BREAKING

Wednesday, 21 December 2022

TMDA YAWAPIGA MSASA WAKAGUZI WA DAWA NA VIFAA TIBA MKONI IRINGA.



Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kanda ya kati Sonia Mkumbwa akitoa mafunzo kwa wakaguzi wa Dawa na vifaa tiba mkoani Iringa
Viongozi mbalimbali wa mkoa wa Iringa wakiongozwa na mganga mkuu pamoja na kaimu katibu tawala mkoa wa Iringa,Elias luvanda wakati wa kufungua mafunzo kwa wakaguzi wa dawa na vifaa tiba mkoani Iringa
Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kanda ya kati Sonia Mkumbwa akitoa mafunzo kwa wakaguzi wa Dawa na vifaa tiba mkoani Iringa


Na Fredy Mgunda,Iringa.

 

 

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kuwajengea uwezo wataalamu wa ukaguzi wa dawa na vifaa tiba katika Halmashauri zote za Mkoa wa Iringa kwa lengo la kuboresha ufanisi wa kazi wawapo kazini ili kulinda afya za watumiaji wad awa na vifaa tiba.

 

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo kaimu katibu tawala mkoa wa Iringa,Elias luvanda alisema kuwa ni kielelezo tosha kuwa wakaguzi ngazi ya Halmashauri mnathamini mchango wa TMDA katika kuwapa elimu kuhusu namna bora ya kutekeleza majukumu na  kulinda Afya za wananchi ili waweze kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa letu la Tanzania.

 

Luvanda alisema kuwa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya Afya, yenye jukumu la kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa Dawa, Vifaa Tiba na Vitendanishi na Taasisi hiyo imeundwa chini ya sheria ya Dawa na Vifaa Tiba sura 219.

Alisema kuwa majukumu yanayofanywa na TMDA na yale yaliyokasimishwa kwenu, lengo lake ni lilelile la kulinda afya ya jamii kwa kuzuia athari zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi. 

 

“Kwa kutambua jukumu zito la TMDA, Serikali iliona ni vema kukasimu baadhi ya madaraka na majukumu yao kwa Halmashauri kwa lengo la kusogeza karibu na wananchi huduma za udhibiti wa ubora na usalama wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi”alisema Luvanda

 

Luvanda aliwataka watendaji wote kufanya kazi kwa kutoa taarifa zilizo sahihi kwa wakati unatakiwa ili kurahisisha utendaji wa taasisi hiyo hivyo Mwongozo wa Kukasimu Madaraka na Majukumu umebainisha wazi kuwa taarifa za utendaji kazi za robo mwaka na taarifa za ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa kazi za udhibiti wa ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa zinazodhibitiwa katika soko zinatakiwa kuandaliwa na kutumwa TMDA kupitia viongozi wa ngazi ya Halmashauri.

 

“Ni mategemeo yangu kwamba mafunzo haya yatatoa maelekezo ya namna ya kuboresha utendaji kazi wenu, na kuondoa changamoto zinazojitokeza mara kwa mara kuwa, wakaguzi wa Halmashauri wanatumia nguvu nyingi nyakati za kaguzi ambazo husababishwa na kutokutoa elimu kwa wateja (wafanyabiashara) Hivyo kukinzana na utaratibu wa ukaguzi wa TMDA ambao umejikita zaidi katika kuelimisha na kuwezesha” alisema Luvanda.

 

Alimalizia kwa kusema kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa itafanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa maagizo na makubaliano yatakayowekwa ili kuhakikisha wananchi wanahakikishiwa upatikanaji wa bidhaa bora na salama.

Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kanda ya kati Sonia Mkumbwa alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwaongezea ujuzi wakaguzi ili waweze kufanya kazi ya ukaguzi kwa kuzingatia sheria.

Mkubwa alisema kuwa wakaguzi watatekeleza kazi zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo kama zilivyotolewa na TMDA kama vile Kufanya ukaguzi wa maeneo yanayohusika na utunzaji, uuzaji na usambazaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi, Kufanya ufuatiliaji na kutoa taarifa za ubora na usalama wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi katika soko.

 

Aliongeza kuwa wakaguzi watatakiwa kuchukua sampuli za bidhaa zinazodhibitiwa kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara pale inapohitajika na kufanya ufuatiliaji wa madhara/matukio yanayohisiwa kusababishwa na matumizi ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi.

