka 2017 cha Maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi
Maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi
Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Mhe Mwigulu Lameck Nchemba akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha kazi cha Mwaka 2017 cha Maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi
SACP Ramadhani Mungi Msimamizi wa
bandari Tanzania na Kamanda
wa polisi mkoa wa Lindi Renata Mzinga wakifatilia kwa makini kikao cha kazi
cha Mwaka 2017 cha Maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi
Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Mhe Mwigulu Lameck Nchemba akisalimiana na Makamu wa kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu Mzee John Samwel Malecela mara baada ya kuwasili katika ufunguzi wa kikao cha kazi cha Mwaka 2017 cha Maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/VikosiWaziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Mhe Mwigulu Lameck Nchemba akisalimiana na baadhi ya Maafisa wa jeshi la Polisi mara baada ya kuwasili katika ufunguzi wa kikao cha kazi cha Mwaka 2017 cha Maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi
Kamanda wa Jeshi la Polisi nchini Ernest Mangu Akisisitiza jambo wakati wa kikao cha kazi cha Mwaka 2017 cha Maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Jordan Lugimbana akitoa salamu za Mkoa wa Dodoma wakati wa kikao cha kazi cha Mwaka 2017 cha Maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi
Na Mathias Canal, Dodoma
Askari na Maafisa wa jeshi la Polisi nchini wameaswa kutotumia madaraka yao vibaya kwa kuwabambikizia wananchi kesi kwani kufanya hivyo ni kushindwa kusimamia dhamira njema ya Mhe Rais ya kuwapatia wananchi wanyonge haki zao stahiki.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Mhe Mwigulu Nchemba wakati akifungua kikao cha kazi cha Siku tatu cha mwaka 2017 kwa maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa LAPF Mjini Dodoma.
Mhe Mwigulu amesema kuwa kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya kuwabambikizia kesi, Kuwabadilishia watu kesi zao za msingi kwa sababu ya kushindwa kutoa rushwa hivyo kikao hicho kinapaswa kuwa na maamuzi na maadhimio yenye dira na taswira njema kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
Amesisitiza pia Askari na Maafisa wa Polisi kutotumia taarifa za watu wanaohasiana kuwa ndio chanzo pekee cha msingi wa shtaka badala yake kufanya uchunguzi kwa kina na kujiridhisha vyema ili kufikia hukumu yenye tija Na haki kwa mtuhumiwa kwani kufanya hivyo kutaimarisha amani na jeshi la Polisi kupata taarifa nyingi za uhalifu kutoka kwa wananchi endapo watajikita katika haki.
Akizungumzia Vita dhidi ya Dawa za Kulevya Mhe Nchemba alisema kuwa serikali imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kukamata na kuziteketeza Dawa za kulevya zilizopo mashambani ambapo ametilia msisitizo zaidi kwa Askari na Maafisa wa Jeshi la Polisi kuendelea kupambana ili kuzikamata Dawa za kulevya zilizopo katika viwanda.
Amesisitiza pia Jeshi la Polisi kuendelea kupambana na kubaini uhalifu sambamba na kushirikiana na vyombo vingine ili kuhakikisha lengo mahususi la serikali ambalo ni kuzuia uhalifu linafanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Mhe Mwigulu amesema kuwa kauli mbiu ya Mwaka 2017 inayosema "ZINGATIA MAADILI TUNAPOPAMBANA NA UADILIFU ILI KUIMARISHA USALAMA KWA MAENDELEO YA TAIFA" endapo kama itatekelezwa kwa vitendo itaijenga nchi na kuzidi kudumisha zaidi amani iliyopo kwa wananchi.
Naye Kamanda wa Jeshi la Polisi nchini Ernest Mangu alisema kuwa kikao hicho cha kazi kwa Maafisa wa Jeshi la Polisi kina dhamira kubwa ya kufanya Tathmini ya utendaji wa mwaka 2016 na kuandaa mikakati mizuri ya mwaka 2017 na kupata fursa ya kubadilika kiutendaji kwa kuzingatia dhamira ya serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli.
Hata hivyo amesisitiza zaidi askari wote nchini kutofanya kazi kwa mazoea, Kuacha Urasimu na kujenga uaminifu na weledi katika kazi.
Mangu amesema matendo ya Askari Polisi nchini yanapaswa kuwa mfano bora wa kuigwa katika jamii hivyo askari Polisi hapaswi kuwa chanzo cha vurugu au kujihusisha na matendo ovu yasiyostahili katika jamii.
Ameongeza kuwa miongoni mwa mambo yatakayopewa kipaombele kwa kujadiliwa katika Kikao hicho itakuwa ni pamoja na Vita dhidi ya Dawa za Kulevya, Vita dhidi ya Magendo, Vita dhidi ya ujangili na Uvuvi sambamba na Vita dhidi ya Ubambikizaji wa kesi kwa wananchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Jordan Lugimbana akitoa salamu za Mkoa wa Dodoma kabla ya kumkaribisha Waziri Mwigulu Nchemba kuzungumza na askari hao amelipongeza jeshi la Polisi kwa kazi kubwa linayofanya ambapo pia ameeleza mpango wa Mkoa katika kupambana na migogoro ya ardhi kwa kuanzisha kamati maalumu ya wataalamu wa sheria kutoka chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) Kupitia na kushauri ili kuweza kumaliza haraka migogoro hiyo.
