BREAKING

Wednesday, 25 October 2023

TAWA YAFADHILI MRADI WA UJENZI WA MADARASA KALIUA, WANAFUNZI WAELEZA HISIA ZAO.







SERIKALI kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imefadhili mradi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa mawili, ofisi moja ya walimu na jumla ya madawati 30 katika shule ya msingi Usinge iliyopo wilaya ya kaliua Mkoani Tabora

Mradi huu ambao tayari umekwishakamilika na kuanza kutumika umegharimu kiasi cha Tsh. Millioni 50 (50,000,000/=) ambazo ni fedha zinazotokana na bajeti ya ndani ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA

Akiongea na waandishi wa habari katika ziara ya ukaguzi wa mradi huo wa maendeleo kwa jamii Oktoba 24, 2023 Afisa habari wa TAWA Beatus Maganja ameeleza kuwa TAWA iliona adha wanazozipata wanafunzi wa Shule ya msingi Usinge kwa kukosa madarasa ya kutosha, ofisi ya walimu pamoja na madawati hivyo ikaona vyema kufadhili mradi huo ili kuwapunguzia adha hizo na kuwapa fursa wananchi kuona faida zitokanazo na shughuli za uhifadhi na  umuhimu wa uwepo wa Taasisi hiyo katika maeneo yao 

"Ifahamike kuwa changamoto  kubwa katika vijiji vinavyozunguka hifadhi ni kwamba shule nyingi zinakosa madarasa na madawati ya kutosha lakini pia wanakosa nyenzo mbalimbali za kuwawezesha wao kuweza kusoma katika mazingira bora" amesema

"..kwahiyo Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania iliona vyema kufadhili miradi hii ili kuwawezesha wananchi wanaozunguka maeneo haya kufaidi rasilimali hizi za Wanyamapori na uhifadhi kwa ujumla" ameongeza

Salma Madua Ally ambaye ni mwanafunzi wa darasa la sita katika shule hiyo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dr. Samia Suluhu Hassan na Taasisi ya TAWA kwa ufadhili huo  ambao ameuelezea kama ni msaada mkubwa kwao ambao hawakuutegemea kwani umepelekea kuongeza uwezo wao wa uelewa na ufaulu darasani

"Nawashukuru wasimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA pia tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea madarasa ambayo hatukutegemea kuwa nayo, pia madarasa haya yametufanya tuweze kuwa tunafaulu na kuwa tunaelewa vizuri" amesema

"...Kipindi cha nyuma tulikuwa tunakaa darasa moja watu wengi, tulikuwa hatuwezi kuelewa kwa urahisi lakini saizi tumegawanyishwa madarasa" ameongeza

Naye Joseph Paulo mwanafunzi wa Shule hiyo ameeleza kuwa kabla ya ujenzi wa madarasa  na kufadhiliwa madawati hayo walikuwa wakikaa chini huku wanafunzi wachache wakikalia madawati hali ambayo ilifanya  nguo zao zichafuke na kukosa umakini darasani, lakini kwa sasa wote wanakaa  kwenye madawati na kusomea kwenye vyumba vizuri vya madarasa

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Bw. Ibrahimu Bakari Juma ameeleza kuwa shule ya Usinge ilikuwa na uhaba wa vyumba sita vya madarasa pamoja na madawati 90 hivyo ufadhili huo uliotolewa na Serikali kupitia TAWA umewezesha idadi ya wanafunzi 90 kukaa kwenye madawati

Aidha ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Dr. Samia Suluhu Hassan lakini pia ameelekeza pongezi na shukrani zake kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA kwa ufadhili huo

No comments:

Post a Comment

 
Copyright © 2016 Shamakala
Designed by Switch International | SHAMAKALA 360
    Twitter Facebook Google Plus Vimeo Videosmall Flickr YouTube