 

 Mkumbwa alisema kuwa wakaguzi wanatakiwa kufanya uhakiki wa bidhaa zisizofaa kwa matumizi kabla ya uteketezaji kwa kujaza fomu ya uhakiki (Kiambatisho Na.7) baada ya mawasiliano na Ofisi ya Kanda ya TMDA na kusimamia zoezi la kuteketeza bidhaa ambazo hazifai kwa matumizi baada ya uhakiki na kisha kujaza fomu ya uteketezaji (Kiambatisho Na. 8) na kuiwasilisha ofisi ya Kanda ya TMDA kwa ajili ya kuandaa cheti cha uteketezaji.

 

Alimazia kwa kuwasema kuwa kila Halmashauri itaandaa na kuwasilisha taarifa za utendaji kazi kwenye Ofisi za TMDA za Kanda  na kuwasilisha nakala kwa Katibu Tawala wa Mkoa ambazo ni taarifa ya utendaji ya robo mwaka na taarifa ya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa kazi za udhibiti wa ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa katika soko.

Tuesday, 30 August 2022

MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA DKT. PHILIP MPANGO AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA SINGAPORE NCHINI TANZANIA


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akifanya mazungumzo na Balozi wa Singapore nchini Tanzania Mhe. Douglas Foo, Mazungumzo yaliofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma leo Tarehe 30 Agosti 2022






Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Singapore nchini Tanzania Mhe.Douglas Foo mara baada ya Mazungumzo yaliofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma leo Tarehe 30 Agosti 2022

Na Mwandishi wetu Ofisi ya Makamu wa Rais..

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 30 Agosti 2022 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Singapore nchini Tanzania Mhe. Douglas Foo, Mazungumzo yaliofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.

 Katika Mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amesema Tanzania ipo tayari kushirikiana na Singapore katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya Bandari, Afya, Viwanda, Elimu, Kilimo, Biashara, Uchumi wa Buluu pamoja na Tehama kupitia uwekezaji katika vifaa vya kielekroniki.

 Amesema serikali ya awamu ya sita imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara hapa nchini ikiwa ni pamoja kushirikiana na mataifa katika masuala mbalimbali na kuhakikisha sera zilizopo ni thabiti na zisizobadilika badilika.

 Makamu wa Rais amesema serikali imeweka mkazo katika kuboresha rasilimali watu ikiwemo kuhakikisha elimu ya msingi na sekondari inatolewa bila malipo, kujenga miundombinu ya elimu pamoja na msisitizo wa elimu ya sayansi husasani kwa wanafunzi wa kike. Pia amesema uwekezaji unafanyika katika sekta ya afya, upatikanaji wa maji safi na salama, ujenzi wa miundombinu ya barabara kuunganisha mikoa na vijiji, kuhakikisha upatikanaji wa nishati pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa.

 Halikadhalika, Makamu wa Rais amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Singapore kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini ikiwemo katika miundombinu ya utalii, kuwekeza katika viwanda na teknolojia rafiki za kuongeza thamani ya mazao ya kilimo pamoja na madini. Aidha amesema kutokana na mafanikio yaliopatikana nchini Singapore katika sekta ya bandari, ipo haja ya kuongeza ushirikiano utakaowezesha mafunzo ya watendaji wa Bandari pamoja  upatikanaji wa mitambo ya kisasa.

 Kwa Upande wake Balozi wa Singapore nchini Tanzania Mheshimiwa Douglas Foo amesema Singapore inatarajia kuongeza ushirikiano na Tanzania katika maeneo mbalimbali hususani biashara na uwekezaji. Ameongeza kwamba kutokana na nchi hiyo  kuwa eneo dogo kwaajili ya shughuli za kilimo hivyo ipo tija kubwa katika ushirikiano na Tanzania kwenye sekta hiyo itakayowezesha kuongezwa thamani ya mazao na kufikia soko la nchi hiyo na nchi zinginezo za bara la Asia.

