Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo ametoa wito kwa wadau wa elimu kuendelea kutoa maoni katika hatua mbalimbali za maandalizi ya Mpango wa tatu wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu ili kuongeza wigo na ubora wa elimu inayotolewa kwa Watanzania.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam wakati akifungua kikao cha wadau wa maendeleo sekta ya elimu wakati wakijadili taarifa ya uchambuzi wa hali halisi ya sekta ya elimu kwa mustakabali wa uimarishaji wa Sekta amesema Wizara ipo katika uandaaji wa Mpango Tatu wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu (2021/22 - 2025/26), hivyo ni ni jambo zuri kufanya uchambuzi wa hali halisi ya sekta katika kipindi cha utekelezaji wa mpango uliomalizika ili kujua yale yaliyopangwa yamefanikiwa kwa kiasi gani.
“Wengi wenu mtakuwa mnatambua kuwa Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu Awamu ya pili (2016/17 - 2020/21) umemalizika, Hivyo uandaaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu (2021/22- 2025/26) umeanza na hatua ya kwanza ni kufanya tathmini ya hali halisi ya sekta katika kipindi cha utekelezaji wa mpango uliomalizika muda wake. Kazi hiyo ya kufanya uchambuzi ndio iliyotukusanya hapa siku hii leo hivyo nawaomba mtoe mchango wenu katika taarifa hii na mapendekezo ya namna ya kuboresha sekta ya elimu nchini,” amesema Katibu Mkuu Akwilapo
Amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa wadau katika kuwahudumia watanzania wote kwa kutoa elimu bora katika ngazi zote, kuanzia elimu ya awali hadi Chuo kikuu na kwamba Wizara itaendelea kushirikiana nao kwa karibu na kuweka mazingira rafiki na wezeshi ili kuharakisha azma ya Serikali ya kuleta maendeleo kwa wananchi
Katibu Mkuu Akwilapo ametumia fursa hiyo kuwashukuru wadau ambao wamegharimia zoezi la uchambuzi wa hali ya sekta ya elimu hapa nchini, ambao ni Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza Benki ya Dunia na UNICEF ambao wamekuwa wasimizi Wakuu wa zoezi zima la tathmini ya sekta. Pia amewapongeza Washauri Elekezi, kitaifa na kimataifa waliotekeleza zoezi la uchambuzi kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Fedha na Mipango.
Kwa upande wake Naibu Katibu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Gerald Mweli amesema kila baada ya miaka mitano Serikali imekuwa ikiandaa Mpango unaotoa mwelekeo wa namna ya kuboresha utoaji wa elimu nchini ili kujua mafanikio na changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa mpango ulioisha.
Aidha amebainisha TAMISEMI imepewa jukumu la kusimamia utoaji wa elimu msingi na sekondari nchini na kwamba kwa mwaka huu wa fedha wamefanikiwa kuajiri walimu wanaofundisha elimu ya msingi na sekondari elfu 14,949 ikiwa ni sambamba ujenzi wa miundombinu ili kuhakikisha ufundishaji unaendelea na katika mazingira yaliyoimarishwa.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Elimu Tanzania Lydia Wilbard ameonesha furaha yake kwa Serikali kufanya kikao hicho na kuwashirikisha wadau amesema ni utaratibu mzuri ndani ya serikali katika kuhakikisha kwamba Sekta ya elimu inapojadiliwa inahusisha wadau wa elimu kwani utekelezaji wa mipango ni jumuishi
“Kushirikishwa kwetu sisi wadau tunapata fursa ya kuona kwa undani sekta yetu elimu imekwendaje na kutusaidia kupanga mikakati maalum ambayo italeta matokeo chanya katika kupanga mkakati unaokuja,”amesema Lydia Makamu Mwenyekiti Bodi ya TENMET.