BREAKING

Monday, 12 June 2023

WAZIRI MKUU ATOA AGIZO KWA WAKUU WA MIKOA TANZANIA BARA





WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaelekeza Wakuu wa Mikoa yote ya Tanzania Bara, wakae na Mabaraza ya Biashara na Wamiliki wa kumbi za Starehe katika mikoa yao kwa madhumuni ya kutafuta muafaka wa pamoja katika utekelezaji wa sheria, kanuni, mwongozo kuhusu udhibiti wa athari zitokanazo na sauti zilizozidi viwango.

 Waziri Mkuu amezielekeza Idara za Mipangomiji katika halmashauri za wilaya zote nchini zitenge maeneo ya ujenzi wa nyumba za ibada kama wanavyotenga maeneo ya taasisi nyingine.  

Ametoa maelekezo hayo leo (Jumatatu, Juni 12, 2023) wakati akizindua Kongamano la Kujengewa Uelewa kuhusu madhara yatokanayo na sauti zilizozidi viwango katika nyumba za ibada. Kongamano hilo liloandaliwa na Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) limefanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Amesema ipo miongozo inayosimamiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inayohusu masuala ya usimamizi wa mipango miji. “Nasisitiza toeni miongozo mahsusi ya mipango ya matumizi ya ardhi .” 

“Kwa upande wa udhibiti wa sauti zilizozidi, kila mamlaka iliyotoa vibali au leseni ya shughuli au biashara, zifuatilie mwenendo wa matumizi ya leseni hizo. Nasisitiza kuwa kila mamlaka itimize wajibu wake kulingana na maelekezo yaliyimo katika Mwongozo wa Uthibiti wa Uchafuzi wa Mazingira Utokanao na Kelele na Mitetemo uliotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais.”

No comments:

Post a Comment

 
Copyright © 2016 Shamakala
Designed by Switch International | SHAMAKALA 360
    Twitter Facebook Google Plus Vimeo Videosmall Flickr YouTube