 Aidha ameikaribisha Tanzania kushirikiana na Singapore katika sekta ya utalii, Uvuvi na uchumi wa Buluu kwa ujumla. Amesema nchi hiyo sekta ya uzalishaji wa viwandani inachangia asilimia 20 katika pato la taifa hivyo ipo tayari kushirikiana na Tanzania kwa kuanzisha viwanda vya uzalishaji pamoja na kutoa elimu ya ufundi hapa nchini itakayoongeza tija katika viwanda hivyo

Pia Amesema Singapore imeendelea na uwekezaji katika teknolojia unaorahisisha ufanyaji kazi pamoja na ufuatiliaji wa masuala mbalimbali ikiwemo masuala ya kiafya na kielimu. Ameongeza kwamba nchi hiyo imeweka mkazo katika utunzaji wa mazingira ikiwemo kuwaka faini kubwa kwa wachafuzi wa mazingira huku ikitarajia kuondoa kabisa uzalishaji wa hewa ukaa ifikapo mwaka 2050. 

MKOMI: LINDENI MALIASILI ZA TAIFA


Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Juma Mkomi akizungmza na Wahifadhi wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Wenyeviti wa Sekretarieti na Maafisa wa Kanda kumi za kiikolojia katika nyanja za intelijensia, uchunguzi na mashtaka ambapo amewataka mafunzo watakayoyapata wayatafsiri kwa vitendo. 

Baadhi ya Wenyeviti wa Kanda za Kiikolojia wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Juma Mkomi wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo Wahifadhi katika nyanja za intelijensia, uchunguzi na mashtaka.

Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Juma Mkomi (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Sekretarieti ya Mafunzo akizungmza  ya kuwajengea uwezo Wenyeviti wa Sekretarieti na Maafisa wa Kanda kumi za kiikolojia mara baada ya kufungua mafunzo hayo.

NAIBU Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Juma Mkomi amewataka Wahifadhi  kwenda kusimamia jukumu ya msingi la Wizara ya Maliasili na Utalii  ambalo ni kulinda na kuhifadhi maliasili za Taifa ikiwemo Misitu na Wanyamapori

 Mkomi  ameyasema hayo leo Jumanne Agosti 30, 2022  Jijini Arusha wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Wenyeviti wa Sekretarieti na Maafisa wa Kanda kumi za kiikolojia katika nyanja za intelijensia, uchunguzi na mashtaka

Mafunzo hayo yanayofanyika kwa muda wa siku mbili kuanzia leo yamehudhuriwa na  Washiriki kutoka  Jeshi la Polisi nchini ,  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Wahifadhi  kutoka TANAPA, NCAA, TAWA na TFS, 

Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo, Mkomi amesema Wahifadhi  wana wajibu wa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama  katika kuwabaini majangili wa wanyamapori na Misitu

Amewataka Washiriki hao kuzingatia mafunzo hayo   na kwenda kuyafanyia kazi kwa kuhakikisha Wahalifu wa wanyamapori na misitu wanakamatwa kabla ya kuharibu Maliasili zetu.  

“ Mafunzo hayo mtakayopewa yakawe chachu katika kuchagiza utalii hivi sasa  filamu ya Royal Tour  imeitangaza vizuri nchi yetu na  Watalii wameanza kumiminika nchini kutokana na kazi kubwa mnayofanya ninyi Wahifadhi msingekuwa mmefanya kazi kubwa kulinda wanyamapori watalii wasingekuja kwa sababu kusingekuwa na wanyamapori ,” amesema.

Kutokana na jukumu walilonalo la kulinda Maliasili, Naibu Katibu Mkuu, Mkomi amewataka wahifadhi hao kuzingatia mafunzo hayo hususani suala la uchunguzi kwa kujifunza mbinu za kuzuia uharibifu wowote unaoweza kutokea kwenye maeneo ya hifadhi 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Wanyamapori, Dkt. Maurus Msuha  amesema suala la Uhifadhi linakabiliwa na changamoto ya usimamizi wa Maliasili hivyo  mafunzo hayo yakalete majawabu katika kulinda maliasili

Pia Dkt. Msuha amesema  mafunzo hayo  yanakwenda kuboresha utendaji kazi kwa kuhakikisha uhalifu wa wanyamapori na Misitu litachochea ufanisi zaidi katika utendaji w kazi wa kulinda maliasili zetu.

Naye Mratibu wa Mafunzo hayo ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Wanyamapori, Robert Mande amesema mafunzo hayo ni muendelezo wa kukumbushana namna ya kushughulika na waharifu wa wanyamapori wa misitu mara wanapokamtwa.

“Lazima tuhakikishe kuwa tunalinda rasilimali za wanyamapori ili watalii wanavyokuja waweze kuziona na waweze kuwa na usalama”Mande amefafanua.

RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA SAMIA SULUHU HASSAN AFUNGUA KIKAO KAZI CHA MAAFISA WAKUU WA POLISI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati akifungua Kikao Kazi Cha Maafisa Wakuu Waandamizi wa Makao Makuu ya Polisi na Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi kilichofanyika katika Chuo cha Polisi (CCP) Mkoani Kilimanjaro tarehe 30 Agosti, 2022.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na viongozi wengine katika picha ya pamoja na Maafisa Wakuu Waandamizi wa Makao Makuu ya Polisi na Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi mara baada ya kufungua Kikao Kazi cha Makamanda hao kilichofanyika kwenye Chuo cha Polisi (CCP) Mkoani Kilimanjaro tarehe 30 Agosti, 2022.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati akifungua Kikao Kazi Cha Maafisa Wakuu Waandamizi wa Makao Makuu ya Polisi na Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi kilichofanyika katika Chuo cha Polisi (CCP) Mkoani Kilimanjaro tarehe 30 Agosti, 2022.







Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan akiagana na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu mara baada ya kufungua Kikao Kazi cha Makamanda hao kilichofanyika kwenye Chuo cha Polisi (CCP) Mkoani Kilimanjaro tarehe 30 Agosti, 2022.


 

Tuesday, 19 July 2022

MHE.RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA SAMIA SULUHU HASSAN APOKEA UGENI MAALUM KUTOKA JAMHURI YA KIDEMOKRASI DRC


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na  Mjumbe Maalum Prof. Serge Tshabangu aliyewasilisha Ujumbe Maalum kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Mhe. Felix Antonio Tshisekedi Ikulu Chamwino Jijini Dodoma tarehe 19 Julai 2022.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea Ujumbe Maalum kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Mhe. Felix Antonio Tshisekedi uliowasilishwa na Mjumbe Maalum Prof. Serge Tshabangu Ikulu Chamwino Jijini Dodoma tarehe 19 Julai 2022.

Wednesday, 11 May 2022

TANESCO KUNUNUA NGUZO ZA UMEME NCHINI,WAZIRI ATANGAZA MASHARTI YAKE.


Waziri wa nishati January Makamba akiongea na wadau wa nguzo za umeme mkoani Iringa akiwaondolea sitofaumu iliyokuwepo ya kutonunua nguzo zao
Waziri wa nishati January Makamba akiwasikiliza wadau wa nguzo za umeme mkoani Iringa akiwaondolea sitofaumu iliyokuwepo ya kutonunua nguzo zaoWaziri wa nishati January Makambaakiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Queen Sendiga wakati wa majadiliano ya kuondoa sitofaumu iliyokuwepo ya kutonunua nguzo zao

 

Na Fredy Mgunda,Iringa.

WAZIRI wa nishati January Makamba ameliagiza shirika la umeme Tanzania (TANESCO) kuingia zabuni za ununuzi wa nguzo za kusambaza umeme kwa wakandarasi wanaokidhi vigezo,ikiwemo kuthibitisha baadhi ya nguzo zimetoka kwa wazalishaji wadogo wa ndani.

Waziri Makamba alisema kuwa TANESCO inatakiwa kushirikiana na taasisi zinazosimamia ubora wa bidhaa,ikiwepo shirika la viwango nchini (TBS) ili kuhakikisha nguzo zinazonunuliwa zinakidhi viwango vinavyotakiwa na shirika hilo.

Makamba alisema kuwa ili kuondoa changamoto kwa wadau wa nguzo na serikali ataunda kamati y wadau wa nguzo watakaokuwa wanafuatilia namna ya utengenezaji wa nguzo bora za umeme ambao utasaidia kuuza nje ya nchi ambavyo wadau wanguzo nchi nyingine wanafanya kwa ubora unaotakiwa.

“Sasa ipo mifano ya mfumo huu wa uwekezaji wa viwanda vya nguzo,nchi kama Afrika Kusini inamfumo mzuri sana na serikali yenu ipo tayari kuwachukua watu kadhaa kwenye kila wadau na kuwapeleka na kuwalipia mkajifunze kuhusu mfumo wa kudhibiti na kuhusu ubora” alisema makamba

Aidha aliwatoa hofu wadau wa nguzo za Miti za Umeme nchini kwa kuwahakikishia soko la kuuza nguzo zenye ubora kwa Shirika la Umeme nchini( TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini ( REA), hapa nchini.

