NA SAID MWISHEHE
KAMPUNI ya mafuta ya Puma Energy, imeunga mkono kampeni ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ya kuokoa maisha maisha watoto wanaogua ugonjwa wa moyo kwa kuchangia Sh milioni 40 ili kufanikisha upasuaji kwa watoto 20.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana mashindano ya michoro ya Usalama Barabarani kwa wanafunzi wa mkoa humo kwa mwaka 2019, Mkurugenzi wa Puma Energy, Dominic Dhanah, alisema hatua ya kuunga mkono kampeni hiyo ni kuhakikisha wanaokoa maisha ya watoto ambao wazazi wao hawana uwezo wa kugharamia matibabu.
Akizungumzia mafunzo ya usalama barabarani kwa watoto wa shule za msingi, alisema yamesaidia kupunguza ajali katika maeneo ambayo wametoa mafunzo hivyo wanaamini kwa kufanya hivyo wanaokoa kizazi cha sasa na kijacho kwa kuwa elimu ya matumizi bora ya barabara inaendelea kusambaa.
“Lengo kubwa la mpango huu ni kuwafanya watoto hawa kuwa na uelewa wa matumizi ya barabara wakiwa bado wadogo. Tunaamini kwa kufanya hivyo tunawaongezea uelewa kuhusu dhima nzima ya usalama barabarani kwa wa Tanzania wengi zaidi,” alisema Dhanah.
Alisema kazi hiyo kwa mwaka huu imefanyika katika mikoa ya Dodoma na visiwani Zanzibar ambapo jumla ya shule 34 zitafikiwa kwa mpango huu kwa mwaka 2019.
“Lengo letu kama kampuni ni kuongeza wigo ili kufikia shule nyingi Zaidi nchi nzima. Pia tutaendelea kuwekeza katika kampeni ya usalama barabarani ikishirikiana na serikali kupitia Jeshi la Polisi ili kuokoa maisha ya Watanzania,” alisema
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alisema kuwa Kampuni ya Puma, imetoa kiasi cha Sh milioni 40 ambapo wamegharamia matibabu ya watoto 20 ambao wanahitaji kufanyiwa upasuaji wa moyo lakini wazazi mwao hawana uwezo wa kulipia matibabu.
“Puma wameonesha njia ya kujali na kutusaidia kwenye moyo. Niliomba msaada huo katika mkutano wa SADC. Nina watoto 500 pale Muhimbili wanaumwa moyo.
“Mimi nikialikwa mahali ninaomba msaada kwa wananchi wangu. Dominick wa Puma nilimuomba na gharama za matibabu kwa kila mtoto ni Shilingi milioni mbili kwa kiasi hiki cha fedha Shilingi milioni 40 sasa tunakwenda kurudisha tabasabu kwa watoto 20.
“Watapata operesheni kwakuwa sehemu ya faraja na mafanikio kwa mtoto atakayefanyiwa opesheni. Hata nilipokutana na Balozi wa Dubai baada ya kumueleza hili, yeye alikwenda kuleta madaktari ambao walifanya upasuaji wa matibabu kwa watoto 50. Mwezi ujao nitaunda kamati ya watu saba kwa ajili ya kusaka Shilingi bilioni moja, ili mpaka tukifika Desemba mwaka huu watoto wote wawe wamefanyiwa upasuaji,” alisema Makonda
Akizungumzia idadi ya watu wanaopata ajali za barabarani, alisema kuwa kwa sasa imepungua kutokana na elimu ya usalama barabarani.
“Tuna imani watoto 1m atakuwa na uelewa iwapo wataelimishwa na wenzao. Watumia vyombo vya moto watambue kila mmoja ana jukumu la kufuata usalama barabarani. Kabla ya Desemba kutakuwa na check up ya bure kwa wanaotaka kwenda likizo.
“Mafundi wa bure watakuwapo, nataka waende vizuri kula likizo na warejee tena Dar wakiwa salama. Trafiki kwenye mwendokasi inafanya vibaya,” alisema
Hata hivyo Makonda aliagiza kukamatwa kwa madereva wanaotumia barabara za mwendokasi.
“Wanatumia barabara ya mwendokasi wakamatwe hakuna gari, pikipiki wala mtu anayepaswa kuitumia, Mwakyoma (RTO), apeleke trafiki hapo,” alisema
Mpaka sasa wanafunzi zaidi ya 20,000 wa shule za msingi katika shule tisa za Jiji la Dar essalaam wamepata mafunzo ya usalama barabarani ambapo katika mashindano hayo Shule ya Msingi Kibamba iliibuka mshindi wa kwanza na kuzawadiwa Sh milioni nne.
No comments:
Post a Comment