BREAKING

Sunday, 27 March 2016

RAIS Dkt JOHN MAGUFULI ASHIRIKI IBADA YA PASAKA AWASIHI WATANZANIA KUWA NA UMOJA

Na Mwandishi Maalum

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewasihi watanzania kuendelea kuwa wamoja na kushirikiana kuijenga nchi yao, badala ya kubaguana.

Rais Magufuli ametoa wito huo leo katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Azania Front Jijini Dar es salaam, ambako amesali ibada ya Pasaka pamoja na waumini wa kanisa hilo.

Amesema Mwenyezi Mungu alimtoa mwanae wa pekee Yesu Kristo kuja kuikomboa dunia bila kuwabagua wanadamu, vivyo hivyo nasi binadamu tunapaswa kutobaguana, iwe kwa dini zetu, makabila yetu, mitazamo ya kisiasa na hata rangi zetu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akilakiwa na Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dkt. Alex Malasusa alipowasili kwa Ibada ya Pasaka katika Kanisa la KKKT la Azania Front jijini Dar es salaam leo Machi 27, 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Mkewe Mama Magufuli wakishiriki na waumini wengine Ibada ya Pasaka katika Kanisa la KKKT la Azania Front jijini Dar es salaam.
Kwaya wakati wa  Ibada ya Pasaka katika Kanisa la KKKT la Azania Front jijini Dar es salaam leo.
.................................

Aidha, Rais Magufuli amewakumbusha watanzania kufanya kazi kama ambavyo vitabu vitakatifu vinasisitiza umuhimu wa kufanya kazi, na amebainisha kuwa Tanzania yenye neema inawezekana endapo kila mtu atazingatia kufanya kazi.

“Tukifanya kazi hatuhitaji hata misaada kutoka nje, nchi hii ina neema nyingi. Kwa kweli tukifanya kazi kwa bidi nchi yetu inapaswa kuwa inatoa misaada kwa nchi nyingine na sio kuomba misaada kutoka nchi nyingine” Amesisitiza Dkt. Magufuli.

Rais Magufuli ambaye amesali kwenye kanisa hilo kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini ikiwa ni mara yake ya nne kusali katika kanisa hilo hata kabla ya kuwa Rais, amewaomba watanzania kuendelea kuliombea Taifa lao na pia kumuombea yeye ili afanikiwe kutekeleza jukumu kubwa na zito la kuiongoza nchi.

Pamoja na kuongoza maombi ya kumuombea Rais Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli waliohudhuria ibada hiyo, Askofu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dkt. Alex Malasusa amempongeza Rais Magufuli kwa tabia yake ya kupenda kuhudhuria ibada na kuwasihi viongozi wengine kupenda ibada.

Askofu Malasusa ameuelezea ufufuo wa Yesu Kristo kuwa jambo la kuleta  matumaini, na hivyo amepongeza mwelekeo wa nchi kwa sasa, huku akisema Kanisa linaona matumaini kwa Taifa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akisalimia waumini huku akisikilizwa na Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dkt. Alex Malasusa na Mchungaji Chalres Mzinga baada ya Ibada ya Pasaka katika Kanisa la KKKT la Azania Front jijini Dar es salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli  na Mkewe Mama Janeth Magufuli wakisalimiana na waumini baada ya Ibada ya Pasaka katika Kanisa la KKKT la Azania Front jijini Dar es salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli  akisalimiana na mtoto Javiera Lyimo (9) anayesoma darasa la tano shule ya Genesis jijini  baada ya  Ibada ya Pasaka katika Kanisa la KKKT la Azania Front jijini Dar es salaam leo Machi 27, 2016.

No comments:

Post a Comment

 
Copyright © 2016 Shamakala
Designed by Switch International | SHAMAKALA 360
    Twitter Facebook Google Plus Vimeo Videosmall Flickr YouTube