Makamba alisema kuwa mkutano ulilenga kuondoa sintofahamu pamoja na minong’ono inayoendelea kwa baadhi ya watu wanaopotosha kuwa Serikali haitanunua nguzo za Umeme za ndani na badala yake zitaagizwa kutoka nje ya Nchi.

Katika mazungumzo yake na Wadau hao, Makamba alisema kuwa, Serikali itaendelea kununua nguzo za miti za Umeme kutoka kwa wazalishaji wa ndani ili kulinda viwanda vya ndani kwa kuzingatia ubora wa nguzo uliowekwa.

“Tutakapo toa zabuni ili ufanikiwe kupata zabuni hiyo lazima angalau asilimia Fulani ya nguzo hizo utakazouza ziwe zimetoka ka watu wadogo wadogo na katika nyaraka yako ya kuomba zabuni iwepo ili ufanikiwa angalau asilimia 20 au 10 ya nguzo iwe inatoka kwa wadau wadogo na wawe wamepewa mikataba inayoeleweka” alisema Makamba

Makamba amewataka Wadau hao kuunda chama Cha wazalishaji wa nguzo ili kiweze kudhibiti ubora unaotakiwa na hata kutoa adhabu kali kwa atakayebainika kuzalisha chini ya Kiwango pamoja na kuandaa sheria zitakazoongoza chama hicho.



“Lengo la Serikali ni kukuza uchumi wa wananchi wake kwa kuboresha bidhaa zao kwa kuwasimamia katika kuzalisha kwa vigezo na ubora uliowekwa, ili wananchi hao waweze kunufaika na kukuza uchumi wao na pato la Taifa kwa ujumla” Alisema Makamba.

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Maharagwe Change, aliwataka Wadau hao kuwa waaminifu pale nguzo zao zinapotakiwa kupelekwa katika maeneo ya miradi kwa kuweka nguzo halisi zilizokaguliwa na siyo kufanya udanganyifu wa kuweka zisizokuwa na ubora.

Amesema kumekuwa na changamoto ya nguzo kuharibika baada ya muda mfupi kutumika kutokana na kuwa chini ya kiwango na ubora unaotakiwa, huku nguzo hizo zikiwa tayari zimekaguliwa na kuonekana zina ubora unaotakiwa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Said, amewahakikishia Wadau hao kuwa soko la nguzo lipo la kutosha kwani bado miradi mingi ya usambazaji wa Umeme vijijini inaendelea na nguzo nyingi zinahitajika.

Akitoa mfano Mkoa wa Iringa kuwa kuna Mradi wa Ujazilizi ambao unatarajia kuanza hivi karibuni katika Mkoa huo na mikoa mingine.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Queen Sendiga amewapongeza wabunge wa Mkoa wa Iringa Kwa kuwa wamoja Katika kutetea ajenda za kimaendeleo zinazohusu Mkoa wa Iringa. 

Alisema kuwa umoja ambao wameonesha kwenye kupigania suala la nguzo za Umeme kuendelea  kununuliwa hapa hapa Nchini wamefanya Jambo la kizalendo sana kwani linaenda kuongeza mapato kwa serikali na Wananchi kwa ujumla. Vivyo hivyo amewataka kuendelea  kufanya hivyo kwenye ajenda nyingine za ki mkoa .

Sendiga Alisema kuwa  Mkoa wa Iringa na Njombe ndio ambao wameuza nguzo zaidi ya asilimia 90 zilizotumika kusambaza Umeme nchini na walishangazwa kusikia hoja ya kuwa nguzo za ndani sio bora wakati tayari nguzo nyingi zimesimikwa Vijijini na zipo imara

"Tukushukuru Mheshimiwa Waziri wa Nishati kwa kufanya maamuzi haya ambayo yana Afya kubwa Kwa uchumi wa mikoa hii miwili na Taifa"

Amewataka Wadau hao kutoa ushirikiano kwa mamlaka husika na kuwa wasikivu kwa kile watakachokuwa wakielezwa kwa lengo la kupata bidhaa Bora kwa manufaa yao na taifa kwa jumla.

