MSHAMBULIAJI wa timu ya Aston Villa inayoshiriki Premier League, Mtanzania, Mbwana Samatta amemhakikishia baba yake mzazi, mzee Ally Samatta kuwa atapambana kuhakikisha anainusuru timu yake isishuke daraja msimu huu.
Samatta ambaye amejiunga na timu hiyo katika usajili wa dirisha dogo msimu huu kwa mkataba wa miaka minne na nusu, ana kazi kubwa ya kuibakisha timu hiyo kutokana na kuwa kwenye nafasi mbaya ya 19 ikiwa na pointi 25 ikifuatiwa na Norwich City ambayo inaburuza mkia ikiwa na pointi 21.
Mzee Samatta alisema kuwa, kutokana na ligi kutarajiwa kurejea tena leo Juni 17, 2020, mtoto wake amemwambia atapambana kuinusuru timu hiyo kushuka daraja.
“Suala la ligi kurejea lipo wazi na kila mmoja amekuwa akilijua vizuri isipokuwa kijana amenieleza nia yake ni kutaka kuinusuru timu isishuke hivyo amepanga kucheza kwa kujituma zaidi ili kufikia malengo.
“Unajua wapo ambao walitaka ligi ifutwe kama zilizofanya nchi nyingine lakini England wao wameona ni bora kumalizia hivyo kila mmoja anatakiwa apambane na yeye ndiye amenieleza kwamba hatamani kuona wakishuka hivyo lazima ajitoe ili kuinusuru timu na msimu ujao waanze pamoja,” alisema mzee Samatta.