Klabu ya Simba ya Dar es Salaam imeingiza wachezaji wawili kwenye kinyang’anyiro cha tuzo ya Mwanasoka Bora wa Klabu Afrika ambayo itatolewa Jumanne ya Januari 7 mwakani katika kilele cha Tuzo ya Mwasoka Bora barani ukumbi wa Citadel Azure, Hurghada nchini Misri.
Hao ni washambuliaji Mnyarwanda Meddi Kagere na Mganda Emmnaule Okwi ambaye hata hivyo amehamia Al Ittihad ya Misri.
Wachezaji hao wameingizwa kwenye kinyang’anyiro hicho baada ya kuiwezesha Simba SC kufika Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita ambako walitolewa na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Ikiwa chini ya kocha Mbelgiji, Simba SC ilizipiku JS Saoura ya Algeria na AS Vita ya DRC baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye Kundi D, ikizidiwa pointi moja na mabingwa wa kihistoria Afrika, Al Ahly ya Misri iliyoongoza kwa pointi zake 10.
Na hiyo ni baada ya kuzitoa Mbabane Swallows ya Swaziland kwa jumla ya mabao 8-1, ikishinda 4-1 nyumbani na 4-0 ugenini na Nkana FC ya Zambia kwa jumla ya mabao 4-3, ikishinda 3-1 Dar es Salaam baada ya kufungwa 2-1 Zambia katika hatua ya mchujo.
Esperance waliopewa ubingwa baada ya Wydad Casablanca kugomea mechi ya marudiano ya fainali dakika ya 59 baada ya refa kukataa bao lao, imetoa wachezaji watano kwenye kinyang’anyiro hicho ambao ni Anice Badri, Taha Yassine Khenissi wote Watunisia, Fousseny Coulibaly wa Ivory Coast, Franck Kom wa Cameroon, Youcef Belaili wa Algeria ambaye amehamia Ahli ya Jeddah.
Zamalek ya Misri imetoa wachezaji watatu, Ferjani Sassi wa Tunisia na watoto wa nyumbani, Mahmoud Alaa na Tarek Hamed, wakati wapinzani wao wa jadi, Al Ahly wametoa mchezaji mmoja, Mtunisia Ali Maaloul.
Wydad Casablanca imetoa wachezaji wawili pia Ismail El Haddad na Walid El Karti wote wa Morocco, sawa na TP Mazembe Meschack Elia na Tresor Mputu wote wa Kongo na Mamelodi Sundowns, Mganda Denis Onyango na Themba Zwane wa Afrika Kusini. Wengine ni Herenilson wa Petro de Luanda ya nyumbani, Angola, Jean Marc Makusu wa AS Vita ya nyumbani Kongo na Mtogo Kodjo Fo Doh Laba wa RS Berkane ya Morocco aliyehamia Al Ain ya Abu Dhabi.
No comments:
Post a Comment