BREAKING

Wednesday, 30 July 2025

BAADA YA JINA LAKE KUKATWA; ALEX MSAMA ATOA NENO

Siku moja tu baada ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuondoa jina lake miongoni mwa watia nia wa Jimbo la Ubunge Ukonga jijini Dar, aliyetia nia, Alex Msama ametoa neno zito.

Msama ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Msama Promotions & Dira Media ametoa neno kwa kuwataka watia nia wote waliokatwa majina yao nchini kote kutoa ushirikiano kwa wale ambao majina yao yanakwenda kupigiwa Kura za Maoni ngazi ya kata na hatimaye kumpata mgombea mmoja atakayepeperusha bendera ya CCM kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Huyu hapa Alex Msama: "Nilitia nia kuomba kuteuliwa na chama changu kugombea Ubunge Jimbo la Ukonga. Lakini isivyo bahati jina langu halikurudi.

"Siyo kwamba sifai. Nafaa ila jina langu halikurudi. Kwa wakati huu wamepatikana wengine ambao wamepewa nafasi na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya chama chetu ili kuendelea na mchakato.

"Sisi sote ni wana CCM. Kwa hiyo wote tuna sifa ila waliopitishwa wanafaa kwa sasa. Nawaomba watia nia wengine wote ambao pia majina yao hayakurudi, tuwape ushirikiano wale ambao majina yao yamerudi. Hiki ni kipindi cha kushikamana badala ya kusambaratika. 

"Kwa hiyo niwaombe wale wote waliotia nia kama mimi lakini majina yao hayakurudi, tushikamane kwa nia ya dhati ya kuendelea kukiweka chama chetu katika umoja ili kumsaidia Mwenyekiti wa CCM-Taifa. Mama yetu, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan."

Msama aliendelea kusema kuwa, katika kipindi hiki hategemei kuwepo kwa makundi kwa sababu ya majina yao kutorudi au kukatwa.

Akasema: "Kama watia nia wenzangu walimsikiliza vizuri Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Amos Makalla baada ya kumaliza kusoma majina yaliyorudi, alisema wote ambao majina yao hayakurudi tuwe watulivu bado chama kina mahitaji mengi. Kwa hiyo tutulie na kushikamana."

AZUNGUMZIA MAREKEBISHO YA KATIBA YA CCM HIVI KARIBUNI 

Aidha, Msama alisema kuwa, wazo la viongozi wa CCM kuamua kurekebisha taratibu ya kurudisha majina mengi badala ya matatu kama ilivyokuwa awali ni wazo la busara na la maana sana.

No comments:

Post a Comment

 
Copyright © 2016 Shamakala
Designed by Switch International | SHAMAKALA 360
    Twitter Facebook Google Plus Vimeo Videosmall Flickr YouTube