Sendiga alisema kuwa baada ya suala la nguzo kumalizika wabunge hao wana wajibu wa kuendelea kusukuma ajenda ya Mkoa wa Iringa ya ujenzi wa barabara ya kiwango cha Lami toka Iringa hadi Ruaha Kwa ajili ya kuchochea kasi ya utalii ndani ya hifadhi ya Taifa ya Ruaha




 

RC SENDIGA ATOA SIKU SABA KWA MKANDARASI PRIPAM KURUDIA UPYA UJENZI WA BARABARA YA ZIZILANG’OMBE NGEREWALA


Mkuu wa mkoa wa Iringa Queen Sendiga akiwa kwenye ukaguzi wa barabara zaTARURA manispaa ya Iringa
Barabara ambazo mkuu wa mkoa wa Iringa alikuwa analalamikia kuwa zimejengwa chini ya kiwango
Barabara ambazo mkuu wa mkoa wa Iringa alikuwa analalamikia kuwa zimejengwa chini ya kiwango

Mkuu wa mkoa wa Iringa Queen Sendiga akiwa kwenye ukaguzi wa barabara zaTARURA manispaa ya Iringa

 Na Fredy Mgunda, Iringa.

 

Mkuu wa mkoa wa Iringa ametoa siku saba kwa mkandarasi Pripam kurudia upya ujenzi wa barabara ya Zizilang’ombe Ngelewala kwa kujenga chini ya kiwango na kusababisha barabara hiyo kuweka nyufa mwezi mmoja tu toka kukamilika kwake.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa barabara za TARURA Manispaa ya Iringa,mkuu wa mkoa Queen Sendiga alisema kuwa hawezi kufarahishwa hata kidogo akikuta barabara imejengwa chini ya kiwango tofauti na thamani ya fedha iliyotolewa kwa mkandarasi.

Sendiga alisema kuwa haiwezekani barabara nyingi za manispaa ya Iringa zimejengwa kwa kiwango kizuri ispokuwa baarabara ya Zizilang’ombe Kitasengwa kwa kuwa imeanza kupasuka mapema jambo ambalo linaashiria kuwa barabara hiyo imejengwa chini ya kiwango.

Aliwataka wataalam Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini wilaya ya Iringa kuhakikisha wanawasimamia vilivyo wakandarasi ambao wanakuwa wamepewa tenda za ujenzi wa barabara wanajenga kwa ubora unaotakiwa kulingana na thamani ya fedha ambayo imetolewa kutoka serikalini.

Sendiga alisema kuwa baada ya siku saba atafanya ziara kukagua barabara hiyo kama imejengwa kwa kiwango kinachotakiwa kulingana na f thamani ya fedha ambayo imetolewa na serikali la sivyo mkandarasi atachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Sijaridhishwa na ujenzi wa barabara inayotoka Zizi la Ng'ombe kuelekea Ngelewala Manispaa ya Iringa.Nimetoa siku saba kwa mkandarasi kuijenga upya kwa gharama zake na katika ubora unaotakiwa.” Alisema Sendiga

Aliwaambia wataalam wa TARURA wilaya ya Iringa kufanya kazi kwa weredi unaotakiwa ili kuiondolea serikali sitofahamu inayokuwa inaendelea kwenye mitandao ya kijamii juu ya ubovu wa barabara zinazojengwa katika wilaya ya Iringa.

Sendiga alimalizia kwa kuwapongeza viongozi wa TARURA Iringa kwa kazi wanayoifanya isipokuwa mradi mmoja wa barabara ya Zizilang’ombe Ngelewala ambao umeweka doa la mkoa kwa video za nyufa za barabara hiyo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

 

Kwa upande wake meneja wa TARURA mkoa wa Iringa Makori George Kisare alisema kuwa wameyapokea mawazo na maagizo yote ya mkuu wa mkoa na watayafanyia kazi haraka ipasavyo kama alivyo agiza.

Akizungumzia swala la kupasuka kwa barabara ya Zizilang’ombe Ngelewala alisema kuwa mkandarasi anawajibu wa kurudia kwa gharama zake kwa kuwa yeye ndio aliyefanya kosa hilo la kiufundi.

 

Alisema kuwa watahakikisha wanamsimamia ndani ya siku hizo saba anafanya marekebisho yanayotakiwa kwenye barabara hiyo.

 


 
Copyright © 2016 Shamakala
Designed by Switch International | SHAMAKALA 360
    Twitter Facebook Google Plus Vimeo Videosmall Flickr YouTube