Naye Makamu wa kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu Mzee John Samwel Malecela alisema kuwa jambo la msingi ambalo askari Polisi wanapaswa kulifanya ni pamoja na kuhakikisha kila mwananchi anapata Uhuru wake na kama jambo hilo likitekelezwa ipasavyo Fikra za Hayati Mwalimu J.K Nyerere zitakuwa zimeenziwa kwa weledi.
13:51
Sunday, 26 March 2017
SERENGETI BOYS WATIMBA BUKOBA, IKIRUDI KUIVAA GHANA
Serengeti Boys ni timu ya vijana ambayo imefuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Gabon kuanzia Mei 14, mwaka huu. Timu hiyo imepangwa Kundi ‘B’ pamoja na mabingwa watetezi Mali, Niger na Angola. Ina lengo la kurejea na Kombe la Afrika kwa vijana.
La ikitokea imekosa nafasi hiyo angalau ikafika nusu fainali ambako kwa mafanikio hayo itakuwa tayari ina tiketi mkononi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia huko India, Novemba, mwaka huu.
Kikosi cha Serengeti Boys kinaundwa na Makipa: Ramadhan Kabwili, Samwel Edward na Kelvin Kayego.
Walinzi: Kibwana Ally Shomari, Nickson Kibabage, Israel Mwenda, Dickson Job, Ally Msengi, Issa Makamba na Enrick Vitalis Nkosi.
Viungo: Kelvin Nashon Naftali, Ally Ng’anzi, Mohamed Rashid, Shaaban Ada, Mathias Juan, Marco Gerald, Abdulhamis Suleiman, Saidi Mussa na Cyprian Benedictor Mtesigwa.
Washambuliaji: Muhsin Malima Makame, Yohana Mkomola, Ibrahim Abdallah, Assad Juma na Abdul Suleiman.
16:54
Friday, 24 March 2017
URUGUAY YACHAPWA NYUMBANI MABAO r4-1 NA BRAZIL PAULINHO, APIGA HAT-TRICK YA HATARI
Paulinho akipiga shuti la umbali wa yadi 25 kufunga bao la kwanza dakika ya 19,nyota huyo alifunga mabao yake hayo matatu katika dakika 19, 52 na 90 katika ushindi wa 4-1 dhidi ya wenyeji Uruguay Uwanja wa Centenario mjini Montevideo Alfajiri ya leo katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia Urusi 2018 kwa kanda ya Amerika Kusini. Uruguay walitangulia kwa bao la penalti la mshambuliaji wa PSG, Edinson Cavani dakika ya tisa wakati bao lingine la Brazil lilifungwa na Neymar dakika ya 74 |
09:32
TIMU YA TAIFA YA RIADHA YAKABIDHIWA BENDERA ,YAELEKEA UGANDA NA MATUMAINI YA KUREJEA NA MEDALI
Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) Anthony Mtaka akikabidhi Bendera kwa manahodha wa timu ya taifa ya riadha kwa upande wa wanaume,Fabian Joseph (kushoto) na Magdalena Shauri (kulia)Wengine ni Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Nyamakumbati Mafuru (mwenye miwani) ,Meneja Mawasiliano wa TANAPA,Pascal Shelutete na kushoto ni Meneja wa timu ya taifa ya riadha Meta Petro.
Raisi wa Shirikisho la Riadha Tanzania ,Anthony Mtaka akizungumza na wanariadha 28 wanaoelekea nchini Uganda kwa ajili ya Mashindano ya Dunia ya Mbio za Nyika wakati wa hafla fupi ya kuwaaga iliyofanyika katika ofisi za Makao Makuu ya TANAPA jijini Arusha.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Nyamakumbati Mafuru akitoa neno kwa wanariadha hao,Shirika la Hifadhi za Taifa ndilo limedhamini wanariadha hao ambao idadi yao katika ushiriki wa mbio hizo imevunja rekodi ya tangu mwaka 1991.
Baadhi ya wanariadha watakao iwakilisha nchi katika mashindano hayo yatakayofanyika jumapili hii.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) Whilleam Gidabuday akizungumza wakati wa hafala hiyo.
Meneja Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Pascal Shelutete akizungumza wakati wa hafla ya kuwaaga wanariadha wa timu ya taifa iliyoandaliwa na shirika hilo jijini Arusha.
Kikosi cha wanariadha 28 na viongozi 12 kitakachopeperusha Bendera ya Taifa nchini Uganda katika Mashindano ya Dunia ya Mbio za Nyika yatakayofanyika Jumapili hii katika mji wa Entebe.
08:54
Subscribe to:
Posts (Atom)