Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Shila Wilayani Nzega mkoani Tabora wakiwa wamebeba mbegu ya Viazi lishe wakielekea kwenye shamba darasa wakati wa uzinduzi wa shamba hilo wilayani humo leo. Shule hiyo ni shule pekee wilayani humo kupata bahati ya kuanzisha shamba hilo.
Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa COSTECH ambaye ni Ofisa Mwandamizi wa COSTECH, Audax Mutagwa (kulia), akimkabidhi mbegu ya mihogo Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Godfrey Ngapula kwa ajili ya kupandwa katika mashamba darasa katika uzinduzi wa mashamba hayo ya mbegu wilayani humo leo.
Wanafunzi wa Shule ya Shila wakiwa shambani wakati wa uzinduzi wa shamaba darasa hilo.
Ofisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Said Babu akizungumza kabla ya kuanza uzinduzi huo uliofanyika katika Wilaya hiyo Shule ya Msingi, Shila.
Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa COSTECH ambaye ni Ofisa Mwandamizi wa COSTECH, Audax Mutagwa, akizungumza katika uzinduzi huo.
Mtafiti wa mazao ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibura, akielezea ubora wa mbegu ya mihogo iliyofanyiwa utafiti kabla ya uzinduzi wa shamba darasa katika Shule ya Msingi ya Shila.
Kaimu Ofisa Ugani wa Halmshauri ya Wilaya ya Nzega, Hassan Mtomekela akizungumza katika uzinduzi huo.
Mtafiti wa mazao ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibura, akielekeza jinsi ya kupanda mbegu ya mihogo hiyo kiutaalamu.
Mtafiti wa mazao ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibura, akimuonesha mbegu hiyo mkuu wa wilaya hiyo.
Mkuu wa Wilaya hiyo akizindua shamba darasa hilo kwa kupanda mbegu ya mihogo katika Shule ya Msingi ya Shila.
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Gunguti Awadh Mzee akipanda mbegu hiyo.
Dada Mkuu wa Shule ya Shilwa, Maria Kulwa akipanda mbegu hiyo.
Upandaji ukiendelea katika shamba hilo.
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Gunguti Awadh Mzee, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu bahati iliyopata shule yake kwa kupatiwa mradi huo wa shamba la mbegu.
Mkulima wa Kijiji cha Shila, Zainabu Kanijo akizungumza na wanahabari.
Wanawake wa Kikundi cha Wasafi Camp Imala Makoye kilichopo Kijiji cha Iyombo Kata ya Utwigu wakiwa wamebeba mbegu ya Viazi lishe wakielekea kupanda katika shamba darasa.
Mtafiti wa mazao ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibura, akiwaelekeza wanakikundi hicho jinsi ya kupanda mbegu hiyo.
Wanawake wa Kikundi cha Wasafi Camp Imala Makoye kilichopo Kijiji cha Iyombo Kata ya Utwigu wakipanda mbegu hiyokatika shamba lao.
Wanawake wa Kikundi cha Wasafi Camp Imala Makoye kilichopo Kijiji cha Iyombo Kata ya Utwigu wakiimba nyimbo za kabila la kisukuma kufurahi mbegu hiyo.
Mtafiti wa mazao ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibura, akiwaelekeza wakulima wa Kijiji cha Upungu Kata ya Puge jinsi ya kupanda mbegu ya mihogo
MKUU wa Wilaya ya Nzega mkoani Tabora, Godfrey Ngapula amesema Sayansi na Teknolojia haiwezi kuepukika katika kilimo nchini.
Ngapula ameyasema hayo leo kwenye uzinduzi na kukabidhi mbegu bora za Mahindi ya Wema 2109, mihogo na Viazi lishe kwa ajili ya kuanzisha mashamba darasa katika vijiji vya Shila, Iyombo, Upungu, Lububu na Kapanga wilayani humo.
Mkuu huyo wa wilaya alisema ili kufanya kilimo chenye tija sayansi na teknolojia haiwezi kuepukika kutokana na changamoto mbalimbali zilizopo.
Alisema kilimo cha kisayansi kina tija kwani mkulima anaweza kulima eneo dogo na kupata mavuno mengi kuliko kilimo cha mazoea ambacho mkulima hulima shamba kubwa mazo kidogo.
Ngapula aliipongeza Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kuwapelekea mbegu hizo kwa kushirikiana na Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB)
Akizungumzia matumizi ya mbegu zilizozalishwa kwa teknolojia ya uhandisi jeni (GMO) alisema hayakwepeki kwa kuwa mbegu hizo zinasifa ya kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukame na wadudu waharibifu wa mazao.
Alisema wilaya hiyo kupelekewa mbegu hizo kwao ni fursa kubwa na kwa kushirikiana na wakulima na maofisa ugani atahakikisha mashamba darasa hayo yanatunzwa vizuri na kuwa ndio chanzo za kutoa mbegu nyingi na kuzisambaza katika maeneo mengine.
Mtafiti wa mazao ya mizizi kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibura aliwaambia wakulima hao kuwa hekta moja ya mihogo iwapo watalipa kwa kufuata ushauri wa wataalamu wataweza kupata tani 25 hadi 32 kwa zao la mihogo na viazi lishe watapata tani 7 hadi 9 kwa hekta moja.
Alisema matokeo hayo watayapata endapo watafuata kanuni bora za kilimo cha mazao hayo kwa kuzingatia nafasi kati ya mche na mche na mstari kwa mstari na matumizi ya mbolea hivyo wataweza kuongeza uzalishaji zaidi tofauti na sasa ambapo kwenye hekta moja ya mihogo wanapata tani nane hadi kumi wakati kwenye viazi lishe wanapata tani moja hadi 3.
Mtafiti huyo alisisitiza kuwa mbegu hiyo ya Mihogo ya Mkombozi imefanyiwa utafiti na kuonekana kustahimili magonjwa hatari ya mihogo ya batobato kali na michirizi ya kahawia ambayo imekuwa ikiwapatia hasara kubwa wakulima wengi na kupoteza hadi asilimia 90 za mazao.
Akizungumzia kuhusu mbegu Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi wa COSTECH ambaye ni Ofisa Mwandamizi wa COSTECH, Audax Mutagwa, alisema mbegu hizo ya mihogo aina ya Mkombozi imefanyiwa utafiti na kuonekana ina uwezo mkubwa wa kustahimili magonjwa kama ya batobato kali na michirizi ya kahawia ambayo imekuwa ikiwapatia hasara kubwa wakulima na ya mahindi ikistahimili hali ya ukame na kutoa mazao mengi.
Mutagwa aliwaomba wakulima hao kuyatunza mashamba hayo ambayo yamegharimu fedha nyingi hadi kukamilika kwake hivyo wayaendeleze kwa ajili ya kuja kutoa matunda kwa wakulima wa wilaya hiyo na kupata chakula cha kutosha na ziada kuuza.
Aliongeza kuwa kazi kubwa ya COSTECH ni kuishauri serikali katika masuala mbalimbali ya sayansi na teknolojia na kuhakikisha matokeo ya tafiti zinazofanyika nchini yanawafikia walengwa ambao ni wakulima.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Shila ambayo ni shule pekee iliyopata baada ya kuwa na shamba darasa la mihogo katika wilaya hiyo, Gunguti Awadh Mzee alisema shamba hilo litakuwa la mfano na kuwa mradi huo utasaidia kuwapatia wanafunzi wake chakula wakiwa shuleni hapo.
No comments:
Post a Comment